• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Mbunge ataka fujo za kisiasa zichunguzwe kwa kina, akidai kuna wanaopanga njama mikutano yao ivurugwe

Mbunge ataka fujo za kisiasa zichunguzwe kwa kina, akidai kuna wanaopanga njama mikutano yao ivurugwe

Na SAMMY WAWERU

MBUNGE wa Kathiani, Robert Mbui ameitaka idara ya polisi (NPS) kuchunguza kwa kina mashambulizi yanayoshuhudiwa katika mikutano ya kisiasa.

Bw Mbui ametoa himizo hilo siku chache baada ya msafara wa Naibu wa Rais William Ruto kushambuliwa Kaunti ya Busia, wakati akiendeleza kampeni katika safari yake kusaka kura kuingia Ikulu 2022.

Kundi la wahuni, lilirushia mawe msafara wa Dkt Ruto na kuharibu magari, NPS Jumapili ikithibitisha baadhi ya wahusika wametiwa nguvuni. Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i kukashifu vikali tukio hilo na kuagiza polisi kukamata waliohusika wachukuliwe hatua kisheria.

Akisisitiza kila mwanasiasa na mgombea wa kiti cha kisiasa ana haki kuzuru eneo lolote la taifa, Dkt Matiang’i alisema fujo na ghasia za aina hiyo hazitastahimiliwa “kwa sababu machafuko ya 2007/2008 yalichochewa na visa kama hivyo”.

Washukiwa wa mashambulizi ya msafara wa Ruto Busia walifikishwa kortini Jumatatu, japo walikana mashtaka. Wanaendelea kuzuiliwa, uchunguzi ukitekelezwa. Kwa upande wake Mbui, kiini cha mashambulizi ya kisiasa kinapaswa kuwekwa paruwanja.

“Si ajabu wanaoshambuliwa wawe ndio wenye kupanga, ili wapate kura za huruma,” mbunge huyo akasema akizungumza jijini Nairobi. “Fujo na ghasia katika mikutano ya kisiasa ni hatia na serikali isizipe nafasi. Idara ya polisi ichunguze kwa kina wanaopanga na kufadhili mashambulizi,” akahimiza.

Naibu Rais alikashifu vikali tukio la msafara wake Busia kushambuliwa, akisisitiza kwamba Kenya ni salama na ina amani akisema siasa za aina hiyo hazitapata mwanya. Kamati ya kuangazia visa vya mashambulizi ya kisiasa, fujo na ghasia za kabla, wakati na baada ya uchaguzi imezinduliwa. Inaongozwa na Jaji Mkuu, CJ Martha Koome.

Kando na idara ya mahakama, inajumuisha ile ya usalama na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC). Akizungumza jijini Nairobi baada ya uzinduzi huo, Waziri Matiang’i alionya wachochezi wa vurugu kwenye mikutano ya kisiasa.

“Tutaihimiza IEBC kupiga marufuku wanasiasa wanaochochea ghasia na vurugu kushiriki uchaguzi mwaka ujao,” Dkt Matiang’i akatahadharisha. Tayari joto la kisiasa limeanza kupanda, ikiwa imesalia chini ya miezi kumi taifa lishiriki uchaguzi mkuu.

Wanaomezea mate nyadhifa za kisiasa wanaendeleza kampeni kusaka kura kuchaguliwa. Naibu Rais, Dkt Ruto na mpinzani wake, kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga wamekuwa wakiandaa mikutano ya umma maeneo tofauti nchini kurai Wakenya kuwapa kura.

You can share this post!

Omanyala atangazwa mwanamichezo bora wa Septemba

Junet ajiondolea lawama kuhusu matamshi yaliyomtia...

T L