• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
Wamunyinyi kutoana kijasho na Wetang’ula kwa useneta

Wamunyinyi kutoana kijasho na Wetang’ula kwa useneta

NA BRIAN OJAMAA

KAMPENI za kiti cha Useneta kaunti ya Bungoma zinaendelea kupamba moto huku mbunge wa Kanduyi Wafula Wamunyinyi akitangaza rasmi kuwa atamenyana na Kinara wa Ford Kenya Moses Wetang’ula kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Wamunyinyi alitangaza kuwa atagombea wadhifa huo kwenye mkutano mkubwa wa kisiasa katika uwanja wa Posta mjini Bungoma Ijumaa.

Atawania useneta kupitia chama kipya cha DAP-K ambacho kimehusishwa na Waziri wa Ulinzi Eugene Wamalwa.

Wakati wa mkutano huo uliohudhuriwa na umati mkubwa, Gavana wa sasa Wycliffe Wangamati aliidhinishwa kutetea kiti chake kupitia DAP-K huku akitarajiwa kumenyana na Spika wa Seneti Ken Lusaka.

“Tunataka kuhakikisha kuwa Wetang’ula anaenda nyumbani. Ni kutokana na hilo ambapo baada ya kuwaza kwa kina na kushauriana na wenzangu, DAP-K itakuwa na mwaniaji wa useneta Bungoma ambaye ni mimi,” akasema Bw Wamunyinyi aliyeingia bungeni kwa mara ya kwanza mnamo 1997.

Bw Wamunyinyi aliungwa mkono na seneta maalumu wa ODM Mercy Chebon ambaye alisema mwanasiasa huyo ana umaarufu ambao utamwezesha kumng’oa Bw Wetang’ula uongozini.

Bw Wamunyinyi, mbunge wa Tongaren Dkt Eseli Simiyu na Gavana Wangamati walijaribu kumbandua Bw Wetang’ula kama kiongozi wa Ford Kenya mwaka 2021, lakini hawakufaulu ndiposa wakajiunga na chama kipya cha DAP-K.

Watatu hao walichaguliwa kwa tiketi ya Ford Kenya mnamo 2017 lakini baadaye wakamlaumu Bw Wetang’ula kwa kutoendesha chama hicho vyema.

Bw Wamalwa aliapa kufanya kampeni kali kuhakikisha kuwa Bw Wangamati atahifadhi kiti cha ugavana, akimtaja kama aliyetekeleza miradi mingi ya maendeleo katika muhula wake wa kwanza.

“Wangamati amefanya vizuri kwa kuwa amejenga barabara, akatoa udhamini kwa wanafunzi kutoka familia maskini wanaojiunga na shule za sekondari na miradi mingine mingi ya kuwafaa wananchi,” akasema Bw Wamalwa.

  • Tags

You can share this post!

Viongozi wa PAA waganda kwa Raila

Jubilee, ODM kuonyesha Ruto ubabe

T L