• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:55 AM
IEBC: Maswali zaidi yachipuka kuhusu kampuni

IEBC: Maswali zaidi yachipuka kuhusu kampuni

JUMA NAMLOLA Na BRIAN WASUNA

MWENYEKITI wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati aliendelea kujikoroga zaidi usiku wa Jumatatu, huku uchunguzi wa Taifa Leo ukionyesha kampuni iliyopewa kandarasi haina afisi nchini.

Bw Chebukati alisambaza barua mitandaoni kuanzia saa sita za usiku, na jana akachapisha tangazo magazetini kujaribu kueleza kuhusu kisa ambapo, raia wa Venezuela alikamatwa katika uwanja wa ndege akiwa na vibandiko vya uchaguzi ndani ya mkoba wake wa kibinafsi.

Kwenye majibu yake aliyoyaweka kwa nambari, jibu la tano ni kuwa kampuni ya Smartmatic iliyopewa kandarasi ilitakiwa kuwa na mshirika au ofisi nchini Kenya.

Mshirika huyo ni kampuni inayojulikana kama Seamless Technologies.

Upekuzi wa Taifa Leo kwenye nyaraka za msajili wa kampuni, unaonyesha kuwa Seamless International ilianzishwa na Muna Mohamed na Hashim Ahmed Hussein mwaka 2010, kila mmoja akimiliki asilimia 50.

Wawili hao baadaye walimwajiri wakili Maria Goretti Nyariki, kuwa katibu wa Seamless Limited. Bi Nyariki baadaye alipanda ngazi na kuwa msajili wa vyama nchini.

Ingawa Seamless Technologies inaonyeshwa kuwa na anwani eneo la Eastleigh, Nairobi, inaendesha shughuli zake katika eneo ambapo watu hukodisha sehemu za kuendeleza kazi zao kwenye barabara ya Dennis Pritt, Hurlingham.

Seamless Technologies inaendesha shughuli zake katika jumba la iHit, eneo linalofadhiliwa na serikali ya Iran, ambapo Wakenya walio na maarifa ya uvumbuzi husaidiwa na wataalamu wa nchi hiyo kutoka Uarabuni.

Juhudi za Taifa Leo kuingia ndani ya iHit jana Jumanne hazikufanikiwa, baada ya maafisa wa usalama kusema mameneja wachache waliokuwa walikuwa katika mkutano wa siku nzima. Wengine walikuwa wamesharejea katika ubalozi wa Iran.

iHit ni eneo ambalo walio na maarifa ya uvumbuzi hukodisha maeneo ya kufanyia shughuli zao kwa malipo nafuu, kinyume kama wangekuwa wakikodisha afisi.

Ukodishaji huu huwa wa kwa muda mfupi, ikiwa na maana kuwa wahusika huwa hawana afisi maalumu ambapo mtu anaweza kuwapata wakitoka hapo.

Cha kushangaza kulingana na kauli ya Bw Chebukati, Seamless Technologies ndio maajenti wa kampuni ya Smartmatic, iliyopewa kandarasi ya kusambaza vifaa vya kuendesha uchaguzi wa Agosti 9.

Kampuni hiyo ya Smartmatic yenyewe inamilikiwa na raia wa Venezuela lakini ikasajiliwa Uholanzi huku makao yake makuu yakiwa jijini London, Uingereza.

Jumanne, kwenye tangazo lake, Bw Chebukati alichapisha maelezo kuhusu Smartmatic aliyoyatoa kwenye mtandao wake, ambayo inaonyesha kuwa ilianzishwa katika jimbo la Florida nchini Marekani mwaka 2000.

Kampuni hiyo ilipewa kandarasi ya Sh4 bilioni mnamo Novemba 2021, isambaze vifaa 14,100 vya KIEMS, vinavyotumika kuwatambua wapiga kura.

Vifaa hivyo, vinapaswa kuwa na vibandiko vya kuvitambua wakati wa kuvisambaza katika vituo vya kupigia kura.

“Ni muhimu kusema kuwa, vibandiko hivyo si muhimu sana kwa uchaguzi,” akasema Bw Chebukati jana Jumanne, bila kujibu maswali yaliyoibuliwa na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI), Bw George Kinoti.

You can share this post!

Tusker yatoa masharti kuachilia kipa Matasi

Ndoto zao zilizimwa ghafla barabarani

T L