• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 PM
Kampeni: Wabunge wako mbioni kubatilisha kanuni za IEBC

Kampeni: Wabunge wako mbioni kubatilisha kanuni za IEBC

Na CHARLES WASONGA

WABUNGE wameanzisha juhudi mpya za kuondoa kabisa sheria inayolenga kudhibiti kiasi cha pesa ambazo vyama vya kisiasa na wagombeaji viti wanapaswa kutumia katika kampeni za kuelekea uchaguzi mkuu ujao.

Sasa wanalenga kuondoa vipengele vinavyoweka udhibiti huo wa matumizi fedha katika kampeni za kujipigia debe.

Wabunge wanataka kufanikisha hilo kupitia Mswada wa Marekebisho ya Sheria ya Ufadhili wa Kampeni za Uchaguzi, 2021.

Mswada huu umedhaminiwa na Mbunge wa Ndaragua Jeremiah Kioni.

Endapo mswada huo utapitishwa, wawaniaji viti vyote sita – kuanzia udiwani hadi urais – hawatawajibika kufichua kwa umma jinsi watakavyotumia pesa kipindi cha kampeni.

Haya yanajiri wiki mbili pekee baada ya kamati ya bunge lote kutupilia mbali kanuni kuhusu ufadhili wa kampeni zilizowasilishwa bungeni na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).

Wabunge kutoka mirengo yote ya kisiasa walisema kuwa tume hiyo iliwasilisha kanuni hizo kuchelewa na hivyo kuzipitisha hakutakuwa na maana yoyote kwa uchaguzi mkuu ujao utakaofanyika Agosti 9, 2022.

Kupitia kanuni hizi, IEBC ilisema kuwa wagombeaji urais hawafai kutumia zaidi ya Sh4.4 bilioni katika kampeni zao (kila mgombea). Kwa upande mwingine vyama vya kisiasa havikuhitajika kutumia zaidi ya Sh17 bilioni kufadhili shughuli za kampeni.

Tume hiyo inasema kuwa kanuni hizo zililenga kuzuia uwezekano wa kuingizwa kwa pesa haramu katika kampeni za kuelekea uchaguzi mkuu na hivyo kutowatendea haki wagombeaji wasio na pesa nyingi.

Lakini sasa mswada huu mpya wa Bw Kioni unalenga kuondoa udhibiti wa jinsi wagombeaji watakavyokuwa wakitumia pesa nyakati za kampeni.

Kamati

Mswada huo ambao umekwisha kusomwa mara ya kwanza bungeni, pia unalenga kuondoa sheria inayovilazimisha vyama vya kisiasa kubuni kamati za kusimamia matumizi ya fedha zao za kampeni.

Kamati hiyo ya watu tisa ilipaswa kuwajibikia matumizi ya fedha za kampeni za kila mgombeaji aliyedhaminiwa na vyama husika vya kisiasa. Vyama vya kisiasa pia vilihitajika kubuni kamati kama hizo.

Wakati huu, kamati hizo zinahitajika kufungua akaunti ambayo itatumiwa kuweka fedha za kampeni.

Wagombeaji wa kujitegemea na wadhaminiwa wa kura za maamuzi pia wanahitaji kufungua akaunti na kuiarifu IEBC kila mara kuhusu jinsi fedha hizo zinavyotumika.

Lakini mswada wa Bw Kioni sasa unalenga kuzuia ukaguzi wa akaunti za wagombeaji na vyama vya kisiasa. Ukaguzi huo huendeshwa na Afisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

“Sheria ya awali inafanyiwa marekebisho kwa kuondoa sehemu ya 27,” mswada huo unasema.

Sehemu ya 27 ya sheria ya awali ilisema hivi: “Mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali, kupitia ombi la tume ya uchaguzi, atakagua akaunti zinazohusiana na matumizi ya fedha za kampeni za wagombeaji, vyama vya kisiasa au kamati za kupanga kura ya maamuzi.”

Mswada wa Bw Kioni sasa unapendekeza kwamba wagombeaji na vyama watahitajika kufichua kiwango cha fedha za kampeni na asili yake.

“Mgombeaji, chama cha kisiasa na kamati ya kura ya maamuzi atafichua, kitafichua au itafichua kiasi na vianzo vya michango iliyopatikana kwa ajili ya kufadhili kampeni za mchujo, uchaguzi au kura ya maamuzi au hali itakavyokuwa,” mswada huo unasema.

You can share this post!

Arsenal wacharaza Norwich City na kupunguzia kocha Arteta...

TAHARIRI: Lalama kuhusu CBC zisipuuzwe