• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 4:23 PM
Kalonzo kupewa mwelekeo baada ya matokeo ya kamati ya Azimio

Kalonzo kupewa mwelekeo baada ya matokeo ya kamati ya Azimio

NA SAMMY WAWERU

MBUNGE wa Kathiani Robert Mbui amesema chama cha Wiper kitatoa msimamo wake kuhusu kinara wake, Kalonzo Musyoka matokeo ya atakayeteuliwa mgombea mwenza katika Azimio La Umoja-One Kenya yakitangazwa.

Kamati teule ya muungano huo inaendeleza mahojiano ya kusaka atakayekuwa mgombea mwenza wa kiongozi wa ODM, Raila Odinga katika uchaguzi mkuu Agosti 9, 2022.

Shughuli hiyo ya mchujo aidha imevutia wagombea 11, Bw Kalonzo akifika Jumanne mbele ya jopokazi hilo kuhojiwa.

Awali, makamu huyo wa rais wa zamani ambaye katika uchaguzi mkuu 2013 na 2017 alikuwa mgombea mwenza wa Bw Raila, alikuwa ameapa hatakubali kupigwa msasa.

Mahojiano hayo yanaendeshwa chini ya uongozi wa Dkt Noah Wekesa, kama mwenyekiti wa kamati.

“Yalikuwa mazungumzo ya muda wa saa mbili na yenye manufaa, wala si kupigwa msasa,” Kalonzo akaambia wanahabari katika mkahawa wa Serena, jijini Nairobi baada ya kuhojiwa.

Huku hatua ya kuhudhuria zoezi hilo ikionekana kuenda kinaya na kauli yake ya awali, Bw Kalonzo alisema “ni uamuzi wangu binafsi kuhudhuria, watu wasiseme nimegoma kuenda”.

Robert Mbui, ambaye ni mwandani wa mwanasiasa huyo mapema Jumanne alisema Wiper Party inasubiri matokeo ya mchujo huo, ili kutoa msimamo wa Kalonzo.

“Tunangoja kujua nani atakayeteuliwa kuwa mgombea mwenza wa Raila Odinga. Bw Kalonzo ni kiongozi mwenye sura ya kitaifa, tajiriba ya muda mrefu na endapo hatapata nafasi hiyo, tutakuwa tumesalitiwa,” mbunge huyo akasema.

Alisema kabla kuitikia kuunga mkono kiongozi wa ODM, Kalonzo alikuwa awe katika kinyang’anyiro cha urais Agosti 9.

“Aliita mkutano akatushawishi nchi hii ni kubwa kuliko mtu binafsi, hivyo basi tumruhusu aunge mkono Raila,” Mbui akaelezea.

Mbunge huyo alionya endapo kinara wao hatateuliwa mgombea mwenza, Wiper haitakuwa na budi ila kutathmini mahesabu yake na kutoa mwelekeo.

Hata ingawa hakufichua hatua ambazo chama hicho kitachukua endapo Kalonzo hatateuliwa, Mbui alisema wandani wake sharti watetee nafasi yake katika uongozi.

Wiper ni miongoni mwa vyama vinavyounda muungano tanzu wa Azimio.

Kufuatia mgogoro wa mgombea mwenza wa Raila unaoendelea kutokota, gavana wa Machakos, Alfred Mutua mnamo Jumatatu aliugura Azimio akilalamikia kuwekwa gizani kuhusu mkataba wa makubaliano.

Dkt Mutua ndiye kiongozi wa chama cha Maendeleo Chap Chap, na alitangaza kujiunga na kambi ya naibu wa rais, Dkt William Ruto anayeongoza muungano wa Kenya Kwanza.

  • Tags

You can share this post!

TUSIJE TUKASAHAU: Dkt Ruto atuambie mradi wa kiwanda cha...

Kimathi aelekea Ureno kupaisha gari duru ya dunia

T L