• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 11:02 AM
Kesi ya vyeti feki yazidi kumwandama Samboja

Kesi ya vyeti feki yazidi kumwandama Samboja

Na JOSEPH WANGUI

AZIMIO la Gavana wa Taita Taveta, Bw Granton Samboja kuwania kiti hicho kwa kipindi cha pili mwaka ujao, sasa linaning’inia pabaya baada ya madai kuwa alitumia vyeti ghushi vya masomo kuibuka upya.

Bw Samboja ambaye ni mwanachama wa Wiper, katika miezi ya hivi majuzi amekuwa akiandamana kwa karibu na Kiongozi wa ODM, Bw Raila Odinga, hali ambayo iliibua mdahalo kuhusu uwezekano wake kuhamia chama hicho.

Masaibu yaliyokuwa yamemwandama kwa muda katika kipindi chake cha kwanza cha uongozi kilichoanza 2017, yameibuka tena baada ya Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kuunga mkono ombi la mwanaharakati Okiya Omtatah, anayetaka mahakama iamue kuwa vyeti vya Bw Samboja ni haramu.

Bw Omtatah alikuwa amewasilisha kesi hiyo Machi mwaka huu, siku chache baada ya Mahakama Kuu kutupa nje kesi nyingine kama hiyo iliyokuwa imewasilishwa na EACC dhidi ya gavana huyo.

Vyeti vinavyotiliwa shaka ni vya Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Upili (KCSE), diploma na digrii.EACC, wakati huo huo, imepinga ombi la Bw Samboja anayetaka kesi hiyo itupwe nje akidai kuwa masuala yaliyowasilishwa upya yalikuwa tayari yashaamuliwa na Jaji James Makau wa Mahakama Kuu.

Kulingana naye, tofauti iliyopo kati ya kesi iliyotupwa nje na ile iliyowasilishwa upya, ni majina ya wahusika. Bw Omtatah hakuwa mhusika katika kesi ile ya kwanza.

Vilevile, gavana huyo amedai kuwa suala hilo ni la kiuchaguzi na muda wa kusikiliza kesi za mizozo ya uchaguzi wa 2017 ulipita.Kupitia kwa wakili Jacky Kibogy, EACC inataka ombi la Bw Samboja lisikubaliwe na badala yake kesi iliyowasilishwa na Bw Omtatah isikilizwe hadi mwisho.

Bi Kibogy alisema kuwa kesi ya Bw Omtatah imeibua masuala kuhusu uadilifu wa gavana ambaye kimsingi, anafaa kufuata sheria za uadilifu chini ya Kifungu cha Sita cha Katiba.

“Omtatah amedai kuwa Bw Samboja alighushi vyeti vya kimasomo kusudi, na hivyo basi akadanganya kuhusu mafanikio yake ya kielimu na kupotosha umma ili apate nafasi za ajira. Hili ombi si la kiuchaguzi jinsi Bw Samboja anavyodai,” akasema Bi Kibogy.

Alieleza kuwa uchunguzi wa EACC ulikuwa umebainisha Bw Samboja hakuwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kenyatta alivyodai, na vyeti anavyotumia havikutoka katika chuo hicho, na Bw Omtatah anategemea kutumia ushahidi huo katika kesi yake.

Kuhusu msimamo wa Bw Samboja kuwa suala hilo tayari liliamuliwa na mahakama, EACC imesisitiza kuna masuala mageni yaliyowasilishwa na Bw Omtatah.

“Cha muhimu zaidi ni kuwa, masuala yaliyowasilishwa katika kesi iliyotangulia hayakusikilizwa kikamilifu kwa sababu mahakama ilitupa nje kesi hiyo kwa msingi wa kuwa korti haikuwa na mamlaka,” akasema Bi Kibogy.

Bw Omtatah ameambia mahakama kuwa alipitia stakabadhi za kesi hiyo ya awali akatambua kuwa Bw Samboja alikubaliwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuwania ugavana licha ya kuwa EACC ilisema vyeti vyake vya elimu vilikuwa ghushi.

Anasema kuwa kesi aliyowasilishwa inastahili kusikilizwa kwa kuwa ile ya awali iliyowasilishwa na EACC ilitupwa nje wakati mahakama iliposema haina mamlaka ya kuamua kuhusu kesi za uchaguzi.

You can share this post!

Lungu akubali rungu la Hichilema nchini Zambia

Rutto aonya ugatuzi utafeli kabisa iwapo mbinu zake...