• Nairobi
  • Last Updated December 2nd, 2023 1:45 PM
Hatuingii Azimio bila Kalonzo, asisitiza Moi

Hatuingii Azimio bila Kalonzo, asisitiza Moi

NA CECIL ODONGO

MWENYEKITI wa chama cha Kanu, Gideon Moi amesema kwamba, chama hicho hakina mpango wa kujiondoa katika muungano wa One Kenya Alliance (OKA), licha ya shinikizo zinazoendelea amteme kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka na kujiunga na Azimio la Umoja.

Bw Moi alipuuzilia mbali taarifa za vyombo vya habari kuwa chama hicho kinaelekea kujiunga na vuguvugu la Azimio akisema pande zote bado zinaendelea na mazungumzo lakini hakuna muafaka umeafikiwa.

“Tungependa kufafanua kuwa chama hiki kiko ndani ya OKA na kinashauriana na vyama vingine tanzu kuhusu ushirikiano wetu na vuguvugu la Azimio,” ikasema taarifa ya Kanu iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi wake, George Wainaina.

“Ningependa kuweka wazi kuwa, chama hiki bado kipo ndani ya OKA japo kuna mazungumzo yanayoendelea na vuguvugu la Azimio. Kama vyama ndani ya OKA tumechukua msimamo kuhusu suala hili ili majadiliano yetu na Azimio yafuate utaratibu, mkondo wa sheria na uwe wenye uwazi,” ikasema taarifa ya Bw Wainaina.

Kwenye taarifa hiyo, Kanu ilisema kauli ya Katibu Mkuu Nick Salat kuwa chama kitahudhuria Kongamano la Kitaifa la Wajumbe wa Azimio (NDC) mnamo Jumamosi, ilikuwa yake binafsi.

“Kauli hiyo haifai kufasiriwa kuwa msimamo wa chama,” ikaongeza taarifa ya Bw Wainaina.

Mnamo Jumatano wakati wa kuzindua Manifesto ya Kanu, Bw Salat alisema chama hicho kilikuwa kimechoka kumbembeleza kinara wa Wiper, Kalonzo Musyoka ili wote waelekee Azimio kwa pamoja.

Bw Salat alilalamika kuwa Bw Musyoka alikuwa akichukua muda mrefu sana kabla ya kuamua iwapo atajiunga na Azimio la Umoja au la.

You can share this post!

Wanaoshukiwa kuvamia mwanamke kukaa kizuizini siku 15

Ulawiti: Mwalimu aachiliwa korti ikikosa ushahidi

T L