• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
JAMVI: Nassir atagundua siri ya kurithi joho la ‘Sultan’?

JAMVI: Nassir atagundua siri ya kurithi joho la ‘Sultan’?

  • Mwandani wake Joho hajajitokeza wazi kutangaza atakayeunga mkono kwa urithi wa ugavana
  • Shahbal ameleta ushindani dhidi yake ndani ya ODM
  • Waliompangia Joho siasa zake akashinda ugavana mara mbili wamejiunga na Shahbal
  • Tofauti na Shahbal ambaye hajaongoza kisiasa, Nassir ameanza kurushiwa mawe kuhusu utendakazi wake wa ubunge

Na VALENTINE OBARA

MBUNGE wa Mvita, Bw Abdulswamad Nassir, ana kibarua kigumu katika juhudi zake za kutaka kurithi kiti cha Gavana wa Mombasa Hassan Joho mwaka 2022.

Hivi majuzi, hesabu za Bw Nassir katika uwaniaji wa kiti hicho zilionekana kuvurugwa wakati mpinzani wake, Bw Suleiman Shahbal alipoamua kuhama Chama cha Jubilee akajiunga na ODM.

Kabla Bw Shahbal kuchukua hatua hiyo, wengi walitarajia mbunge huyo hangepata upinzani mkubwa katika ODM kwani Mbunge wa Likoni, Bi Mishi Mboko ambaye awali alikuwa akiazimia kuwania ugavana, hajajitokeza kimasomaso kujipigia debe katika siku za hivi majuzi.

Hata hivyo, ujio wa Bw Shahbal katika chama hicho sasa unamaanisha kuwa huenda chama kikalazimika kufanya kura ya mchujo ili kuamua atakayepeperusha bendera ya ODM katika uchaguzi wa ugavana Mombasa 2022.

Ijapokuwa sheria za chama hicho huruhusu wagombeaji wa kisiasa kuteuliwa moja kwa moja bila kupitia kura ya mchujo, duru ziliambia Taifa Leo kwamba Kiongozi wa ODM Raila Odinga alimhakikishia Bw Shahbal kutakuwa na mchujo kwa njia huru na ya haki walipokutana Mombasa wiki mbili zilizopita.

Bw Nassir hata hivyo husisitiza kuwa ana hakika wananchi wanajua ni kiongozi yupi ana nia ya kuwahudumia kwa njia ambayo itawaletea mabadiliko bora katika maisha yao.

“Mimi si nabii lakini nawahakikishia ifikapo mwaka ujao kwa majaliwa ya Mungu, tutapanda majukwaa haya haya na tofauti itakayokuwepo ni kuwa, mmoja kati yenu wawili (Bw Odinga na Bw Joho) atakuwa ni rais na mimi ndiye nitamwalika hapa kuzungumza nikiwa gavana wa kaunti hii,” alisema, katika hafla ya uzinduzi wa kituo maalumu cha kisasa cha matibabu ya moyo Hospitali Kuu ya Rufaa ya Pwani iliyo Mombasa.

Tangu wakati Bw Nassir alipotangaza azimio lake miaka michache iliyopita, wengi walitarajia kuwa angepata uungwaji mkono kutoka kwa Bw Joho.

Hii ni kutokana na jinsi wawili hao wamekuwa wandani wa kisiasa kwa muda mrefu na walikuwa wakiandamana katika hafla nyingi ambapo Bw Joho alikuwa akiendeleza miradi ya maendeleo ya kaunti.

Uswahiba huo wao ulifasiriwa na wadadisi wa kisiasa kumaanisha Bw Joho alikuwa akimwandaa mbunge huyo kurithi kiti chake wakati atakapokamilisha kipindi chake cha mwisho cha uongozi kikatiba mwaka ujao.

Bw Joho hajajitokeza wazi kutangaza atakayemuunga mkono kwa kiti hicho, na katika miezi michache iliyopita, alianza kuonekana kuwa karibu na Bw Shahbal ambaye kwa muda mrefu katika miaka iliyopita alikuwa hasimu wake wa kisiasa.

Wiki iliyopita, Bw Joho aliandamana Bw Nassir na katika hafla Hospitali Kuu ya Rufaa ya Pwani lakini akakwepa kumtangaza mbunge huyo kuwa anayefaa kurithi ugavana.

Licha ya miito kutoka kwa umati, Bw Joho alisisitiza tu kwamba kiti hicho kinastahili kubaki kwa mwanachama wa ODM, huku akisema yeye anaelekea kupigania nyadhifa za kitaifa kwa hivyo siasa za Mombasa zitabaki kushindaniwa na Bw Nassir na wenzake.

“Mimi ni mwanachama wa ODM. Baba (Bw Odinga) ni kiongozi wa chama na mimi ni naibu kiongozi. Serikali inayoongoza Mombasa ni ya ODM na inatekeleza miradi ya maendeleo kwa sababu maono makuu ya chama ni kuhusu maendeleo kwa wananchi. Nchi hii yahitaji viongozi wanaojali masilahi ya wananchi,” alisema Bw Joho.

Mtihani mwingine ambao huenda ukamwandama Bw Nassir ni kuwa, Bw Shahbal tayari alikusanya kikosi kilichomsaidia Bw Joho kisiasa miaka iliyopita.

Kikosi hicho kinajumuisha aliyekuwa meya wa Mombasa, Bw Ahmed Mohdhar, mshauri wa masuala ya kisiasa Idris Abdirahman na aliyekuwa mbunge wa Kisauni, Bw Rashid Bedzimba.

Katika mikutano yao ya hadhara kufikia sasa, kikosi hicho cha Bw Shahbal hukosoa uongozi wa Bw Nassir katika kipindi alichotumikia kama mbunge wa Mvita.

Hata hivyo, mbunge huyo hujivunia kwa kuanzisha miradi ya maendeleo kama vile katika sekta ya elimu na afya eneobunge la Mvita.

Katika mahojiano na Taifa Jumapili, alisema mafanikio aliyoyaleta yako wazi na amepanga kushirikiana na wengine kukuza Kaunti ya Mombasa akiwa gavana.

“Mimi siwezi kupoteza pumzi yangu kujibizana na wengine. Huko ni kupoteza wakati,” akasema.

Mwelekeo huu wa kukosoa utendakazi wake unaonekana kumpendelea Bw Shahbal kwa vile hajawahi kushikilia wadhifa wowote wa uongozi wa kisiasa na hivyo basi ni vigumu kwake kukosolewa kwa madai ya uongozi duni.

Badala yake, mfanyabiashara huyo hutumia weledi wake wa kibiashara kama ishara ya usimamizi bora ambao unaweza kuongezea kaunti mapato, na kutoa mandhari bora ya uwekezaji ambayo yataongeza nafasi za ajira kwa wakazi wa Mombasa.

“Mimi ni mfanyabiashara na ninaamini uchumi wetu hutegemea biashara ndogondogo. Mojawapo ya ajenda zangu kuu itakuwa ni kustawisha hizo biashara. Watu wetu si wavivu, wanachohitaji ni mandhari bora yatakayokuza biashara zao,” akaambia Taifa Jumapili.

Kulingana naye, uwezo wake kutoa nafasi za ajira kupitia kwa uwekezaji kama vile katika Benki ya Gulf, Gulf Energy na nyinginezo hauwezi kuigwa na mwanasiasa yeyote mwingine anayetaka kuwa gavana wa Mombasa mwaka 2022.

You can share this post!

JAMVI: Madhara yanukia IEBC ikibanwa na muda wa maandalizi...

Drama washukiwa wa utekaji nyara wakinaswa