• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 5:26 PM
Lungu akubali rungu la Hichilema nchini Zambia

Lungu akubali rungu la Hichilema nchini Zambia

Na AFP

MFANYABIASHARA tajiri ambaye pia ni kiongozi wa upinzani Hakainde Hichilema ametangazwa mshindi wa urais katika uchaguzi uliokuwa na ushindani mkali.

Hichilema alijizolea kura 2,810,757, na kumbwaga aliyekuwa rais Edgar Lungu aliyepata kura 1,814,201, kulingana na matokeo rasmi yaliyoripotiwa Jumatatu, kutoka jumla ya maeneobunge 155 of 156.

“Hivyo basi namtangaza Hakainde Hichilema kuwa rais aliyechaguliwa wa Jamhuri ya Zambia,”mwenyekiti wa tume ya uchaguzi, Jaji Esau Chulu, alisema kupitia taarifa iliyopeperushwa kwenye televisheni.

Ushindi huo uliibua nderemo na vifijo barabarani kufuatia uchaguzi ulioandamana na visa vya ghasia.Hichilema, alikuwa mkurugenzi katika kampuni ya ukaguzi wa vitabu vya fedha kabla ya kujitosa kwenye ulingo wa siasa.

Anakabiliwa na kibarua kigumu cha kukarabati mifumo ya kiuchumi katika taifa hilo ambalo ni moja kati ya mataifa maskini zaidi ulimwenguni.

Uchaguzi huo ulikuwa mara ya sita kwa Hichilema kugombea afisi ya rais na mara ya tatu kwake kumkabili Rais Lungu mwenye umri wa miaka 64.

Mnamo 2016, alishindwa na Lungu kwa karibu mno kwa takriban kura 100,000.Lungu amekuwa mamlakani kama rais kwa muda wa miaka sita.

Alijitosa debeni wakati uhasama ulipokuwa unazidi kuongezeka kuhusu kupanda kwa gharama ya maisha na msako mkali dhidi ya migawanyiko katika taifa hilo la Afrika Kusini.

Hichilema alijivunia uungwaji mkono kutoka kwa vyama 10 vya upinzani katika uchaguzi huo uliofanyika Alhamisi, kupitia chama chake cha United Party for National Development (UPND), ambacho ndicho kikubwa zaidi cha upinzani nchini Zambia.

Lungu alianza kuteta hata kabla ya mshindi kutangazwa akidai kuwa uchaguzi huo haukuwa huru wala wa haki kutokana na visa vya michafuko vilivyoripotiwa katika ngome za Hichilema.

Kupitia taarifa kutoka kwa afisi ya rais, alidai kuwa maajenti wake wa kuangazia uchaguzi walishambuliwa na kufukuzwa kutoka vituo vya kupigia kura.

Maafisa kutoka chama chake Hichilema cha UPND, walipuuzilia mbali taarifa ya Lungu wakiitaja kama inayotoka kwa watu “wanaojaribu kusambaratisha uchaguzi wote ili tu wakwamilie kazi zao.”

Kulingana na katiba ya Zambia, ikiwa Lungu anataka kutatua malalamishi hayo au kufutilia mbali matokeo ya uchaguzi, ni sharti awasilishe kesi katika Korti ya Kikatiba kabla ya siku saba kuisha baada ya mshindi kutangazwa.

Waangalizi wa kimataifa walipongeza jinsi chaguzi hizo zilivyoendeshwa kwa njia ya wazi na amani lakini wakakashifu kukatizwa kwa uhuru wa kukusanyika na kusafiri wakati wa kampeni za uchaguzi.

You can share this post!

Natembeya awatimua maafisa wa usalama

Kesi ya vyeti feki yazidi kumwandama Samboja