• Nairobi
  • Last Updated April 17th, 2024 5:11 PM
JAMVI: Mtihani mgumu wamsubiri Ruto kuhusu miungano

JAMVI: Mtihani mgumu wamsubiri Ruto kuhusu miungano

Na CHARLES WASONGA

MSIMAMO wa Naibu Rais William Ruto kwamba chama cha United Democratic Alliance (UDA) hakitabuni muungano na vyama vidogo vinavyounga azma yake ya urais umeibua hisia mseto miongoni mwa wandani wake na wadadisi.

Baadhi ya wandani wa Dkt Ruto wanahisi kuwa UDA itazongwa na misukosuko endapo itabuni miungano na vyama vingine kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

Lakini kuna tapo na wandani wake wanaohisi kuwa Dkt Ruto ataboresha nafasi yake ya kuingia Ikulu kwa kufanya muungano na vyama vingine vyenye “maono sawa na UDA.”

Kwa upande wake mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Dismus Mokua anashikilia kuwa Naibu Rais hana budi kukubali kuwa enzi ambapo Kenya ingeongozwa na chama kimoja ilipita baada ya KANU kuondolewa mamlakani 2002.

“Ikiwa kweli lengo la Dkt Ruto ni kuingia Ikulu, basi ni sharti akubali UDA ishirikiane na vyama vingine ambavyo havitadhamini wagombeaji urais lakini vimekubali kumuunga mkono. Itakuwa vigumu kwa chama chochote nchini kushinda urais kivyake,” anaeleza.

Lakini Dkt Ruto amesisitiza mara si moja kwamba vyama kama hivyo vinafaa kuvunjwa ili kuipa UDA nguvu sura ya kitaifa kilivyokuwa Jubilee kabla ya kuzongwa na changamoto 2018.

Akihutubu wiki jana nyumbani kwake, Sugoi, kaunti ya Uasin Gishu alipokea ujumbe wanasiasa kutoka eneo la Magharibi mwa Kenya, Naibu Rais alitaja vyama hivyo kama “vya kikabila ambavyo haviwezi kuunganisha taifa hili.”

“Nia yetu ni kustawisha UDA ili kiwa chama kikubwa cha kitaifa ndiposa kiweze kuendeleza ajenda yake ya kuinua maisha ya mahasla kupitia mfumo wa kukuza uchumi kuanzia chini. Kwa hivyo, nataka ieleweke kwamba UDA haitashiriki muungano na hivyo vya vidogo vya kikabila,” Dkt Ruto akasema.

Naibu Rais alikuwa akirejelea chama cha The Service Party (TSP) kinachoongozwa na aliyekuwa Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri, Chama cha Kazi (CCK) chake Mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kuria na Chama cha Mashinani (CCM) kinachoongozwa na aliyekuwa Gavana wa Bomet Isaac Rutto.

Kuvunja vyama

Licha ya Mbw Kiunjuri, Kuria na Rutto kutangaza wazi kwamba wanaunga mkono azma ya Dkt Ruto ya kuingia Ikulu 2022, wameshikilia kuwa katu hawatavunja vyama vyao ili kuungana na UDA.

“Sisi kama wanachama wa TSP tumekubali kuunga mkono azma ya Dkt Ruto kuingia Ikulu kwa sababu tunakubaliana na sera na mpango wa Hustler Nation ambao unalenga kuwaimarisha Wakenya wa tabaka la chini kiuchumi. Lakini tutafanya hivyo ndani ya chama chetu; hatutakivuja ili kuungana na UDA,” Bw Kiunjuri akasema wiki jana kwenye mahojiano katika runinga ya KTN.

Aidha, wanasiasa huyo ambaye zamani alihudumu kama Mbunge wa Laikipia Mashariki, alipasua mbarika na kufichua kuwa sababu kuu ya yeye kukataa kujiunga na UDA kama mwanachama wa kawaida ni kwamba haamini kuwa mchujo wa chama hicho utaendeshwa kwa njia huru na haki.

“Sote tunajua yale yaliyoendelea katika makao makuu ya Jubilee kule Pangani ambapo watu fulani walinyimwa tiketi licha ya kwamba walishinda katika mchujo. Hatutaki kuingia kwenye kichinjio kama hicho na ndiposa tumekataa kuvunja chama chetu na kujiunga na UDA, “ akaeleza huku akiongeza kuwa TSP kitadhamini wagombeaji kwa nyadhifa zote tano isipokuwa wadhifa wa urais.

Kwa upande wake Bw Kuria anashikilia kuwa chama chake cha CCK hakitavunjwa kwa sababu lengo lake ni kutetea masilahi ya wakazi wa Mlima Kenya kwa ujumla.

“Ikiwa lengo la kuundwa kwa chama chetu lilikuwa ni kupigania ugavi sawa na rasilimali za kitaifa na nyadhifa serikalini kwa manufaa ya Mlima Kenya, mbona tuambiwe tukivunje? Ningependa kufafanua kuwa chama chetu kinamuunga mkono Dkt Ruto katika kinyang’anyiro cha urais lakini hakitavunjwa,” Mbunge huyo wa Gatundu Kusini akaambia ‘Taifa Jumapili‘ kwenye mahojiano kwa njia ya simu.

Uchaguzi ujao

Sawa na Bw Kiunjuri, Bw Kuria anasema kuwa CCK kitadhamini wagombeaji wa viti vya udiwani, ubunge, useneta na ugavana katika uchaguzi mkuu wa Agosti 2022.

Hata hivyo, mbunge huyo alisema hatawania kiti chochote katika uchaguzi huo ila atasalia kuwa kiongozi wa kitaifa wa chama hicho.

“Mimi sitawania kiti chochote lakini tutatumia idadi ya madiwani, wabunge, maseneta na magavana ambao watashinda kwa tiketi ya CCK kupigania ugavi sawa wa rasimali za kitaifa kwa watu wetu wa Mlima Kenya. Hilo tutafanya na mgombeaji wa urais yeyote ambaye ataibuka mshindi, sio Dkt Ruto pekee,” Bw Kuria anafafanua huku akikariri msimamo wake kwa eneo hilo sharti litengewe asilimia 40 za nyadhifa serikalini.

Bw Rutto, naye anashikilia kuwa CCM ni chama kongwe zaidi kuliko UDA na hivyo haiwezi kuvunjwa.

“Mnamo 2020, nilitangaza wazi katika uwanja wa Bomet Green Stadium kwamba nimeamua kuzika tofauti za kisiasa na Naibu Rais William Ruto na kuunga mkono azma yake ya kuingia Ikulu 2022. Kadhalika nilichukua hatua hiyo kwa ajili ya umoja wa jamii yetu ya Kalenjin. Sasa mbona watu wengine wanataka nivunje chama cha CCM ilhali katiba inaruhusu demokrasia ya vyama vingi?” akauliza mwanasiasa huyo ambaye pia alihudumu kama mwenyekiti wa Baraza la Magavana (CoG) kati ya 2013 na 2015.

Lakini Seneta wa Meru Mithika Linturi na wabunge Rigathi Gachagua (Mathira) na Benjamin Washiali (Mumias Mashariki) wanaunga kauli ya Dkt Ruto kwamba UDA haifai kubuni muungano na vyama vingine.

“Wanasiasa hawa kutoka Mlima Kenya wanawakanganya raia kwa kubuni vyama vidogo ili kuendeleza masilahi yao lakini sio ya wananchi. Nia yao ni kumwekea masharti Naibu Rais uchaguzi mkuu unapowadia kwa manufaa yao ya kibinafsi. Hatufai kubuni muungano na watu kama hawa,” anaeleza.

Anaongeza: “Kiunjuri alikuwa na chama chake cha Grand National Unity (GNU); aliuzia Uhuru na akateuliwa waziri. Munya (Peter) alikuwa na PNU; akaipiga mnada na akapata cheo cha waziri wa Kilimo. Hayo ndiyo masilahi ya kibinafsi ninayoerejelea.”

Kwa upande wake Bw Gachagua anadai Mbw Kuria na Kiunjuri wanaongozwa vyama visivyo na ufuasi wowote katika eneo la Mlima Kenya.

“Kando na Kuria, je unafahamu mwanachama mwingine wa CCK katika eneo la Kati mwaka Kenya au popote nchini?” Hatutaki kuyumbishwa na vyama vya mikoba ilhali azma yetu kuu ni kunadi UDA,” akaeleza.

Lakini kulingana na Bw Mokua, vyama hivyo vidogo huenda vikageuka kuwa kimbilio la wanasiasa ambao watatendewa hiana katika mchujo wa UDA.

“Tayari minong’ono imeanza kuibuka kuwa Dkt Ruto amekwisha kuidhinisha wanasiasa fulani kwa nyadhifa fulani katika ngome za UDA za Mlima Kenya na Rift Valley. Hii ni ishara tosha kwamba baadhi ya wagombeaji wa UDA watakaohisi kutotendewa haki watahamia vyama hivi. Kwa hivyo, ni muhimu kwa Dkt Ruto kuvikumbatia la sivyo vitaamua kuunga mkono wapinzani wake haswa Raila Odinga,” anaeleza.

You can share this post!

Ruto atua Nyanza akitaka Uhuru, Raila waunge mkono azma yake

Walioingia mitini