• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 3:16 PM
KIGODA CHA PWANI: Umoja wa Pwani kusalia ndoto isiyotimilika milele

KIGODA CHA PWANI: Umoja wa Pwani kusalia ndoto isiyotimilika milele

NA PHILIP MUYANGA

TAKRIBANI siku nane zimesalia kabla ya Wakenya kuelekea kwenye uchaguzi mkuu lakini kwa wakazi wa Pwani, suala la umoja wa viongozi wao katika siasa limebakia tu kuwa ndoto.

Hii ni kwa sababu ya kuwa kila wakati, mwaka mmoja au miezi kadhaa kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika, mikutano mingi huandaliwa kila pembe ya ukanda wa Pwani, wenye kaunti sita, huku viongozi wakitafuta umoja huo baina yao.

Wakati huu wa uchaguzi mambo hayajakuwa tofauti kwani kuanzia mwaka 2021, mikakati mingi imepangwa na baadhi ya viongozi wa kijamii na kisiasa kwa madhumuni ya kuunganisha ukanda huu ili uwe na usemi mmoja katika upigaji kura.

Baadhi ya wanasiasa ambao hujadili umoja wa Pwani kila kukaribiapo uchaguzi mkuu hudai kuwa muungano wa kisiasa wa jamii za Wapwani ndio unaoweza kuwatoa katika lindi la upweke wa siasa za kitaifa.

Hata hivyo, shughuli na mikakati hiyo huisha kabisa wakati wa kura za mchujo kwani viongozi wengi hufuata njia tofauti huku kila mmoja akifuata chama chake cha kisiasa na maslahi yake ya kibinafsi huku akiwaacha wakazi wa Pwani bila msimamo wowote wa kisiasa.

Wachanganuzi wa siasa za Pwani wanasema kuwa umoja unaotajwa kila mara uchaguzi unapowadia utabaki kuwa ndoto iwapo hakutaundwa mikakati mwafaka inayohusisha wakazi ili kusaidia kuzindua na kuendeleza umoja huo.

Wanasema kuwa tofauti na sehemu nyingine nchini ambazo zinaonekana kuwa na umoja wa kisiasa, eneo la Pwani lina makabila mengi ndiposa umoja huo unaonekana kutofaulu.

Baadhi ya vyama vyenye mizizi yake Pwani vilionekana kuwa na nia ya kuunganisha wakazi wa Pwani lakini mikakati hiyo ilionekana kutofaulu.

Vyama vya Communist Party of Kenya,Shirikisho Party,Kadu Asili,Umoja Summit na Republican Congress Party vilikuwa vimeonakana kuwa vitaungana na kuwasilisha wagombeaji wa viti mbalimbali chini ya mwavuli mmoja lakini jambo hilo halikutimia.

Kuanzishwa kwa chama cha Pamoja African Alliance (PAA) na Gavana wa Kilifi, Bw Amason Kingi kulionekana kutwaa jukumu la kuunganisha jamii ya Wapwani kisiasa.

Hata hivyo, licha ya kuwa na wagombeaji wa viti katika sehemu mbalimbali za ukanda wa Pwani,hakijaweza kuunganisha Wapwani wote ilivyotarajiwa.

Mwaka 2021 katika mkutano ulioleta pamoja baadhi ya wafuasi wa chama hicho mjini Mombasa, Bw Kingi alisema kuwa kila kona ya nchi watu wanajipanga na kwamba wakati wa eneo la Pwani kujipanga umewadia.

“Tumezoea kupangwa, wakati sasa umefika tujipange sisi wenyewe,” akasema Gavana Kingi katika mkutano huo.

Akizungumza pia katika mkutano huo, aliyekuwa mbunge wa Malindi, Bw Lucas Maitha alisema kuwa ni lazima wakazi wa Pwani waingie katika uchaguzi ujao wakiwa katika chama kimoja.

Bw Maitha alisema kuwa vyama walivyokuwa navyo hapo awali havijawatumikia Wapwani ipasavyo.

Kulingana na mshauri wa masuala ya siasa, Bw Bozo Jenje, umoja wa kisiasa wa Pwani utasalia kuwa ndoto kwani baadhi ya wanasiasa wanadhani kuwa wakibakia katika vyama vinavyojulikana watachaguliwa.

Bw Jenje anasema kuwa chama cha PAA kimeshindwa kuleta umoja wa kisiasa katika ukanda wa Pwani kwa kuwa malengo yake hayakuwa hayo.

“Chama hicho kilizinduliwa baada ya kuasi chama cha Orange Democratic Movement (ODM). Kilipoundwa, vyama vingine vilivyokuwa na viongozi kama magavana, wabunge na maseneta walikataa kubanduka,” akasema Bw Jenje.

Prof Hassan Mwakimako, ambaye pia ni mchanganuzi wa siasa, anasema kuwa suala la umoja wa Pwani linapendwa na wananchi lakini tatizo huwa ni nguvu ya kujipanga.

Anaongeza kuwa wanasiasa hulitumia suala hilo kwa manufaa yao wenyewe bila kujali maslahi ya wapiga-kura au wananchi.

Prof Mwakimako anaongeza kuwa tatizo kubwa ni kuwa wananchi wanafikiria kwamba umoja huo wa wa Pwani utaletwa na wanasiasa.

“Viongozi wa kisiasa wa Pwani hawawezi kuleta umoja huo unaosemwa,jamii za Pwani zinafaa kujipanga na kuleta umoja huo kupitia mabaraza ya uongozi wa kila jamii,” asema Prof Mwakimako na kuongeza kuwa kila jamii ilikuwa na baraza la kuiongoza wala hapakuwa na kiongozi mmoja anayeongoza isipokuwa baraza hilo.

Prof Mwakimako anasema kuwa baadhi ya viongozi hawakuongea kuhusu umoja wa Pwani wakati vikundi kadhaa vya kijamii vilipokuwa vinajadiliana lakini waliunda vyama vyao kama vyombo vya kujiendeleza kisiasa.

Baadhi ya wanasiasa wa Pwani ambao wako katika vyama au miungano inayosemekana kuwa ya kitaifa wanadai kuwa Pwani haiwezi kujiendeleza na kusimama peke yake bila kujihusisha na jamii nyingine nchini.

Hata hivyo, wachanganuzi wa siasa za ukanda wa Pwani wanasema kuwa umoja wa kisiasa wa viongozi ndio unaoweza kuupa ukanda wa Pwani nafasi kuu ya kutetea wananchi katika mgao wa rasilimali za kitaifa nchni.

Baadhi ya viongozi wanaopigia chapuo wazo hilo ni Gavana wa Mombasa, Ali Hassan Joho (ODM) na mwenzake wa Kwale, Gavana Salim Mvurya (UDA).

Aidha, mumo humo yumo pia mbunge wa Malindi, Aisha Jumwa (UDA).

Kwa sasa wananchi wanasubiri iwapo viongozi watakaochaguliwa wataweza kuyapatia kipao mbele maswala yanayokabili ukanda wa Pwani.

  • Tags

You can share this post!

Mahafali 6,500 wafuzu vizuri kwenye sherehe ya kufana MKU

Mashirika, viongozi wa kidini wataka IEBC kuzingatia...

T L