• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
JAMVI: Dalili mwafaka umepatikana Mlimani kuhusu kura ya 2022

JAMVI: Dalili mwafaka umepatikana Mlimani kuhusu kura ya 2022

Na WANDERI KAMAU

KAULI za magavana Francis Kimemia (Nyandarua) na Kiraitu Murungi (Meru) kuwa ukanda wa Mlima Kenya utakuwa na mgombea urais mmoja kwenye uchaguzi mkuu wa 2022 zimeibua juhudi za kuondoa tofauti ambazo zimekuwa zikishuhudiwa katika eneo hilo.

Kumekuwa na tofauti kali za kisiasa kati ya ukanda wa Mlima Kenya Mashariki na Mashariki kuhusu yule anayepaswa kuwa mrithi wa Rais Uhuru Kenyatta atakapong’atuka uongozini mwaka 2022.

Mlima Kenya Mashariki inazishirikisha kaunti za Meru, Embu na Tharaka-Nithi, huku Magharibi ikizishirikisha kaunti za Nyeri, Nyandarua, Kirinyaga, Kiambu, Murang’a, Nakuru na Laikipia.

Mashariki imekuwa ikilaumu Magharibi kwa “kujipenda kisiasa” tangu uhuru, kwani viongozi wengi ambao wamekuwa wakitwa uongozi wanatoka katika eneo la Kati, linaloishirikisha jamii ya Agikuyu.

Mashariki inazishirikisha jamii za Ameru, Aembu na Mbeere.

Kwenye uzinduzi wa wasifu wa Bw Murungi katika hoteli moja jijini Nairobi Jumanne, magavana hao walisisitiza kuwa lazima Mlima Kenya iwe na mgombea mmoja wa urais “kutokana na idadi kubwa ya wapigakura wake.”

“Lazima tuwe na mtu atakayetuwakilisha katika ngazi ya kitaifa, wakati maeneo mengine yatakapokuwa yakijadili kuhusu taratibu za kugawana uongozi wa nchi,” akasema Bw Kimemia.

Ni kauli iliyoungwa mkono na Bw Murungi, ambaye amekuwa katika mstari wa mbele kusisitiza kuwa lazima Magharibi “warudishe mkono kwa kumuunga mkono mmoja wa viongozi kutoka Mashariki kuwania urais.”

Ikizingatiwa wawili hao ni mwenyekiti na naibu mwenyekiti wa Muungano wa Kiuchumi wa Kaunti za Eneo la Kati (CEREB) mtawalia, wadadisi wanasema kauli zao zinapaswa kuchukuliwa kwa uzito.

Kulingana na Bw Kiprotich Mutai, ambaye ni mdadisi wa siasa, kauli zao zinaonyesha kuwa kuna dalili kwamba kuna mwafaka ambao umefikiwa na pande hizo mbili kuwa na mwaniaji mmoja wa urais, ili kuondoa tofauti ambazo zimekuwa zikishuhudiwa miongoni mwa viongozi.

Kufikia sasa, baadhi ya viongozi kutoka eneo hilo ambao wameonyesha nia ya kuwania urais ni aliyekuwa gavana wa Kiambu, Bw William Kabogo, magavana Anne Waiguru (Kirinyaga), Mwangi wa Iria (Murang’a), mwanasiasa Peter Kenneth, Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi kati ya wengine.

Viongozi wa Mashariki wamekuwa wakimpigia debe Bw Muturi, baada ya kutawazwa rasmi na baadhi ya viongozi na wazee mwezi uliopita kuwa msemaji rasmi wa kisiasa katika ukanda wa Mlima Kenya.

ASILI

Hafla hiyo ilifanyika katika eneo la kitamaduni la jamii ya Agikuyu, Mukurwe wa Nyagathanga, Kaunti ya Murang’a, ambako inaaminika ndiko asili ya jamii hiyo.

Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa Kati walijitokeza kuikashifu hafla hiyo, wakiitaja “kukiuka taratibu za kitamaduni za jamii ya Agikuyu katika kumtawaza kiongozi ama msemaji wake.”

“Mwafaka ulioonekana kuwepo kati ya magavana hao wawili uliashiria taswira kuhusu juhudi za kuwapatanisha viongozi ambao wamekuwa wakifarakana kuhusiana na hatua ya Bw Muturi kutangaza azma ya kuwania urais. Kiundani, wao ni wawakilishi wa Magharibi na Mashariki, hivyo kauli zao zinonyesha kuwa kuna juhudi zinazoendelea kuondoa tofauti hizo,” asema Bw Mutai.

Kulingana naye, ikiwa mwelekeo huo umefikiwa, basi kuna uwezekano mkubwa kuwa huenda Bw Muturi ndiye amepata “baraka” hizo.

Anamtaja Bw Muturi kuwa kiongozi ambaye anaendelea kujitokeza wazi kuvumisha azma yake ikilinganishwa na vigogo wengine.

Majuzi, Bw Muturi aliashiria wazi atakuwa debeni kwenye uchaguzi wa 2022, na hatamwogopa yeyote.

“Natangaza rasmi nitakuwa debeni. Nafanya hivyo ili kuwaonyesha wapinzani wangu kuwa sina mchezo hata kidogo. Nishaanza harakati za kuwafikia wananchi katika maeneo mbalimbali nchini ili kuwaeleza ruwaza, maono na mipango yangu katika kuistawisha nchi,” akasema Bw Muturi.

Licha ya hayo, baadhi ya wadadisi wanasema kuwa licha ya mwafaka huo kupatikana, mwelekeo kamili utajulikana wakati Rais Kenyatta atajitokeza wazi na kutangaza kiongozi ambaye angempendelea kuwa mrithi wake.

“Ni mapema sana kueleza kuwa kuna mwafaka ambao umepatikana. Uongozi wa eneo hilo si jambo rahisi. Lazima pawe na majadiliano ya kutosha yatakayowashirikisha viongozi wote, hasa wale ambao tayari wametangaza azma za kuwania urais. Nahofia huenda migawanyiko zaidi ikaendelea kushuhudiwa ikiwa ushirikishi ufaao hautafanyika,” asema Bw Wycliffe Muga, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Hata hivyo, washirika wa Naibu Rais William Ruto wanasema kuwa ni wazi sasa eneo hilo limechoshwa na “uongozi wa kitabaka” na lipo tayari kuongozwa na “viongozi wanaotangamana na wananchi.”

“Enzi ambapo mikakati ya uongozi ilikuwa ikipangiwa kwenye mikahawa na majumba ya mikutano zimeisha. Wananchi wanawataka viongozi ambao watakuwa sehemu yao, kama ilivyodhihirika kwenye matokeo ya uchaguzi mdogo wa eneobunge la Kiambaa,” asema mbunge Ndindi Nyoro (Kiharu) ambaye ni mshirika wa karibu wa Dkt Ruto.

Sawa na washirika wengine, anashikilia kuwa wananchi ndio watakaojifanyia maamuzi huru bila kushurutishwa na yeyote.

You can share this post!

DINI: Ugumu wa maisha usikufanye upoteze imani au kulaumu...

Lucy Murigi aibuka mshindi wa mbio za kupanda mlima mita...