• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 12:04 PM
JAMVI: Kuna hatari ya Raila ‘kujikwaa’ kisiasa kwa kumtetea Rais

JAMVI: Kuna hatari ya Raila ‘kujikwaa’ kisiasa kwa kumtetea Rais

Na WANDERI KAMAU

KUMEIBUKA hofu huenda kutajwa kwa Rais Uhuru Kenyatta kuwa miongoni mwa watu walioficha mabilioni ya fedha ng’ambo kukaathiri mpango wake kumuunga mkono kiongozi wa ODM, Raila Odinga, kuwania urais 2022.

Rais Kenyatta alitajwa Jumatatu pamoja na jamaa zake kumiliki zaidi ya akaunti kumi na utajiri wa zaidi ya Sh3 bilioni katika akaunti fiche, kwenye ufichuzi unaoitwa ‘Pandora Papers.’

Wadadisi wanasema ingawa hilo halimaanishi Rais Kenyatta na familia yake walipora fedha hizo, kuna uwezekano ukatia doa juhudi za Rais kutangaza vita vikali dhidi ya ufisadi.

Vile vile, wameeleza hatua ya Bw Odinga kujitokeza wazi kumtetea Rais Kenyatta hadharani dhidi ya sakata hiyo itatia doa sifa yake kama mtetezi wa haki, uwajibikaji na ukweli.

Ijapokuwa viongozi na mashirika kadhaa ya kutetea umma yamejitokeza kumkashifu Rais, Bw Odinga alimtetea vikali Rais Kenyatta, akisema anapaswa kupewa nafasi kueleza ukweli kuhusu yale anayojua.

Kwenye mahojiano na vituo kadhaa vya redio Jumatano, Bw Odinga alisema “si makosa kwa Mkenya yeyote kuwa na akaunti fiche ughaibuni.”

“Sioni kosa, kwani kuna Wakenya wengi wenye akaunti hizo. Ningewaomba kujitokeza na kuzitangaza wazi. Imani yangu ni kuwa kama alivyoeleza Rais, ukweli kamili utajulikana,” akasema.

Sifa

Kutokana na kauli yake, wadadisi wa siasa wanaonya kwamba kuna uwezekano mkubwa Bw Odinga akaanza kupoteza sifa miongoni mwa baadhi ya wafuasi wake, kwani ataonekana kama mtetezi wa wafisadi.

“Tangu miaka ya tisini, Bw Odinga amejijengea sifa ya kisiasa kama mwanamageuzi, mtetezi wa haki na sauti ya mnyonge. Ni kutokana na uanaharakati wake ambapo alikamatwa na kufungwa gerezani na utawala wa marehemu Daniel Moi. Kuna hatari kubwa kwa kiongozi huyo kupoteza ushawishi wake kwani wengi wanamwona kama mtetezi wa watu wafisadi,” asema Bw Kipkorir Mutai, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Wadadisi wanasema ni kinaya kwa Bw Odinga kunyamazia maovu yanayoendelea chini ya utawala wa Jubilee, ambapo sasa wajibu huo “ameuachia” Naibu Rais William Ruto na waandani wake.

“Katika muhula wa kwanza, Raila tuliyemwona wakati huo ni tofauti sana. Ni kupitia juhudi zake ambapo Wakenya walifahamu kuhusu sakata kama mikopo tata kama Eurobond. Je, ujasiri huo u wapi? Fichuzi kama hizo ndizo zilizomjengea sifa kama mtetezi wa wanyonge,” asema Bw Dismus Mokua, ambaye ni mdadisi wa siasa.

Kulingana na wadadisi, kuna hatari Bw Odinga “kujikwaa kisiasa” kwa kumtetea Rais Kenyatta, na badala yake kumpa nafasi Dkt Ruto kujijenga.

Hili linatokana na hatua ya baadhi ya washirika wa Dkt Ruto kujitokeza kumkashifu Rais Kenyatta na familia yake, wakimtaka kueleza na kutoa ufafanuzi kamili kuhusu fedha hizo.

“Kwa muda mrefu, Dkt Ruto amekuwa akihusishwa na sakata za ufisadi, hasa kutokana na michango mikubwa ya pesa ambayo amekuwa akitoa katika makanisa. Ni michango ambayo vigogo kama Bw Odinga wametilia shaka asili yake, wakiihusisha na uporaji wa fedha za umma. Amekuwa hata akiyarai makanisa kukataa fedha hizo, akidai zinatokana na ufiasadi. Anapojitokeza sasa kuanza kumtetea Rais Kenyatta, ataonekana kama kiongozi mnafiki, kwani ikiwa angekuwa anaeleza ukweli, wengi walimtarajia kumshinikiza Rais kuwajibika, kama ambavyo amekuwa akimhimiza Dkt Ruto,” asema Bw Wycliffe Muga, mdadisi wa siasa.

Ingawa Dkt Ruto hajazungumzia wazi ufichuzi huo tangu ulipoibuka, washirika wake wamemtaka Rais Kenyatta na jamaa zake kuwaeleza Wakenya kuhusu namna walivyopata fedha hizo.

Baadhi ya washirika hao ni wabunge Kimani Ichung’wa (Kikuyu), Gladys Shollei (Uasin Gishu), Millicent Omanga (Seneta Maalum) kati ya wengine.

“Ni wakati Rais awaeleze Wakenya anachofahamu kuhusu fedha hizo. Je, zinatokana na uporaji wa mali ya umma? Mbona wakaziweka ng’anbo badal ya kuziwekeza nchini? Hayo ndiyo majibu ambayo Wakenya wanataka kutoka kwa Rais na jamaa zake,” akasema Bw Ichung’wa.

Wadadisi wanasema ikizingatiwa huu ni ufichuzi unaojulikana kimataifa, huenda ukaamwathiri sana kisiasa Bw Odinga, kwani huenda Wakenya wengi wakakosa kuamini kauli yake kuhusu juhudi atakazoweka kupambana na ufisadi.

Wanaonya ikiwa hataweka mikakati ifaayo kisiasa, huenda Dkt Ruto akaigeuza na kuanza kuwaponda wote wawili (Raila na Uhuru) kama wafisadi, hivyo “kujitakasa” dhidi ya lawama ambazo amekuwa akielekezwa na wawili hao kama kiongozi mfisadi.

“Wakenya wengi wanahangaika sana kutokana na gharama ya juu ya maisha. Wengi wanamtaka kiongozi ambaye atawahakikishia kwamba ataweka mikakati ya kutosha kuwakabili wafisadi. Hivyo, suala la ufisadi litakuwa miongoni mwa ajenda kuu zitakazozingatiwa kwenye kampeni za 2022,” asema Bw Muga.

Ingawa washirika wa Bw Odinga wanasisitiza hakumtetea Rais Kenyatta bali alieleza hisia zake, kambi ya Dkt Ruto inashikilia Bw Odinga amewasaliti Wakenya, hivyo “hii ni nafasi yake (Ruto) kuwakomboa Wakenya.”

You can share this post!

Waumini wafokea pasta dikteta

MALENGA WA WIKI: Kauli za washairi nguli kuhusu adabu za...