• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 6:55 PM
Kibwana alia kuwekewa vizingiti katika kampeni za Azimio Ukambani

Kibwana alia kuwekewa vizingiti katika kampeni za Azimio Ukambani

NA CHARLES WASONGA

GAVANA wa Makueni Kivutha Kibwana amejiondoa kutoka shughuli za kuvumisha muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya katika eneo la Ukambani.

Kupitia ujumbe katika akaunti yake ya Twitter Jumatano, Aprili 20, 2022 Profesa Kibwana alisema kuwa hatua hiyo imechangiwa na kile alichokotaja kama usumbufu kutoka kwa kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka.

Alisema imekuwa vigumu kumfanyia kampeni mgombeaji urais wa Azimio Raila Odinga katika eneo pana la Ukambani kutokana na “vizingiti ninavyowekewa na Kalonzo”.

“Imekuwa vigumu kwangu kufanya kazi na Kalonzo katika muungano wa Azimio eneo la Ukambani. Baada yake kujiunga nasi amekuwa akishinikiza kuwa niondoke kutoka asasi mbalimbali za Azimio,” Profesa Kibwana akaeleza.

Gavana huyo sasa anasema atajitenga na shughuli za Azimio la Umoja-One Kenya kwa sababu ya “kumulikwa kila wakati bila sababu na Bw Kalonzo.”

Kiongozi huyo wa Wiper amekuwa akipinga kujumuishwa kwa viongozi wa vyama vidogovidogo vilivyoko ndani ya Azimio katika baraza kuu la muungano huo.

Wiki iliyopita Bw Musyoka na wandani wake walimsuta mwaniaji urais kwa tiketi ya Azimio, Raila Odinga, kwa kuongeza idadi ya wanachama wa baraza hilo kutoka saba hadi 12 ili kushirikisha viongozi wa vyama vidogo.

Wiki jana, Profesa Kibwana alimtaka Bw Musyoka kufanya kazi na viongozi wengine kutoka Ukambani kunadi Azimio, akisema vyama vyote vinavyomuunga mkono Bw Odinga sharti viruhusiwe kumfanyia kampeni.

Gavana Kibwana ni kiongozi wa chama cha Muungano ambacho ni kimojawapo cha vyama tanzu katika Azimio, na alisema vyama vyote viruhusiwe kuendesha kampeni bila kukabiliwa na vikwazo kutoka kwa vyama vingine.

“Huu uhasama wa zamani mingoni mwa vyama vilivyoko katika Azimio usiwe kikwazo katika mchakato wa kuendesha kampeni za kumpigia debe Bw Odinga,” akasema Profesa Kibwana.

“Azma ya mwaniaji urais yeyote yule ni kupata kura nyingi kiasi cha kutosha. Kwa hivyo, vyama vyote vinavyounga mkono Bw Odinga vinafaa kuruhusiwa kuendesha kampeni bila vikwazo. Kalonzo anafaa kukumbatia watu wote sio hii falsafa ya kiti chenye miguu mitatu. Ukambani kuna jumla ya wapiga kura 2.5 milioni, ndani na nje ya eneo hilo,” Profesa Kibwana akasema wiki jana.

Hata hivyo, Gavana huyo wa Makueni alisema kuwa ataendelea kumfanyia kampeni Bw Odinga bila kushirikiana na Bw Musyoka.

  • Tags

You can share this post!

Washukiwa watatu wa mauaji ya mwanafunzi wa JKUAT kusalia...

Arteta akiri hajakuwa akimtendea Nketiah haki kwa kumlisha...

T L