• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 1:02 PM
Junet ajiondolea lawama kuhusu matamshi yaliyomtia kikaangoni

Junet ajiondolea lawama kuhusu matamshi yaliyomtia kikaangoni

Na SAMMY WAWERU

MBUNGE wa Suna Mashariki, Junet Mohammed amejitetea vikali kufuatia matamshi yake yaliyojawa kejeli kuhusu safari ya kiongozi wa ODM, Raila Odinga kuingia Ikulu 2022.

Akizungumza katika hafla ya mchango Nyamira iliyoongozwa na Bw Raila na Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i, mbunge huyo alisema endapo kiongozi wa ODM atatwaa serikali mwaka ujao itakuwa ya watu wa Nyanza.

“Baba (akimaanisha Raila Odinga) akishinda, serikali ni ya watu wa Nyanza,” Junet akasema. Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Waziri wa Afya, Bw Mutahi Kagwe na mbunge huyo kwenye mazungumzo aliskika kutania waziri huyo na jamii ya Mlima Kenya anakotoka.Alisema Bw Kagwe atakuwa akizuru eneo la Nyanza kama mgeni.

Junet alisema “watu wa Kagwe”, akiashiria jamii ya Mlima Kenya, imeridhia na kufurahia uongozi kwa zaidi ya miaka 20 hivyo basi ikiwa Raila ataibuka kidedea katika uchaguzi wa 2022 itakuwa awamu ya Nyanza kusherehekea matunda.

“Sitaki watu wa gazeti waskie hiyo. Mutahi Kagwe anaweza kasirika. Lakini hata nyinyi mlikuwa nayo (akimaanisha kuwa serikalini) zaidi ya miaka 20 na safari hii ni ya watu wa Nyanza. Mutahi utakuja hapa kama mgeni,” akasema.

Rais Uhuru Kenyatta, mtangulizi wake Rais (mstaafu) Mwai Kibaki na Hayati Mzee Jomo Kenyatta ambaye pia ni baba wa rais wa sasa, ndio marais kutoka eneo la Kati ambao wamepata fursa kuongoza Kenya.

Ni matamshi ambayo yameweka mbunge huyo taabani, wanasiasa wanaohusishwa na mrengo wa Tangatanga, unaoegemea upande wa Naibu wa Rais, Dkt William Ruto wakidai ni ya uchochezi.

Hata hivyo, kulingana na Bw Junet ujumbe wake ulitafsiriwa isivyofaa.“Tunapoenda Mlima Kenya, Pwani, Turkana…kati ya maeneo mengine huambia wakazi serikali ni yao.“Ujumbe wangu ulitafsiriwa vibaya. Sikuzungumzia kutenga jamii yoyote ile.

Matamshi yangu yalilenga kuleta pamoja jamii tofauti ili tupate kura,” akajitetea akizungumza jijini Nairobi. Junet alilaumu wabunge na viongozi wa UDA, chama kinachohusishwa na Dkt Ruto, kwa kile alidai ni kueneza propaganda kumpaka tope.

Alisema vuguvugu la Bw Raila, Azimio la Umoja, linalenga kuleta Wakenya pamoja na kuhubiri amani. Kufuatia matamshi ya Junet Nyamira, wadadisi wa masuala ya kisiasa wameonya huenda yakaathiri mahesabu ya Raila kuingia Ikulu mwaka ujao, ikizingatiwa kuwa yanalenga jamii ya Mlima Kenya na ambayo Waziri huyo Mkuu wa zamani anajaribu juu chini kuiweka kwenye kapu lake la kura.

You can share this post!

Mbunge ataka fujo za kisiasa zichunguzwe kwa kina, akidai...

IEBC yaeleza wasiwasi kuhusu idadi ya chini ya...

T L