• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 5:01 PM
Jubilee sasa mbioni kukabili UDA Bonde la Ufa

Jubilee sasa mbioni kukabili UDA Bonde la Ufa

STANLEY KIMUGE NA BARNABAS BII

CHAMA cha Jubilee kimeanza mchakato wa kufufua umaarufu wake eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa kikilenga kutoa ushindani mkali wa UDA katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Kutimiza lengo hilo, Jubilee jana iliwateua maafisa wake wapya katika eneo hilo ambapo Naibu Rais Dkt William Ruto ana ushawishi mkubwa wa kisiasa, wakazi wengi wakiunga mkono UDA.

Katika uchaguzi mkuu uliopita, Jubilee ilizoa karibu viti vyote eneo hilo ila umaarufu wake ulififia baada ya Rais Uhuru Ken – yatta kukosana na Naibu wake Dkt William Ruto kisha kuingia kwenye ukuruba wa kisiasa na Kinara wa ODM Raila Odinga mnamo Machi 2018.

Tayari baadhi ya wanasiasa wengi waliokuwa Jubilee wamehamia UDA, chama ambacho wanalenga kukitumia kutetea viti vyao.

Hapo jana, Jubilee ilimteua Mwakilishi wa Wadi ya Langas Francis Muya, kama kaimu mwenyekiti wake mpya katika Kaunti ya Uasin Gishu. Zachary Githaiga na Dkt Paul Maina walipokezwa nyadhifa za mwekahazina na katibu mtendaji mtawalia.

Maafisa wengine wa chama hicho ni Mumbi Ngugi na Titus Osirimong ambao ni wawakilishi wa wanawake na vijana mtawalia. Maafisa hao wote waliahidi kumvumisha Bw Odinga ambaye ni mwaniaji wa Urais wa vuguvugu la Azimio.

“Tunatangaza kuwa tunaunga mkono Bw Odinga ambaye ni chaguo la Rais Uhuru Kenyatta,” akasema Bw Muya.

Mrengo wa Kenya Kwanza unaoongozwa na Dkt Ruto, Musalia Mudavadi na Moses Wetang’ula, umekuwa ukipana nguvu na ule wa Azimio, yote ikilenga kudhibiti kura za Bonde la Ufa.

Mrengo wa Azimio la Umoja umekuwa

ukijivumisha kwa kuwatumia viongozi wa kijamii pamoja na washauri wa kisiasa ili kupenya kisiasa. Kwa upande mwingine, mrengo wa Kenya Kwanza umekuwa ukiandaa misururu ya mikutano ya kisiasa kujipigia debe.

“Wapigakura wanafaa waruhusiwe kuwachagua viongozi ambao wanapenda. Hakuna mtu ambaye anafaa kutishwa na tuko tayari kupambana na wenzetu wa UDA debeni,” akasema Gavana wa Elgeyo-Marakwet Alex Tolgos.

Bw Tolgos analenga kumenyana na Seneta Kipchumba Murkomen kutwaa wadhifa wa Useneta baada ya kumaliza kuhudumu mihula miwili kama gavana wa kaunti hiyo.

Gavana huyo alisema kuwa wanalenga kuhakikisha kuwa Bw Odinga anapata zaidi ya asilimia 40 za kura za wakazi wa Kaskazini mwa Bonde la Ufa.

“Kila mtu yupo huru kuuza sera zake na ni raia ambao watafanya uamuzi huo. Kile ambacho tunahitaji ni kampeni za amani. Seneti inahitaji watu wenye hekima na uelewa mpana wa ugatuzi na binafsi nipo tayari kumenyana na Murkomen,” akaongeza.

Licha ya misururu ya mikutano iliyoongozwa na Naibu Rais katika eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa, kibarua kigumu ni jinsi ya kuandaa uteuzi huru ikizingatiwa wanasiasa wengi wanalenga kutwaa tiketi ya chama hicho.

  • Tags

You can share this post!

Waathiriwa wa ghasia waonya wanasiasa

Mpinzani wa Mbadi ajiondoa na kumuunga mkono ugavana Homa...

T L