• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Mzozo wa madiwani na SRC kutatiza shughuli muhimu

Mzozo wa madiwani na SRC kutatiza shughuli muhimu

NA CHARLES WASONGA

HUENDA shughuli muhimu katika serikali za kaunti zikakwama kutokana na mvutano unaoendelea kati ya madiwani na Tume ya Mishahara Nchini (SRC) kuhusu nyongeza ya mishahara.

Hii ni baada ya mwenyekiti wa tume hiyo Lyn Mengich kupinga pendekezo la madiwani la kutaka mishahara yao iongezwe kwa kiwango cha asilimia 40 ya mishahara ya magavana.

Tayari zaidi ya mabunge 24 ya kaunti yamesitisha shughuli zao madiwani wakitaka waongezewe mishahara.

Wakati huu kila moja wa madiwani 1,450 hupokea mshahara wa Sh144,375 kila mwezi.

Kwa kuwa magavana sasa hupokea mishahara wa Sh924,000 kila mwezi, ina maana kuwa madiwani hao wanataka mshahahara wao uongezwe hadi Sh390, 270.

Alipofika mbele ya Kamati ya Seneti kuhusu Ugatuzi mnamo Alhamisi, Bi Mengich alisema vigezo vya utathmini wa kazi vilivyowekwa katika Katiba na Sheria ya SRC ya 2011 havisemi mishahara ya madiwani inafaa kukadiriwa kwa kuzingatia mishahara ya magavana.

“Hatukadirii mishahara ya maafisa wa serikali kwa ngazi fulani kwa kuzingatia mishahara ya maafisa wenye vyeo vya juu. Hatutumii kigezo kinachosema kwamba kwa sababu rais anapokea mshahara wa kiwango hiki, sharti tutumie kiwango hicho kukadiria mishahara ya wengine,” akawaambia wanachama wa kamati hiyo chini ya uenyekiti wa Seneta wa Homa Bay, Moses Kajwang.

Mnamo Juni 2023, SRC iliongeza mshahara wa kila diwani kwa Sh10,000 kutoka Sh144,375 hadi Sh154,481 kuanzia mwezi huu wa Julai.

Kulingana na nyongeza hiyo, ambayo itatekelezwa kwa awamu mbili, madiwani watapokea mshahara wa Sh165,588 katika mwaka wa kifedha wa 2024/2025.

Hata hivyo, wamepinga nyongeza hiyo wakisema SRC haikuzingatia haki.

“Tulichunguza upya majukumu yote ya madiwani kwa usaidizi wa wataalamu wetu. Tulirudia shughuli hiyo mara tano lakini mshahara wa madiwani ulisalia katika kundi D4. Hiyo ndio maana mshahara wao umesalia katika kiwango hicho,” akasema mwenyekiti wa SRC Amani Komora.

Katibu Mkuu wa Muungano wa Mabunge ya Kaunti (CAF) Chege Mwaura aliitaka SRC kusitisha utekelezaji wa nyongeza ya mishahara ya mwaka wa kifedha wa 2023/2024 hadi mvutano huo utakapomalizwa na muafaka kupatikana.

“Tunaitaka SRC kusimamisha utekelezaji wa nyongoze hiyo ya mishahara hadi kamati hii ya seneti kuhusu ugatuzi itakaposuluhisha suala hili,” akasema Bw Mwaura ambaye ni diwani wa wadi ya Ngara, Kaunti ya Nairobi.

Naye Katibu Mkuu wa Muungano wa Mabunge ya Kaunti Stanley Karanja alisema mabunge ya kaunti hutengewa fedha za kutosha kufanikisha nyongeza ya mishahara wanayotaka.

 Zaidi ya mabunge 24 yamesitisha shughuli yakilalamikia nyongeza ya mishahara.

Maseneta Samson Cherargei (Nandi), Mohammed Chute (Marsabit) na Seneta Maalum Peris Tobiko wameunga mkono shinikizo la madiwani la kutaka SRC iwaongezee mishahara.

  • Tags

You can share this post!

Kibarua cha Raila Sabasaba ikiwadia

Cynthia Wanjala apigwa breki katika awamu ya robo-fainali...

T L