• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Jumla ya watu 55 wanataka kuwania urais

Jumla ya watu 55 wanataka kuwania urais

NA CHARLES WASONGA

HUENDA karatasi ya kupiga kura ya urais ikawa ndefu zaidi katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022 ikiwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) itawaidhinisha jumla ya watu watu 55 ambao wameonyesha nia ya kutaka kuwania urais.

Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari Jumatano, Mei 18, 2022 mgombea mmoja ndiye ameonyesha nia ya kuwania kwa tiketi ya chama cha muungano.

Huyo ni Raila Odinga ambaye atapeperusha bendera ya chama cha muungano wa Azimio La Umoja-One Kenya.

Wengine 14 akiwemo Naibu Rais William Ruto wamewasilisha majina yao wakitaka kuwania urais kwa udhamini wa vyama vya kisiasa.

Dkt Ruto anawania urais kwa tiketi ya chama chake cha, United Democratic Alliance (UDA) ambacho ni miongoni mwa vyama tanzu katika muungano wa Kenya Kwanza (KKA).

Katika taarifa hiyo, mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati alisema kuwa jumla ya watu 55 wamewasilisha majina yao wakitaka kuwania urais kama wagombeaji wa kujitegemea.

“Wawaniaji hawa wote waliwasilisha majina yao na yale ya wagombea wenza wao kwa IEBC kufikia tarehe ya mwisho kufanya hivyo mnamo Mei 16, 2022,” Bw Chebukati akaeleza.

Lakini kwenye notisi iliyochapishwa katika gazeti rasmi la serikali mnamo Machi 13 IEBC ilikuwa imeorodhesha jumla ya wawaniaji 38 wa kujitegemea.

Bw Chebukati aliongeza kuwa jumla ya wawaniaji 244 wa ugavana na wawaniaji wenza wao pia waliwasilisha majina yao kwa afisi za IEBC katika ngazi za kaunti kufikia Mei 16.

Wawaniaji hao wanajumuisha 167 ambao watawania kwa udhamini wa vyama vya kisiasa na 77 watakaowania kama wawaniaji huru.

“Wawaniaji wa urais na wale wa ugavana watasajiliwa rasmi na wasimamizi wa uchaguzi kati ya Mei 29 na Juni 7, 2022.

Hii ni baada ya uhitimu wao kimasomo kati ya mahitaji mengine kuthibitishwa,” Bw Chebukati akasema.

Kando na hayo jumla ya watu 748 wanataka kuwania viti vya ubunge kama wawaniaji huru, 74 wanasaka ugavana, useneta (108), wabunge wawakilishi wa kike (95) huku jumla ya 4, 738 wanataka kuwania viti vya udiwani.

  • Tags

You can share this post!

Malumbano ya Sonko, Haji yazidi kutokota

Himizo Mkaguzi ashirikishe umma huku akizindua nakala ya...

T L