• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Ipsos: Raila kifua mbele huku zikisalia siku 6

Ipsos: Raila kifua mbele huku zikisalia siku 6

NA CHARLES WASONGA

MGOMBEA urais wa muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya Raila Odinga yuko kifua mbele dhidi ya mwenzake wa Kenya Kwanza Dkt William Ruto, kulingana na matokeo ya kura ya maoni yaliyotolewa Jumanne, Agosti 2, 2022.

Kulingana na utafiti huo uliofanywa na kampuni ya Ipsos, asilimia 47 ya wapiga kura waliohojiwa kote nchini walisema watampigia kura Bw Odinga.

Kwa upande mwingine asilimilia 41 ya wapiga kura hao walisema kuwa watamuunga mkono Dkt Ruto ambaye pia ndiye Naibu Rais katika serikali ya sasa.

Mgombea urais wa chama cha Roots naye ana uungwaji mkono kutoka kwa asilimia 2.9 ya wapiga kura huku David Mwaure Waihiga ikitarajiwa atapigiwa kura na asilimia 0.2 ya wapiga kura.

Asilimia 5.1 ya waliofikiwa katika utafiti huo walikataa kusema ni mgombea urais yupi watampigia kura ilhali asimilia 3.8 kati yao walisema hawajafanya uamuzi kuhusu yule ambaye watampigia kura.

Kulingana na Afisa wa Masuala ya Umma katika kampuni hiyo ya Ipsos Sam Muthoka, jumla ya watu 6,105 walihojiwa katika utafiti huo kutoka kaunti zote 47 ndani ya kipindi cha wiki moja iliyopita.

“Mahojiano yaliendeshwa kwa njia ya ana kwa ana na waliohojiwa ni wale ambao wamesajiliwa kuwa wapiga kura pekee,” Bw Muthoka akawaambia wanahabari katika mkahawa wa Serena, Nairobi.

Matokeo ya utafiti huo yanaonyesha kuwa Bw Odinga ana uungwaji mkono mkubwa katika kaunti 18 ambapo asilimia 55 ya wapiga kura walisema watampigia kura Agosti 9.

Kwa upande mwingine Dkt Ruto ana ushawishi mkubwa katika kaunti 17, sawa na asilimia 55.

Jumla ya kaunti 11 zinaonekana kama ambazo zitashuhudia ushindani mkubwa kati ya wagombea urais hawa wakuu.

Afisa wa Masuala ya Umma katika kampuni ya Ipsos Sam Muthoka akitangaza matokeo ya kura ya maoni katika mkahawa wa Serena, Nairobi, Agosti 2, 2022

  • Tags

You can share this post!

Mnikumbuke wiki ijayo, Raila asihi

Ruto asihi ngome yake kuwakataa wawaniaji wasio wa chama...

T L