• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 7:12 PM
Kalonzo kupambana na Kingi kuwania cheo cha spika bunge la Seneti

Kalonzo kupambana na Kingi kuwania cheo cha spika bunge la Seneti

NA BENSON MATHEKA

KIONGOZI wa Wiper Kalonzo Musyoka, sasa ndiye atapeperusha bendera ya Azimio la Umoja-One Kenya katika kinyang’anyiro cha uspika wa Seneti leo Alhamisi.

Bw Musyoka, ambaye alihudumu kama naibu spika wa Bunge la Kitaifa kutoka 1988 hadi 1992, jana aliidhinishwa kuwania wadhifa huo wakati wa mkutano kundi la wabunge wa Azimio.

Katika mkutano huo ambao ulifanyika katika mkahawa wa Maasai Mara, Kajiado na kuongozwa na Rais Uhuru Kenyatta, Seneta wa Kilifi Stewart Madzayo atawania wadhifa wa Naibu Spika wa Seneti.

Bw Musyoka sasa atapambana na aliyekuwa Gavana wa Kilifi Amason Kingi, ambaye anadhaminiwa na muungano wa Kenya Kwanza unaoongozwa na Rais Mteule William Ruto.

Hii ni baada ya aliyekuwa Seneta wa Mombasa Hassan Omar kujiondoka katika kinyang’anyiro hicho na kutangaza kuwa atamuunga mkono Bw Kingi.

Seneta wa Meru Kathuri Murungi naye atashindana na Bw Madzayo katika uchaguzi wa naibu spika wa Seneti.
Mrengo wa Kenya Kwanza una idadi ya maseneta 24 huku mrengo wa Azimio ukiwa na maseneta 23.

Jana Jumatano, wawaniaji viti hivyo walirejesha stakabadhi zao kwa karani wa Seneti Jeremiah Nyeng’enye katika afisi yake iliyoko majengo ya bunge.

Katika bunge la kitaifa, Seneta wa Bungoma Moses Wetang’ula na Spika wa zamani Kenneth Marende ndio watakaokabana koo katika kinyang’anyiro cha uspika.

Jana Jumatano, Bw Wetang’ula alijiuzulu wadhifa wake wa useneta ili aweze kuwania kiti hicho.

“Ninawania kiti hiki kwa sababu nina uwezo wa kuongoza Bunge la Kitaifa katika kutekeleza wajibu wake. Ninawashauri wabunge kutoka pande zote mbili kuniunga mkono ili tuweze kujenga asasi ya bunge na kuleta maendeleo nchini Kenya,” Bw Wetang’ula akasema.

Katika uchaguzi wa naibu spika, wataoshindana ni Mbunge Mwakilishi wa Uasin Gishu Gladys Boss Shollei (Kenya Kwanza) na Mbunge wa Dadaab Farah Maalim.

  • Tags

You can share this post!

Haaland atambisha Man-City dhidi ya Sevilla katika UEFA

Uhuru bado kuamini Ruto alishinda urais

T L