• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 8:50 AM
Arsenal moto balaa, Manchester machozi!

Arsenal moto balaa, Manchester machozi!

NA MASHIRIKA

WOLVERHAMPTON Wanderers walipiga Manchester City breki kali katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa kuwapokeza kichapo cha 2-1 ugani Molineux, mnamo Jumamosi.

Mabingwa hao watetezi wa EPL walikubali kung’atwa na mbwa-mwitu hao, siku tatu baada ya Newcastle United kuwadengua kwenye raundi ya tatu ya kombe la Carabao EFL 1-0 uwanjani St James’ Park.

Wolves walianza mechi kwa matao ya juu na wakawekwa kifua mbele na beki Ruben Dias aliyejifunga kunako dakika ya 13.

Ingawa Julian Alvarez alirejesha Man-City mchezoni katika dakika ya 58, chombo cha miamba hao kilizamishwa kabisa na Hwang-hee Chan kunako dakika ya 66.

Chini ya kocha Pep Guardiola, Man-City walipoteza fursa ya kuweka rekodi ya kushinda mechi saba mfululizo za ufunguzi wa msimu wa EPL kwa mara ya kwanza katika historia.

Crystal Palace nao walilipiza kisasi dhidi ya Manchester United kwa kusajili ushindi wa 1-0 uwanjani Old Trafford huku Arsenal wakikomoa Bournemouth 4-0 ugani Vitality.

Man-United walijitosa ulingoni wakijivunia kukomoa Palace 3-0 katika EFL Cup mnamo Jumanne na kujikatia tiketi ya kuvaana na Newcastle katika raundi ya nne.

Aston Villa walipokeza wageni Brighton kichapo kinono cha 6-1 nyumbani Villa Park.

Wenyeji Newcastle United wakacharaza Burnley 2-0 katika uga wa St James’ Park.

Ilikuwa siku nzuri pia kwa wenyeji West Ham waliokung’uta Sheffield United 2-0 jijini London.

Hata hivyo, wenyeji wengine Everton walinyukwa 2-1 na limbukeni Luton Town ugani Goodison Park.

Sawa na Wolves waliotandikwa 3-2 na Ipswich Town katika EFL Cup ugenini mnamo Jumanne, Man-City pia walishuka dimbani wakiwa na kiu ya kujinyanyua.

Wafalme hao mara saba wa EPL sasa wanajivunia alama 18 kutokana na mechi saba.

Pengo la pointi 11 linawatenganisha na Wolves, walioshuka ulingoni wakiwa wamepoteza mechi nne mfululizo katika mashindano yote.

Ushindi wa Jumamosi unamaanisha Wolves walikwepa kupoteza mechi tatu mfululizo za ufunguzi wa msimu wa EPL uwanjani Molineux kwa mara ya kwanza tangu 1986-87.

Kwa kuangusha Bournemouth, Arsenal waliendeleza ubabe uliowavunia ushindi wa 1-0 dhidi ya Brentford katika EFL Cup ugani Gtech Community, Jumatano.

Winga Bukayo Saka alifungulia wanabunduki ukurasa wa mabao kabla nahodha Martin Odegaard na kiungo mshambuliaji Kai Havertz kupachika penalti kisha Ben White kufunga goli la nne.

Sasa wana pointi 17 ligini huku pengo la alama 14 likiwatenganisha na Bournemouth.

MATOKEO YA EPL (Jumamosi):

Aston Villa 6-1 Brighton

Bournemouth 0-4 Arsenal

Everton 1-2 Luton Town

Man-United 0-1 Crystal Palace

Newcastle 2-0 Burnley

West Ham 2-0 Sheffield Utd

Wolves 2-1 Man-City

RATIBA (Jumapili):

Nottm Forest vs Brentford (4:00pm)

Jumatatu:

Fulham vs Chelsea (10:00pm)

  • Tags

You can share this post!

KNUT yasema haiwezi kumtetea mwalimu wa kuwataka watoto wa...

Gachagua asifu Azimio kwa kusitisha maandamano japo...

T L