• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 8:46 PM
Uhuru bado kuamini Ruto alishinda urais

Uhuru bado kuamini Ruto alishinda urais

NA BENSON MATHEKA

RAIS Uhuru Kenyatta bado hajakubali kwamba naibu wake William Ruto atakuwa mrithi wake hata baada ya ushindi wake kuidhinishwa na Mahakama ya Upeo.

Akihutubia mkutano wa Wabunge wa muungano wa Azimio la Umoja One Kenya uliofanyika jana katika Kaunti ya Kajiado, Rais Kenyatta alisema anaamini mgombea urais wa muungano huo Raila Odinga alishinda uchaguzi wa Agosti 9.

“Nitakabidhi mamlaka nikitabasamu kwa sababu ni jukumu langu la kikatiba kufanya hivyo. Lakini kiongozi wangu ni Baba Raila Odinga. Siasa sio kitu cha kuweka kwa mifuko yako,” alisema.

Ingawa Rais Kenyatta mnamo Jumatatu alisema aliheshimu uamuzi wa Mahakama ya Upeo na kuahidi kuhakikisha kuwa atampokeza mamlaka Dkt Ruto hapo Jumanne wiki ijayo, bado hajampongeza naibu wake wa miaka 10 iliyopita.

Wakati wa kampeni Rais Kenyatta alikuwa akisisitiza kuwa hatapokeza madaraka kwa Dkt Ruto, lakini sasa hana budi kwa sababu za kikatiba.

Mnamo Jumanne, Rais Kenyatta na Bw Odinga walikutana kupeana pole kufuatia kushindwa kwao na Naibu Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Mnamo Jumatatu, Mahakama ya Upeo iliidhinisha ushindi wa Dkt Ruto kuwa Rais Mteule wa Kenya na kutupilia mbali kesi ambayo ilikuwa imewasilishwa na Bw Odinga na walalamishi wengine saba.

“Ikiwa kuna mtu anayeumia baada ya Azimio kubwagwa kwenye uchaguzi, ni Rais Kenyatta ambaye alishindwa kumzima Dkt Ruto kumrithi kupitia Bw Odinga. Waziri Mkuu huyo wa zamani pia anaumia kwa kushindwa katika jaribio lake la tano la kuingia ikulu hasa baada ya majaji wa Mahakama ya Upeo nchini kutupilia mbali ushahidi wake,” akasema mbunge mmoja wa Azimio ambaye aliomba tusitaje jina.

Picha zilizosambazwa mtandaoni zilionyesha Rais Kenyatta akiwa na Bw Odinga, mkewe Ida na binti yao Winnie katika nyumba ya kiongozi huyo wa chama cha ODM mtaani Karen, Nairobi.

Katika picha nyingine, viongozi hao wanaonekana wakiwa na Gavana wa Siaya James Orengo na Profesa Makau Mutua ambaye alikuwa msemaji wa Bw Odinga kwenye uchaguzi wa Agosti 09, 2022.

Bw Orengo naye aliongozwa mawakili waliowakilisha Bw Odinga katika kesi ya kupinga ushindi wa Dkt Ruto. Viongozi hao hawakutoa taarifa rasmi kuhusu mkutano huo au kuchapisha picha hizo katika mitandao yao ya kijamii.

Inaaminika kuwa viongozi hao walijadili matokeo ya uchaguzi na kutupiliwa mbali kwa kesi ya kupinga matokeo na majaji saba wa Mahakama ya Upeo. Mkutano wao ulitangulia wa jana ambapo walikutana na wabunge waliochaguliwa kwa tikiti ya vyama tanzu vya muungano wa Azimio kabla ya Bunge kufunguliwa leo Alhamisi.

Rais Kenyatta aliitisha mkutano huo ili viongozi hao wajadili mwelekeo baada ya kushindwa na Dkt Ruto na muungano wake wa Kenya Kwanza.

Mkutano huo ulijiri huku washirika wa Rais Kenyatta na Bw Odinga wakilaumiana kufuatia kushindwa kwa muungano wa Azimio katika uchaguzi uliokuwa na ushindani mkali.

Baadhi ya washirika wa Bw Odinga wanamlaumu Rais Kenyatta kwa kile wanasema ni kukosa kutumia ushawishi wake kikamilifu kusaidia muungano wao kushinda. Kulingana na mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino, huenda Rais Kenyatta alimcheza Bw Odinga.

“Baba, daima utakuwa shujaa wangu. Walikuwa wakikucheza tu. Ulikuwa utapeli, lakini tutaishi kupigana siku nyingine,” Bw Owino alisema saa chache kabla ya Mahakama ya Upeo kutoa uamuzi mnamo Jumatatu.

Baadhi ya wanachama wa Azimio wanahisi kwamba muungano huo ulijiangusha kwa mikakati na mipangilio duni hasa kwa kutokuwa na maajenti katika vituo vyote vya kupigia kura.

Katika chama cha ODM, baadhi ya wandani wa Bw Odinga wanamlaumu mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohammed na aliyekuwa Gavana wa Mombasa Hassan Joho.

  • Tags

You can share this post!

Kalonzo kupambana na Kingi kuwania cheo cha spika bunge la...

Kylian Mbappe aongoza PSG kuzamisha chombo cha Juventus...

T L