• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
Kesi ya kumpinga Kavindu kuanza leo

Kesi ya kumpinga Kavindu kuanza leo

Na KITAVI MUTUA

MAHAKAMA Kuu ya Machakos Jumatatu inatarajiwa kuanza kusikiza kesi inayolenga kumzuia mgombeaji wa Wiper katika uchaguzi mdogo wa kaunti hiyo Agnes Kavindu Muthama kushiriki shughuli hiyo wiki hii.

Wapiga kura Wilfred Manthi Musyoka na Philippe Sadja waliwasilisha kesi hiyo wanadai Bi Muthama hajahitimu kielimu kuwania kiti wadhifa huo.Wanadai mgombeaji huyo wa Wiper alikiuka Sheria za Uchaguzi kwa kufeli kuwasilisha stakabadhi za uhitimu kutoka taasisi za elimu ya juu kwa Tume huru ya Uchaguzi Nchini (IEBC) alipokuwa akisaka uidhinishaji kuwania kiti hicho.

Kesi hiyo imeorodheshwa kuwa ya dharura.Musyoka na Sadja pia wamejumuisha IEBC na chama cha Wiper kama washtakiwa katika kesi hiyo.

“Hili ni suala ambalo linafahamika na umma. Naamini kuwa Bi Muthama hajahitimu kwa sababu hakupata alama hitajika katika shule ya upili kumwezesha kupata elimu ya juu,” Bw Musyoka anasema katika stakabadhi za kesi ambazo Taifa Leo ilipata.

Wapiga kura hao wawili wanadai kuwa uteuzi wa Bi Muthama na chama cha Wiper na uidhinishwaji wake na IEBC ni kinyume cha sheria na katiba na hivyo utapaswa kufutiliwa mbali.

Wanataka mwaniaji huyo azimwe kushiriki uchaguzi huo mdogo ambao umeratibiwa kufanyika Machi 18.Musyoka na Sadja wanasema kuwa sehemu ya 22 ya Sheria ya Uchaguzi inasema kuwa mwaniaji wa kiti cha ubunge na useneta sharti awe na uhitimu wa ngazi ya vyuo.IEBC ilipewa stakabadhi za kesi mnamo Alhamisi lakini asasi hiyo ikasema kesi hiyo imepitwa na wakati.

Mshirikishi wa uchaguzi katika afisi ya IEBC mjini Machakos Joyce Wamalwa anasema alizingatia sheria alipomwidhinisha Bi Muthama.

“Hii ni baada ya kuridhika kuwa mgombeaji huyo wa Wiper alitimiza mahitaji yote kulingana na Sheria za Uchaguzi. Wakati huu hitaji la masomo ya juu halijaanza kufanya kazi kwa hilo litatekelezwa kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022,” Bi Wamalwa akaambia Taifa Leo.

Mzozo unaozingira uhitimu wa kimasomo wa Agnes Kavindu unakumbusha jinsi mumewe wa zamani Johnston Muthama alilazimika kusaidiwa na mahakama kuweza kugombea useneta wa Machakos 2013. Inadaiwa kuwa Bw Muthama alikatiza masomo yake katika kiwango cha shule ya msingi.

Mnamo Oktoba 2011, aliwasilisha kesi mahakamani akipinga uhalali wa Sheria ya Uchaguzi 2011, iliyokuwa imepitishwa na Bunge la Kitaifa.Alidai sheria hiyo ilikwenda kinyume cha Katiba inayosema kila mtu ana haki ya kuwania kiti chochote cha kisiasa, bila kudhibitiwa kwa misingi ya uhitimu kimasomo.

Katika kesi yake, Bw Muthama alishtaki Waziri wa Haki na Masuala ya Kikatiba na Mwanasheria Mkuu.Mwanasiasa huyo aliambia mahakama kwamba hakufaa kuzuiwa kuwania kiti cha kuchaguliwa kwa misingi ya mahitaji ya Sheria ya Uchaguzi, kwa sababu masomo yake yalikomea kiwango cha shule ya msingi.

Alisema kuwa hakuendelea na masomo katika kiwango cha shule ya upili kwa kukosa karo.

You can share this post!

Wanaolengwa na chanjo ya crorona waingiwa na hofu

Nyota wa ‘Vuta Pumzi’ alifariki kutokana na...