• Nairobi
  • Last Updated April 17th, 2024 5:55 AM
Kiunjuri ajipendekeza kuwa naibu wake Ruto

Kiunjuri ajipendekeza kuwa naibu wake Ruto

Na JAMES MURIMI

KIONGOZI wa chama cha The Service Party (TSP), Bw Mwangi Kiunjuri amesema ndiye mwanasiasa kutoka Mlima Kenya anayefaa zaidi kuwa mgombea-mwenza wa Naibu Rais William Ruto kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Bw Kiunjuri alisema ana tajriba ya kisiasa ya miaka mingi, hivyo atatumia chama chake kupiga jeki azma ya Dkt Ruto kuwania urais mwaka 2022.

Kwenye mahojiano na ‘Taifa Leo’ Jumatatu, Bw Kiunjuri, ambaye alihudumu kama Waziri wa Kilimo, alisema atatumia chama chake kuhakikisha ametwaa nafasi hiyo.

“Nimekuwa katika siasa za Kenya kwa muda mrefu. Viongozi wa kisiasa ambao wananizidi kitajriba katika ukanda wa Mlima Kenya ni Bw Kiraitu Murungi na Bi Martha Karua pekee. Yule ambaye atakuwa naibu rais ataidhinishwa na Mungu. Hakuna mwanadamu anayeweza kugeuza mpango wa Mungu,” akasema Bw Kiunjuri.

“Tutatumia chama chetu kufikisha siasa zetu katika kiwango cha kitaifa. Rais na Naibu Rais ni marafiki wangu wa karibu. Huwa waniomba ushauri kila mara wanapohitaji maelezo ya kina kuhusu mwelekeo wa kisiasa katika eneo hilo,” akaongeza.

Hata hivyo, mbunge Rindikiri Mugambi (Buuri) alisema chama cha UDA ambacho kinahusishwa na Dkt Ruto hakijamtaja mtu yeyote atakayeidhinishwa kuwa mgombea-mwenza wa Dkt Ruto.

“Niko katika UDA na hatujamwidhinisha yeyote kuwa mgombea-mwenza wa Dkt Ruto. Chama cha Jubilee kilisambaratika kitambo na sasa lengo la serikali ni kumhangaisha mwananchi kwa kuongeza ushuru kwa bidhaa za msingi. Serikali ya Jubilee haina huruma kwa mwananchi,” akasema Bw Mugambi.

Bw Kiunjuri alipuuzilia mbali mipango ya baadhi ya viongozi kubuni miungano ya kisiasa kabla ya uchaguzi ujao.

“Wakenya wataamua ikiwa ninafaa kuhudumu katika mojawapo ya nafasi za juu za uongozi. Ninawaomba Wakenya kuniombea na wajiunge na TSP. Daima, nimekuwa mwanasiasa mkweli katika safari yangu ya kisiasa. Ni sababu hiyo ambapo Rais na naibu wake huwa wananiamini.”

You can share this post!

Viongozi wataka wanawake Waislamu wasikubaliwe kuabiri...

Wanawake watwaa majukumu ya kiume wazee wakilewa tu!