• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 6:50 AM
Ndoto zao zilizimwa ghafla barabarani

Ndoto zao zilizimwa ghafla barabarani

NA WAANDISHI WETU

MNAMO 2020, Mary Mwandisha, 28, alikuwa miongoni mwa wanafunzi wa udaktari waliofanikiwa kufuzu kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi.

Kulingana na familia yake, Mary alikuwa na ari ya kutumikia jamii kwa vile wasamaria wema walichangia pakubwa kufadhili masomo yake, na hivyo basi akafanya juu chini kuhakikisha mafunzo yake yanakuwa kwa manufaa ya umma.

Mwanga wa heri ulianza kumulika matumaini yake alipofuzu kwenye mahojiano ya udaktari katika Hospitali ya Kaunti ya Taita Taveta, lakini hayo yote yakazimwa ghafla alipopoteza maisha kwenye ajali mbaya ya barabarani iliyohusisha basi la kampuni ya Modern Coast katika Mto Nithi, Jumapili.

Wakati wa ajali hiyo iliyosababisha vifo vya watu 34, alikuwa akielekea Voi kuchukua barua ya kuanza kazi.

“Nina uchungu mwingi sana moyoni. Wakati ulikuwa umewadia kwa mwanagu kuvuna matunda ya bidii yake. Alikuwa amepata kazi ya serikali halafu anaaga hata kabla ya kuchukua barua yenyewe,” alisema mamake, Bi Angeline Mwandisha.

Dkt Mary alikuwa mtoto wa nne wa Bw John Jilani na Bi Mwandisha.

Kufikia kifo chake, alikuwa amefanya kazi katika hospitali ya Lifetime iliyoko katika Kaunti ya Meru kwa miezi mitatu.

Akizungumza na wanahabari katika kijiji cha Kwa Mike mjini Kilifi, Bi Mwandisha, alieleza masikitiko makuu.

“Nilizungumza na msichana wangu Jumapili asubuhi aliponiambia kuwa angesafiri kuelekea Voi kuchukua barua ya kazi. Alipaswa kurejea Meru Jumatatu usiku. Alinieleza kuwa angenitumia ujumbe pindi tu atakapofika,” akasema.

Mamake mwendazake anaeleza kuwa kuchelewa kwa arafa kutoka kwa mwanawe kulimtia wasiwasi.

“Niliamka saa kumi na moja asubuhi na nikamtumia ujumbe wa kumtakia safari njema iwapo hakuwa amefika. Licha ya hayo sikuweza kupata usingizi. Nilipiga simu zake mbili ila ilikuwa imezimika. Hapo wasiwasi ukazidi na nikashindwa hata kulala tena,” alieleza.

Nduguye, Bw Marsden Mwandisha, alieleza kuwa ripoti za kuwa dada yao alikuwa ameaga ziliwafikia kupitia jamaa zao wanaoishi Nairobi.

“Tulienda hadi kwenye afisi za kukatia tikiti za kampuni ya Modern Coast na tukafahamishwa alikuwa amekata tikiti ya kiti nambari mbili. Baadaye tulipigiwa simu na wafanyakazi wenzake walio Meru waliothibitisha kifo chake,” alisema nduguye.

Mwili wa Dkt Mwandisha umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhi maiti cha Lee jijini Nairobi. Atazikwa katika kijiji cha Shelemba katika kaunti ya Taita- Taveta.

Kwa familia za Nicholas Ariyo na Agnes Kawira, ajali hiyo ni pigo kuu kwa mipango ya wawili hao kuanzisha familia pamoja.

Wapenzi hao wawili walikuwa wanarejea Mombasa kutoka Meru ambapo Nicholas na jamaa zake walikuwa wameenda kukutana na familia ya Agnes kushauriana kuhusu masuala ya mahari.

Katika basi hilo la mauti, kulikuwa pia na babake Nicholas, Bw James Otieno, na kakake mkubwa, Bw John Ochieng’, ambao walilazwa hospitalini wakiwa na majeraha.

“Walikutana miezi michache iliyopita, wakapendana na walikuwa wamepanga kuoana hivi karibuni,” jamaa wao, Bw James Oloo, akasema.

Walikuwa wanaishi katika mtaa wa Magongo, Kaunti ya Mombasa.

Familia ya Jane Karambu Mwithimbu, ilikuwa bado inaomboleza kifo cha kakake, Edward Mwithimbu, wakati Karambu, mkazi wa Mombasa, alipokufa katika ajali hiyo. Karambu alikuwa ametoka Meru kwa mazishi ya kakake.

  • Tags

You can share this post!

IEBC: Maswali zaidi yachipuka kuhusu kampuni

Sababu za Raila kukunja mkia

T L