• Nairobi
  • Last Updated November 28th, 2023 7:53 PM
Gachagua asifu Azimio kwa kusitisha maandamano japo ‘mjeledi wa kuwanyorosha uko tu karibu’

Gachagua asifu Azimio kwa kusitisha maandamano japo ‘mjeledi wa kuwanyorosha uko tu karibu’

NA CHARLES WASONGA

NAIBU Rais Rigathi Gachagua ametoa kauli isiyo ya kawaida kwake kutoa kwa kuusifu mrengo wa Azimio la Umoja-One Kenya kwa kusitisha maandamano ya kuipinga serikali ya Kenya Kwanza.

Akiongea Jumamosi, Septemba 30, 2023, katika Kaunti ya Isiolo, Bw Gachagua alisema kuwa viongozi wa Azimio wamegeuka watu wazuri.

“Sheikh amesema ni makosa kwa mtu yeyote kutoa fujo na matamshi ya kusababisha uhasama. Wale tuliowashinda ndio walikuwa wanapenda kutoa fujo lakini siku hizi wamekoma na kugeuka watu wazuri,” akasema.

“Mheshimiwa Kiraitu Murungi amesema anaogopa huu mjeledi niliyopewa kama zawadi. Lakini huu mjeledi kazi yake imeisha kwa sababu watu wamekuwa wazuri, wameacha fujo. Wakijaribu kurudi tena kufanya maandamano nitatoa huu mjeledi na kuwacharaza nao,” Bw Gachagua akasema.

Alikuwa akirejelea mjeledi wa kitamaduni aliotunukiwa wakati wa sherehe ya kutoa shukrani iliyoandaliwa kwa heshima ya Katibu katika Wizara ya Kawi anayesimamia Idara ya Petroli Mohamed Liban.

Bw Gachagua alisema angetumia mjeledi huo kuwacharaza watu wanaoleta fujo lakini sasa hatafanya hivyo kwa sababu viongozi wa Azimio walisitisha maandamano.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa hatasita kutumia mjeledi huo endapo wafuasi wa upinzani watarejelea maandamano.

Mrengo wa Azimio unaoongozwa na Raila Odinga ulisitisha maandamano ya kila wiki mnamo Julai na kukubali kushiriki mazungumzo ya maridhiano na mrengo tawala wa Kenya Kwanza, kupitia Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo (NADCO).

Vikao vya kamati hiyo vinafanyika katika ukumbi wa Bomas of Kenya chini ya uenyekiti wa Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka (Azimio) na Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wah.

Kwa muda wa wiki moja sasa kamati hiyo, inayosaidiwa na kamati ya kiufundi na kisheria, imekuwa ikikusanya maoni na mapendekezo kutoka kwa wadau mbalimbali kuhusu namna ya kukomesha changamoto mbalimbali zinazolikumba Kenya wakati huu.

Changamoto hizo zinahusiana na masuala kama vile kupanda kwa gharama ya maisha, utata katika uchaguzi wa urais, uteuzi wa makamishna wapya wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) miongoni mwa masuala mengine.

  • Tags

You can share this post!

Arsenal moto balaa, Manchester machozi!

Pasta amuumbua mkewe hadharani, waumini wabaki na alama ya...

T L