• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 5:50 AM
Jeremiah Kioni adai maajenti wa Azimio walifurushwa Mlima Kenya

Jeremiah Kioni adai maajenti wa Azimio walifurushwa Mlima Kenya

NA CHARLES WASONGA

KATIBU Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni sasa anadai kuwa maajenti wa mgombea urais wa Azimio la Umoja-One Kenya Raila Odinga walifurushwa kutoka vituo vya kupigia kura ili kutoa nafasi kwa ukora.

Akiongea na wanahabari Jumatano katika makao makuu ya chama hicho, jijini Nairobi, Bw Kioni alidai kuwa maajenti wa Jubilee pia walizuiwa kuingia katika vituo vya kupigia kura mnamo Agosti 9.

“Maajenti wetu wote walizimwa kuingia katika vituo vya kupigia kura ilhali wengine waliruhusiwa. Ilidaiwa kuwa barua zao za uajiri hazikuwa zimepigwa muhuri. Sababu sawa na hiyo ilitumiwa kuwazuia maajenti wa mgombea wetu wa urais Raila Odinga,” akawaambia wanahabari.

Madai ya Bw Kioni yanajiri siku kadhaa baada ya baadhi ya wafuasi wa Bw Odinga kulaumu wandani wake kwa kutowaajiri maajenti wa “kulinda” kura zake katika ng’ombe za Naibu Rais William Ruto za Mlima Kenya na Bonde la Ufa.

Inadaiwa kuwa kutokuwepo kwa maajenti wa Bw Odinga katika maeneo hayo ndiko kulitoa mwanya wa kukithiri kwa visa vya wizi wa kura na maovu mengine.

Bw Kioni, ambaye ni Mbunge anayeondoka wa Ndaragua, pia alidai kuwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ilipandisha kiwango cha watu waliojitokeza kupiga kura katika eneo la Mlima Kenya kuwa asilimia 55.

“Ukweli ni kwamba kiwango cha wapiga kura waliojitokeza kupiga kura katika eneo la Mlima Kenya kilikuwa asilimia 40 wala sio asilimia 55, ilivyodai IEBC,” akasema.

Bw Kioni pia alidai hongo ilitumika kuwashawishi wapiga kura wa Mlima Kenya wamgie kura “mgombea urais fulani.”

“Hii ndio maana wapiga kura waliruhusiwa kupiga kura karatasi zao za kupigia kura baada ya kuweka alama ili watume picha hizo kwa watu fulani ambao waliwalipa,” Katibu huyo mkuu alisema.

Hata hivyo, mwanasiasa huyo hakutoa ushahidi kuonyesha kuwa visa hivyo vilikuwa vikitendeka.

Aidha, hakusema iwapo yuko tayari kutoa madai hayo katika Mahakama ya Juu ambayo inasikiliza kesi ya kupinga ushindi wa Dkt Ruto.

  • Tags

You can share this post!

Gachagua asema ndiye wa kuaminiwa kutetea maslahi ya Mlima...

PSG yaponda Lille bila huruma katika pambano la Ligi Kuu ya...

T L