• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 4:10 PM
Kilichosukuma Ruto kuteua wanasiasa wengi mawaziri

Kilichosukuma Ruto kuteua wanasiasa wengi mawaziri

NA CHARLES WASONGA

RAIS William Ruto ameamua kuteua idadi kubwa ya wanasiasa, kuliko wataalamu, katika baraza lake la mawaziri kutokana weledi katika kufafanua ajenda za serikali yake kwa wananchi.

Aidha, kulingana na wadadisi, kwa kuteua wanasiasa wengi kuwa mawaziri Dkt Ruto analenga kusuka kundi litakalomsaidia kushinda urais mwa muhula wa pili, 2027 kwa urahisi.

“Maswali mengi yameibuka kuhusu ni sababu zipi zilizochangia Rais kuamua kuteua wanasiasa wengi kuwa mawaziri, tofauti na mtangulizi wake, Uhuru Kenyatta. Ukweli ni kwamba hawa ndio watu ambao wanaweza kumsaidia kuelezea sera za serikali yake kwa ufasaha kuliko wataalamu,” anasema mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Moi, Prof Masibo Lumala.

Manifesto

Prof Lumala ambaye ni mchanganuzi wa masuala ya kisiasa na uongozi, anaongeza kwa kusema: “Mbali na hayo, Rais ameonyesha dalili kuwa anawataka watu ambao watakuwa na manufaa makubwa kwake atakapotetea kiti chake, 2027.”

Bw Martin Andati anashikilia uzi uo huo anapoelezea kuwa Rais amewateua wanasiasa kwa sababu hawa ndio wanaoweza kutangamana na wananchi kwa ukaribu na “hivyo kuelezea utendakazi wa serikali kufungamana na manifesto yao.”

“Ukichunguza kwa makini, wanasiasa ambao Dkt Ruto amewateua ni miongoni mwa wale ambao alikuwa akizunguka nao kote nchini akiuzua mfumo wa kiuchumi wa kuinua maisha ya walalahoi. Bila shaka ni wao walio katika nafasi bora ya kutekeleza mfumo huo na ajenda zote zilizo katika manifesto ya Kenya Kwanza,” Bw Andati anaeleza.

Kwenye orodha ya watu 22 waliopendekezwa kushikilia nyadhifa za uwaziri katika serikali yake ya Kenya Kwanza, 17 ni wanasiasa.

Kati yao ni seneta mmoja, wabunge wawili na wanasiasa waliowania nyadhifa mbalimbali katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9, lakini wakabwagwa.

Wandani

Wanasiasa hao wanajumuisha wandani wa karibu wa Dkt Ruto Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen (ambaye amependekezwa kuwa Waziri wa Uchukuzi), Mbunge wa Kandara Alice Wahome (Maji), Mbunge wa Garissa Mjini Aden Duale (Ulinzi) na aliyekuwa Seneta wa Tharaka Nithi Kithure Kindiki (Usalama wa Ndani).

Wengine ni aliyekuwa Seneta wa Meru Mithika Linturi (Kilimo), aliyekuwa Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi (Mwanasheria Mkuu), aliyekuwa Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa (Utumishi wa Umma na Jinsia), aliyekuwa Gavana wa Machakos Alfred Mutua (Masuala ya Kigeni) na Kiongoni wa ANC Musalia Mudavadi (Mkuu wa Mawaziri), miongoni mwa wengine.

Seneta Murkomen, Bw Duale pamoja na Bi Wahome watalazimika kujiuzulu nyadhifa zao katika seneti na bungeni, mtawalia.

Hii ni kwa sababu kulingana na kipengele cha 152 (3) mawaziri hawapaswi kushikilia nyadhifa za kisiasa.

Nao Bw Mudavadi na Dkt Mutua watajizulu kama viongozi wa vyama vya ANC na Maendeleo Chap Chap (MCCP) kwa msingi huo huo.

Mawaziri wateule watano pekee ndio ambao hawajawahi kushiriki siasa za kushindania viti katika uchaguzi mkuu mwaka huu au chaguzi za awali. Wao ni Davis Chirchir (Kawi), Rebecca Miano (Jumuiya ya Afrika Mashariki), Simon Chelugui (Vyama vya Ushirika), Zacharia Mwangi (Ardhi) na Prof Njuguna Ndung’u (Fedha).

Hii ni tofauti kabisa na baraza la kwanza la mawaziri la Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, aliyeteua idadi kubwa ya wataalamu. na wanasiasa wawili pekee.

Wanasiasa hao walikuwa ni kiongozi Narc Charity Ngilu (Ardhi) na aliyekuwa kiongozi wa chama cha Republican Council of Kenya (RCK) Najib Balala.

Baada ya kung’amua udhaifu wa wataalamu katika kuelezea sera za serikali, Rais Kenyatta na Dkt Ruto (kama Naibu Rais) walioamua kuongeza idadi ya wanasiasa katika serikali yake baada ya uchaguzi mkuu wa 2017.

Wao ni aliyekuwa Mbunge wa Saboti Eugene Wamalwa (aliyeteuliwa Waziri wa Ugatuzi), mwanaharakati wa kisiasa Rashid Echesa (Michezo) na aliyekuwa Gavana wa Marsabit Ukur Yatani (Fedha).

Wengine walikuwa aliyekuwa Gavana wa Meru Peter Munya na aliyekuwa Mbunge wa Laikipia Mashariki Mwangi Kiunjuri (Kilimo) na aliyekuwa Seneta wa Nyeri Mutahi Kagwe (Afya).

Wakati wa utawala wa Uhuru, wa miaka 10, wengi wa mawaziri wasio wanasiasa walihofia kufika mbele ya kamati za bunge kujibu masuali kutoka kwa wabunge.

Aidha, ilikuwa nadra kwa baadhi yao kuzunguka nyanjani kufafanua mipango na miradi ya serikali kwa wananchi.

Baada ya kung’amua ulegevu huu, Dkt Ruto, mnamo Agosti 17, alitangaza wazi katika serikali yake, mawaziri watakuwa wakifika bungeni kujibu maswali kutoka kwa wabunge.

“Serikali ya Kenya Kwanza itapendekeza sheria za bunge zifanyiwe marekebisho ili mawaziri wawe wakifika bungeni kujibu maswali. Kwa njia hii serikali yetu itawajibika kwa wananchi kupitia wawakilishi wao, tofauti na hali ya sasa ambapo mawaziri hufika katika kamati za bunge pekee,” Dkt Ruto akasema alipokuwa na viongozi waliochaguliwa kwa tiketi ya vyama tanzu katika makazi ya Naibu Rais, Karen Nairobi.

Bw Andati anasema baada ya mawaziri wateule, ambao wamekuwa wanasiasa, kuidhinishwa na wabunge, ajenda za serikali ya Dkt Ruto zitashughulikiwa kwa urahisi ndani na nje ya bunge.

  • Tags

You can share this post!

‘Tatizo la vijana kukosa kazi lastahili...

Kibarua cha kusimamia serikali ya robo mkate

T L