• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 3:09 PM
Kalonzo hatimaye ajiunga na Raila dakika za mwisho

Kalonzo hatimaye ajiunga na Raila dakika za mwisho

NA CECIL ODONGO

KIONGOZI wa Wiper, Kalonzo Musyoka, Jumamosi alitupilia mbali azma yake ya urais, akaingia katika muungano wa Azimio La Umoja na kutangaza kuwa atamvumisha kiongozi wa ODM Raila Odinga katika kila pembe ya nchi ili ashinde urais kwenye uchaguzi wa Agosti 9.

Juhudi za kuhakikisha Bw Musyoka anaingia katika Azimio La Umoja zilifanikishwa na Rais Uhuru Kenyatta ambaye kwa mara ya kwanza Jumamosi alihudhuria mkutano wa hadhara wa kumpigia debe Bw Odinga katika uwanja wa Jacaranda, Nairobi.

Ni katika mkutano huo ambapo Bw Musyoka ambaye alikaribishwa na Rais Kenyatta kuhutubu, alisema alikuwa tayari kuwania urais lakini akaamua kumwachia Bw Odinga nafasi hiyo kwa mara ya tatu.

“Nilikuwa tayari sana kuwania urais lakini tunaangalia umri pia. Hii Azimio-One Kenya Alliance ni kubwa na inajumuisha msingi wa Jubilee, ODM na Wiper na vyama vingine vyote,” akasema Bw Musyoka huku akishangiliwa na maelfu ya wafuasi waliosubiri kwa zaidi ya saa kumi kuwasikiliza viongozi hao.

“Ndugu Raila tumetoka mbali na tumekula vitoa machozi pamoja.Tulianza LDP, tukaingia ODM, Cord na NASA ambako tulinaswa. Nimekuja kutangaza kubuniwa kwa Azimio-One Kenya Alliance na kusema kuwa mwaniaji wetu wa urais ni Raila Odinga.”

“Nawarai wafuasi wetu wote wa OKA wamuunge mkono na ninaamini Raila hatatuangusha. Kwa roho safi ninasema Raila Odinga tosha kwa mara ya tatu na nitamtafutia kura Kenya nzima,” akaongeza.

Bw Musyoka amekuwa na uhasama mkubwa na Bw Odinga kuhusiana na muafaka wa uliokuwa muungano wa NASA anaodai ulikiukwa na ODM.

KUSITASITA

Alikuwa amejivuta kujiunga na Azimio La Umoja akisisitiza Bw Odinga alifaa kumuunga mkono na kumtangaza mgombea urais.

Juhudi za kumfanya abadilishe msimamo zimekuwa zikiendelea kwa miezi kadhaa hadi jana alipokubali kujiunga na muungano huo. Duru zinasema ilibidi Rais Kenyatta kutumia weledi wake wa kisiasa kuyeyusha moyo wa Bw Musyoka kwa kukubali baadhi ya matakwa yake na washirika wake.

Mnamo Juni 16, 2021, kwenye runinga ya NTV, Bw Musyoka alisema angekuwa mtu mjinga zaidi kumuunga mkono Bw Odinga kwa mara ya tatu baada ya kufanya hivyo mnamo 2013 na 2017.

Kabla ya kuelekea uwanja wa Jacaranda, viongozi hao walihudhuria mkutano mfupi wa wajumbe wa Azimio la Umoja katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Kenyatta (KICC) ambapo vyama 26 vilitia saini mkataba wa kushirikiana kumvumisha Bw Odinga chini ya muungano huo.

Wajumbe katika KICC pia walisubiri kuanzia saa tatu hadi saa nane viongozi hao wakikamilisha mazungumzo na kutayarisha mkataba wa Azimio La Umoja. Baadhi ya vyama hivyo ni, Narc, Democratic Action Party of Kenya , Devolution Empowerment Party , Farmers Party, Party of National Unity, KANU, Kenya National Congress, Pamoja African Alliance, United Party of Independent Alliance (UPIA), Kenya Union Party, United Progressive Alliance (UPA), Maendeleo Chap Chap, Muungano Party, Kenya Union Party (KUP), Ubuntu People Forum.

Mbele ya wajumbe hao wengi waliokuwa viongozi na maafisa wa vyama tanzu vya Azimio La Umoja, Rais Kenyatta alimshukuru Bw Musyoka kwa kuzima azma yake na kukubali kumuunga mkono Bw Odinga kwa mara ya tatu, akisema lengo la muungano wao ni kuwaunganisha Wakenya.

“Tumemchagua mheshimiwa Raila Odinga awe Rais wa tano wa Kenya. Sina shaka ana uwezo, nia na Mungu atamjaalia ahakikishe taifa linasonga mbele likiwa na umoja, maendeleo na kupigana na ufisadi,” akaongeza.

Vilevile, Kenyatta aliahidi kumvumisha Bw Odinga na kusema muafaka walioafikiana 2018 ulisaidia sana kuhakikisha taifa linadumisha umoja.

“Hamkuwa mkiona nikifanya kampeni lakini kwa sababu ni siku ya kihistoria, lazima nionyeshe upande ambao ninaegemea. Wengi hawakuwa wakiamini kuwa mimi na Raila tunaweza kuwa upande moja. Waliokuwa wakifikiria tunadanganyana kwa miaka minne iliyopiga, waone na wasikie,” akasema Rais Kenyatta.

Aliposimama kuhutubu KICC, Bw Odinga alikiri kuwa kumekuwa na uhasama kati yake na Bw Musyoka ila baada ya mkutano huo, wameridhiana na sasa lengo lao ni kutwaa uongozi wa nchi kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti.

“Ndugu Kalonzo tulikuwa na shida, leo tumeongea, tumesalimiana na kuamua kusafiri pamoja kwa mara nyingine,” akasema Bw Odinga.

Gavana wa Pokot Magharibi John Lonyangapuo aliwasilisha hoja ya kuwapendekezea wajumbe waliokwepo KICC wamuunge mkono Bw Odinga.

Mbunge wa Likoni Mishi Mboko aliunga hoja hiyo iliyokuwa kumbukumbu ya aina yake kwa Bw Odinga kuandamana na Rais Kenyatta katika uwanja wa Jacaranda ambapo alikatazwa na serikali kuandaa mkutano wa kisiasa baada ya kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu wa 2017.

You can share this post!

Liverpool wakomoa Brighton na kuendeleza presha kwa...

WALIOBOBEA: Muthaura alichapa kazi akaaminiwa na Kibaki

T L