• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Jubilee, ODM kuonyesha Ruto ubabe

Jubilee, ODM kuonyesha Ruto ubabe

Na BENSON MATHEKA

MIKUTANO mikuu ya kitaifa ya wajumbe (NDC) ya vyama vya Jubilee na ODM itakayofanyika wakati mmoja mwezi huu Februari, imepangwa ili kuashiria mwanzo wa muungano wa Azimio la Umoja na kuonyesha ubabe wa kukabili ule wa Kenya Kwanza (KKA) unaoongozwa na Naibu Rais William Ruto.

Baada ya mikutano hiyo itakayofanyika Februari 25 na 26 jijini Nairobi, Rais Uhuru Kenyatta ataanza rasmi kampeni kali ya kumpigia debe kiongozi wa ODM Raila Odinga eneo la Mlima Kenya ambalo Dkt ana ufuasi mkubwa.

Chama cha Jubilee kitafanya mkutano mkuu wa kitaifa wa wajumbe katika Kenyatta International Convention Centre (KICC) huku ODM ikifanya mkutano sawa katika uwanja wa michezo wa Nyayo.

Duru kutoka vyama hivyo zinasema kwamba lengo ni wajumbe kuidhinisha ushirikiano wa vyama hivyo kwenye uchaguzi mkuu ujao na kutia rasmi saini mkataba wa muungano wa Azimio la Umoja kuhakikisha Bw Odinga atamrithi Rais Kenyatta na kuwa rais wa tano wa Kenya.

Bw Odinga amekuwa akishirikiana na washirika wa Rais Kenyatta kuvumisha vuguvugu la Azimio la Umoja, ambalo litasajiliwa rasmi kuwa muungano wa kisiasa utakaokabili KKA.

Muungano wa KKA unaleta pamoja chama cha United Democratic Alliance (UDA) cha Dkt Ruto, Amani National Congress (ANC) cha Musalia Mudavadi na Ford Kenya cha seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula.

Baadhi ya washirika wa Dkt Ruto wanaungama kuwa kampeni za uchaguzi mkuu wa Agosti 9 zitabadilika baada ya NDC za Jubilee na ODM.

“Niko UDA lakini Tsunami kamili itashuhudiwa baada ya Februari 26. Naweza kukuhakikishia kuwa mazingira ya siasa za urithi yatabadilika na kushika kasi hasa eneo la Mlima Kenya Rais Kenyatta akianza kumpigia debe Bw Odinga,” alisema mbunge mmoja aliyeomba tusitaje jina lake.

Inasemekana baada ya Jubilee na ODM kuungana rasmi, Rais Kenyatta atajitosa katika kampeni za siasa na kueleza wafuasi wake katika Mlima Kenya sababu ya kutofautiana na Dkt Ruto ambaye aliunda UDA na kutangaza Jubilee imekufa.

Mnamo Ijumaa, Rais Kenyatta alikutana na kundi la wabunge wa Jubilee na akanukuliwa akisema atajibwaga katika siasa waziwazi.Wakereketwa wa Jubilee wanasema chama hicho tawala kinajipanga upya bila Dkt Ruto na washirika wake katika UDA.

Kulingana na Katibu Mkuu wa Jubilee, Bw Raphael Tuju chama hicho kitazindua nembo na kubadilisha katiba, hatua ambayo wadadisi wanasema inalenga kukisafisha kabla ya kuungana na ODM chini ya Azimio la Umoja.

“Chama kitachunguza upya na kuidhinisha sera zake, kuidhinisha mageuzi yaliyopendekezwa kufanyiwa katiba ya chama na kuidhinisha nembo mpya, alama na bendera yake,” alisema Bw Tuju kwenye ilani kwa wajumbe.

Mageuzi hayo yanalenga kumuondoa Dkt Ruto na wandani wake waliounda UDA.Duru zinasema uzinduzi wa muungano wa Azimio la Umoja utahudhuria na vyama vingine vinavyounga azima ya Bw Odinga.

Baadhi ya vyama hivyo ni Democratic Alliance Party of Kenya (DAP-K), Party of National Unity (PNU), Narc, Maendeleo Chap Chap miongoni mwa vingine.

Duru zilieleza Taifa Jumapili kwamba baadaye Azimio la Umoja litaungana na One Kenya Alliance (OKA) unaoleta pamoja vyama vya Wiper, Narc Kenya, Kanu na UDP kabla ya kuanza kampeni kali dhidi ya KKA.

You can share this post!

Wamunyinyi kutoana kijasho na Wetang’ula kwa useneta

Hatutakubali utupange, Ruto aambia Uhuru

T L