• Nairobi
  • Last Updated May 9th, 2024 6:50 AM
Gusa Uhuru uone, Raila aonya Ruto

Gusa Uhuru uone, Raila aonya Ruto

NA WANDERI KAMAU

VIONGOZI wa muungano wa Azimio la Umoja jana Jumapili walimuonya Rais William Ruto na uongozi wa serikali ya Kenya Kwanza dhidi ya ‘kumdhuru’ Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta kwa namna yoyote ile.

Viongozi hao waliapa kufanya kila wawezalo kumlinda na kumtetea Bw Kenyatta, wakisema kuwa wamechoshwa na mtindo wa Rais Ruto na washirika wake kuendelea “kumkosea heshima” rais huyo mstaafu na familia yake.

Wakihutubu kwenye mkutano wa muungano huo katika uwanja wa Kamukunji, eneo la Kibera, Kaunti ya Nairobi, viongozi hao walimwambia Rais Ruto kushughulikia changamoto zinazoikumba nchi badala ya kuelekeza ghadhabu zake kwa Bw Kenyatta.

“Wewe (Ruto) shughulikia changamoto zinazoikumba nchi. Achana na Uhuru Kenyatta! Huyu ni kiongozi anayefaa kuheshimiwa. Achana naye! Jaribu kumgusa!” akasema aliyekuwa Waziri wa Ulinzi, Eugene Wamalwa.

Bw Wamalwa alisema kuwa wako tayari kumtetea Bw Kenyatta bila kumwogopa Rais Ruto na “vitisho” kutoka kwa serikali yake.

“Tungependa kumwambia Ruto kuwa katika enzi ya marehemu Jaramogi Oginga Odinga na Masinde Muliro katika miaka ya tisini, tulifanikiwa kumshinikiza Rais Mstaafu (marehemu) Daniel arap Moi kuanzisha mfumo wa vyama vingi vya kisiasa kupitia chama cha Ford. Ikiwa tuliweza kumkabili Moi na udhalimu wake, wewe (Ruto) huwezi kututisha hata kidogo,” akasema Bw Wamalwa.

Kauli yake iliungwa mkono na Katibu Mkuu wa chama cha Jubilee, Bw Jeremiah Kioni, aliyesema kuwa wako tayari kumtetea Bw Kenyatta kwa njia yoyote ile.

“Mnamo 2003, Rais Ruto alisema alikuwa tayari kumtetea Mzee Moi, hata ikiwa hilo lingemaanisha kupoteza uhai wake. Vivyo hivyo, ninamwambia ajaribu kumgusa Uhuru; pengine afanikiwe tukiwa hatuko hai. Tutafanya kila tuwezalo kumlinda na kumtetea kama kiongozi wetu,” akasema Bw Kioni, aliyehudumu kama mbunge wa Ndaragwa.

Viongozi hao waliutaja utawala wa serikali ya Kenya Kwanza kama ulioshindwa kutekeleza majukumu yake, ukisisitiza kuwa badala ya kushughulikia changamoto zinazowakumba Wakenya, Rais Ruto na washirika wake wameanza kutumia taasisi za umma kuhangaisha wakosoaji wao.

“Binafsi, nimepokea vitisho kutokana na msimamo wangu. Hata hivyo, siogopi lolote. Ningeoenda kumwambia Rais Ruto na washirika wake kutahadhari kwani, viongozi wengi waliong’olewa mamlakani kupitia maasi ya raia, walianza kuchukua mwelekeo anaochukua,” akasema mbunge Babu Owino (Embakasi).

Mzozo baina ya serikali na familia ya Bw Kenyatta ulianza wiki iliyopita, baada ya Rais Ruto na Naibu Rais Rigathi Gachagua kudai kuwa kuna watu maarufu na wenye ushawishi ambao wamekuwa wakikwepa kulipa ushuru.

Baadaye, maseneta kadhaa wa Kenya Kwanza walidai kuwa na “habari za kijasusi” kwamba mbali na kutolipa ushuru, Rais Kenyatta ndiye amekuwa akifadhili mikutano inayoendeshwa na mrengo wa Azimio.

“Tuna maelezo ya kutosha yanayoonyesha kuwa Bw Kenyatta ndiye anayefadhili mikutano hiyo ya Azimio ili kukwepa kuagizwa kulipa ushuru. Wito wetu kwa Bw Kenyatta ni kuwa anafaa kulipa ushuru kama Wakenya wengine. Huenda hata tukaiagiza Halmashauri ya Kukusanya Ushuru Kenya (KRA) kufanya ukaguzi kubaini kiwango cha ushuru ambacho familia ya Bw Kenyatta haijalipa,” akasema Seneta John Methu (Nyandarua).

Wakati huo huo, viongozi wa Azimio jana Jumapili walitangaza kuanzisha vuguvugu jipya la Movement for the Defence of Democracy (MDD) ili “kuwahamasisha raia na kuishinikiza serikali kutimiza ahadi ilizotoa kwa wananchi”.

Katibu Mkuu wa ODM, Edwin Sifuna, alisema kuwa vuguvugu hilo litakuwa kama jukwaa la Azimio kuanza maasi yake makali dhidi ya utawala wa Rais Ruto kwa “kuwasaliti raia.”

  • Tags

You can share this post!

TUSIJE TUKASAHAU: Walimu wakuu bado wameorodhesha ada...

Utata wazidi kukumba Sekondari ya Msingi

T L