• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 7:50 AM
Tusker yatoa masharti kuachilia kipa Matasi

Tusker yatoa masharti kuachilia kipa Matasi

NA CECIL ODONGO

UTATA mkubwa umezuka kati ya mabingwa wa Ligi Kuu (KPL) Tusker na Kenya Police kuhusu uhamisho wa mnyakaji wa Harambee Stars Patrick Matasi.

Kenya Police inataka kumpa kipa huyo ajira hatua ambayo inafasiriwa na Tusker kuwa kipa huyo huenda akajiunga na kikosi cha soka cha walinda usalama hao.

Kwa hivyo, wameshikilia kuwa Matasi ni mchezaji wao na Kenya Police lazima itoe kitita kikubwa kulingana na mkataba wake kabla wamruhusu ajiunge na idara ya polisi.

Katika mahojiano na Taifa Spoti, Matasi alikiri kuwa amepokea barua ya kujiunga na Idara ya Polisi Nchini lakini kizungumkuti ni Tusker kumkwamilia na kiwango cha fedha ambacho kinadaiwa kabla yake kuruhusiwa kuhama.

“Ndiyo nimepata barua ya kujiunga Idara ya Polisi Nchini lakini bado kuna vuta ni kuvute kwa sababu Tusker wanasitasita kuniachilia. Hata hivyo, nitaendelea kusukuma kwa sababu hii ni kazi na kuna maisha baada ya mpira,” akasema mnyakaji huyo mwenye umri wa miaka 34.

“Tusker inataka polisi iwalipe ndio nitoke lakini bado hakuna muafaka. Binafsi ningependa kujiunga na idara ya Kenya Police kwa sababu za kikazi nao umri wangu pia unasonga,” akasema Matasi.

Tayari mwanadimba huyo amegomea mazoezi na mabingwa hao mara 13 wa KPL kama mbinu ya kusukuma aelekee Kenya Police.

Kocha wa timu hiyo Robert Matano tayari ameanzisha mazoezi na wachezaji wengine.

Alipofikiwa, Afisa Mkuu Mtendaji wa Kenya Police Chris Mmbwanga alisema kuwa idara hiyo inataka kumpa Matasi kazi lakini huo ni uamuzi wake binafsi na mwenyewe aafikiane na Tusker.

“Tuna makipa watatu bora katika kikosi chetu. Matasi ni mnyakaji bora pia na amepokea barua ya kujiunga na Idara ya Polisi (NPS) kwa hivyo, suala la kujiunga na idara hiyo ni yake mwenyewe na Tusker,” akasema Onguso.

Matasi alijiunga na Tusker mnamo Agosti mwaka jana kama mchezaji huru na aliridhisha kiasi kuwa mwishoni mwa msimu, aliibuka kipa bora na kuwaongoza mabingwa hao kutwaa Ligi ya KPL.

You can share this post!

TUSIJE TUKASAHAU: Dkt Ruto akifanikiwa ajenge mabwawa ya...

IEBC: Maswali zaidi yachipuka kuhusu kampuni

T L