• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
JAMVI: Gavana Kingi aning’inia kisiasa Muungano wa Pwani ukijikokota

JAMVI: Gavana Kingi aning’inia kisiasa Muungano wa Pwani ukijikokota

?ANTHONY KITIMO na VALENTINE OBARA

HATIMA ya Gavana wa Kilifi Amason Kingi katika enzi ijayo ya kisiasa inaendelea kuning’inia huku mazungumzo ya kuleta umoja wa wanasiasa wa Pwani yakizidi kuchelewa kutamatika.

Licha ya joto la kisiasa kutanda katika kaunti hiyo kwa miezi kadhaa sasa, Bw Kingi aliyekuwa mstari wa mbele kupigania uundaji wa muungano wa Pwani kabla 2022 amejituliza tuli.

Wiki iliyopita, Bw Kingi hakuhudhuria mikutano ya Kiongozi wa ODM Raila Odinga katika kaunti hiyo licha ya kuwa yeye ndiye mwenyekiti wa chama hicho Kilifi.

Bw Kingi alionekana tu hadharani wakati Rais Uhuru Kenyatta alipozuru kaunti hiyo kukagua miradi ya maendeleo baadaye Alhamisi.

Bw Odinga hakuandamana na Rais kuelekea Kilifi jinsi imekuwa desturi yao kukagua miradi ya maendeleo wakiwa pamoja katika maeneo mengine nchini.

Hotuba nyingi zilizotolewa katika hafla ambazo Bw Odinga alihudhuria zililenga kuwasuta viongozi walioasi chama hicho cha nembo ya chungwa, huku kukiwa na sisitizo kwamba bado kina umaarufu Kilifi.

Kando na ODM, Chama cha United Democratic Alliance (UDA) kikiongozwa na Naibu Rais William Ruto pia kimekuwa kikiendeleza ziara nyingi katika kaunti hiyo kwa nia ya kufifisha umaarufu wa ODM kabla uchaguzi ujao.

“Mnafahamu vyema kuwa Kiifi ni ngome ya ODM. Watu wengi watasema watakavyo lakini mwishowe ODM ndiyo itavuma Pwani. Tunajua nani atakuwa Ikulu mwaka ujao na tuna imani atakuwa ni Raila Amolo Odinga,” alisema Seneta wa Kilifi, Bw Stewart Madzayo, alipokuwa akikashifu kampeni za mapema zinazoendelezwa na UDA.

Jumapili iliyopita, vyama vitano vya Pwani ambavyo Bw Kingi amekuwa akishinikiza viungane vilikutana mjini Voi, Kaunti ya Taita Taveta kuendelea kupanga mikakati yao.

Mikutano hiyo imekuwa ikifanyika kwa muda mrefu sasa ila uamuzi wa mwisho kuhusu mwelekeo utakaochukuliwa bado haujatolewa.

Vyama hivyo vya Shirikisho Party of Kenya (SPK), Kadu-Asili, Republican Congress Party of Kenya, Umoja Summit Party of Kenya (USPK) na Communist Party of Kenya vimeamua havitavunjwa kuunda chama kimoja bali vitaungana kuunda muungano wa vyama vya kisiasa vilivyo na mizizi yao Pwani.

Kwa msingi huu, huenda Bw Kingi atalazimika kuhamia mojawapo ya vyama hivyo ikiwa bado anaazimia kuendeleza juhudi za kuleta umoja wa Wapwani kisiasa ifikapo 2022.

Katika mahojiano na Taifa Jumapili, Katibu Mkuu wa Chama cha Shirikisho, Bw Adam Mbeto, alisema kufikia sasa uamuzi ambao umefanywa ni kuunda muungano wa vyama vya kisiasa ila uamuzi wa mwisho bado haujafanywa.

“Hatutakuwa na chama kimoja bali muungano wa vyama. Mazungumzo bado yanaendelea kuhusu suala hilo,” akasema Bw Mbeto kupitia kwa mahojiano ya simu Alhamisi iliyopita.

Bw Kingi ambaye ni mmoja wa magavana wa Pwani wanaotumikia kipindi cha pili ambacho ni cha mwisho cha ugavana hajakuwa wazi kuhusu maazimio yake ya baadaye kisiasa akilinganishwa na Gavana wa Mombasa Hassan Joho ambaye amekuwa akijiandaa kuwania urais.

Katika Kaunti ya Kwale, Gavana Mvurya ambaye ni mwanachama wa Jubilee pia amekuwa akielezea nia yake ya kujitosa katika siasa za kitaifa wakati atakapokamilisha kipindi chake cha ugavana mwaka ujao.

Bw Mbeto aliambia Taifa Jumapili kwamba vyama vitano vya Pwani sasa vimeunda kamati ambazo zitatoa mwelekeo wa kisiasa kwa Wapwani hivi karibuni.Imebainika kamati hizo ziko chini ya makundi ya Coast Initiative Development Initiative (CIDI) na Coast Political Parties’ Convention (CPPC) ambayo yatashauriana na kutoa mwongozo wa kiuchumi na kisiasa mtawalia utakaowanufaisha Wapwani.

Vile vile, imebainika kuwa mashauriano hayo yatalenga kutoa mwongozo wa jinsi muungano utafaa kuundwa ili kuunganisha manifesto ya vyama vyote tanzu bila kusababisha migogoro.

Miezi michache iliyopita, Bw Kingi alisuta viongozi wanaokashifu uundaji wa muungano wa vyama ambavyo vina mizizi Pwani kwa madai kuwa mpango huo ni wa kikabila.

Alisema vyama vinavyoendeleza mashauriano vimesajiliwa kama vyama vya kitaifa kwa hivyo vina uhuru wa kutafuta vingine kuunda nao muungano.

“Hakuna chama kinaundwa hapa, ni vyama vya kitaifa vimeundwa kisheria vinakuja pamoja kumiliki ngome yao. Kwa hivyo jambo hili lisichukuliwe kikabila,” alisema Bw Kingi.

Bw Joho ambaye pia ni naibu kiongozi wa ODM alisema Pwani itaendelea kuwa ngome ya kisiasa ya ODM na hakuna nafasi kwa chama kingine chochote, kiwe kipo tayari au kinatarajiwa kuundwa, kuchukua nafasi hiyo.

“Tumeona watu wakijaribu kupenya eneo la Pwani na kujaribu kuwashawishi wanachama wa ODM waondoke chamani. Nataka kuwaambia sisi hatulali na tutalinda wanachama wetu. Tumejifunza kutoka eneo la kati ambapo kuna watu waliohamia vyama vingine bila mpangilio,” akasema.

Alisisitiza kuwa chama hicho ndicho kitaunda serikali ijayo kwa hivyo haitakuwa busara kwa Wapwani kuanza kufikiria kuelekea kwingine wakati huu.

You can share this post!

Aliyejaribu kuua polisi kukaa gereza la viwandani

Ruto afaulu kunusuru UDA baada ya mzozo kutatuliwa