• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 2:00 PM
Kibarua kizito kwa ‘warithi’ 4 wa Joho

Kibarua kizito kwa ‘warithi’ 4 wa Joho

Na WINNIE ATIENO

WANASIASA wanne wanaowania kumrithi Gavana wa Mombasa, Hassan Joho katika uchaguzi wa Agosti 2022 wameanza kuwatafuta wapiga-kura wakiendeleza kampeni za kushawishi wapiga kura.

Kiti hicho kimevutia wanasiasa watano wakiwemo mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir (ODM), naibu gavana wa Mombasa William Kingi (ODM), bwanyenye Suleiman Shahbal (ODM), aliyekuwa senata wa Mombasa Hassan Omar (UDA) na mbunge wa Kisauni Ali Mbogo (Wiper).

Hata hivyo, wadadisi wa siasa wanasema atakayeshinda tikiti ya ODM ndiye atakayekuwa na nafasi bora ya kutwaa ugavana.

Tikiti ya ODM inamezewa mate na Bw Nassir, naibu gavana wa Mombasa Kingi na Bw Shahbal ambaye alijiunga na chama hicho hivi majuzi.

Gavana Joho anayehudumu muhula wake wa mwisho hajatangaza anayemuunga mkono lakini naibu wake ana imani atapata tiketi hiyo.

“Chama cha ODM bado ni maarufu sana katika Kaunti ya Mombasa, ndiyo maana itakuwa rahisi kwa yeyote atakayeshinda tiketi hiyo kuwa gavana. Jiulize kwa nini wagombea wengi wanamenyania tiketi hiyo,” alisema Bw Philip Mbaji mdadisi wa siasa.

Hata hivyo, Bw Mbaji alisema Bw Nassir ana uwezo mkubwa wa kushinda tiketi ya ODM sababu amekuwa katika chama hicho tangu aingie katika siasa.

“Ugavana wa Mombasa ni wa farasi wawili tu, ni kati ya Bw Shahbal na Bw Nassir. Ukilinganisha Bw Shahbal na Bw Nassir, Bw Nassir ana nafasi kubwa sana ya ushindi sababu ya urafiki wake wa karibu na kinara wa ODM Raila Odinga, lakini Bw Shahbal aliingia ODM majuzi tu kutoka Wiper na hata Jubilee, ametangatanga vyama vingi, sana hii inamanaisha hana msimamo,” Bw Mbaji aliongeza.

“Bw Nassir ni mwanasiasa mzoefu wa ODM katika Kaunti ya Mombasa. Lakini Bw Shahbal alipata pigo kubwa sana baada ya maseneta kusimamisha mradi wake wa Sh6 bilioni, anafaa kujisafisha kwa umma. Kwa sasa anaonekana vibaya mbele ya umma baada ya ubomozi wa majumba,” alisema.

Lakini mchanganuzi huyu asema Bw Shahbal ni stadi wa kufanya kampeni vijijini.

“Bw Mbogo, Dkt Kingi na Bw Omar wana kibarua kigumu sana, tumebakia na miezi 11 kabla ya uchaguzi mkuu, muda umeyoyoma. Lakini Bw Omar anafaa kuwakumbusha wapiga kura anachokitaka. Chama cha ODM ndio kusema Mombasa, atakayepewa tikiti ndiye gavana,” alisema.

Bw Mbaji aliwashauri Bw Mbogo na Dkt Kingi, kushirikiana ili kuzoa kura za Wamijikenda.

Lakini Dkt Kingi ana imani kuwa atapata tiketi ya ODM na kushinda kiti hicho.

“Kutokana na tajriba yangu uongozini kama naibu gavana, nimeamua kujitosa kwenye siasa ili nimalize miradi yetu na Gavana Joho,” alisisitiza huku akipinga madai kuwa alishurutishwa kugombea kiti hicho na mabwanyenye wa Mombasa.

Kibarua chake kikubwa ni kupambania tiketi ya ODM na Bw Shahbal na Bw Nassir.

Bw Mbogo ambaye pia amekita kambi vijijini katika maeneobunge ya Mvita, Changamwe, Likoni, Nyali na Jomvu anaendelea ‘kuuza’ manifesto yake akiapa kushughulikia masuala ya elimu, afya na barabara.

You can share this post!

Vilio vya Muturi, Waiguru vyazua maswali mengi

Wasiwasi KRA ikifunga akaunti za chuo kikuu kwa deni kuu