• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
Kundi lataka wandani wa Raila na Ruto wazuiwe kugombea vyeo Agosti 9

Kundi lataka wandani wa Raila na Ruto wazuiwe kugombea vyeo Agosti 9

NA CHARLES WASONGA

WANDANI wa wagombeaji wakuu wa urais Naibu Rais William Ruto na Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga ni miongoni mwa wanasiasa 24 ambao Jumapili walitajwa kama watu wasiofaa kuwania nyadhifa katika uchaguzi mkuu ujao kwa utovu wa maadili.

Muungano wa mashirika ya umma Jumapili uliwataja mgombea mwenza wa Dkt Ruto, Rigathi Gachagua, Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru, Seneta wa Kakamega Cleophas Malala, Mbunge wa Malindi Aisha Jumwa, Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi, miongoni mwa wengine, kama watu wasiofaa kuidhinishwa kuwania viti katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Chini ya mwavuli wa vuguvugu la kitaifa la kutetea maadili (National Integrity Alliance-NIA) mashirika hayo pia yalitoa wito kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kutowaidhinisha wandani wa Bw Odinga, Babu Owino (Mbunge wa Embakasi Mashariki), Gavana wa Busia Sospeter Ojaamong, Samuel Arama (Nakuru Magharibi) na Philip Kaloki ambaye ni mgombea mwenza wa wadhifa wa ugavana wa Nairobi.

Bw Ojaamong’ anayekabiliwa na tuhuma za ufisadi ametangaza kuwa anawania kiti cha ubunge cha Teso Kusini kwa tiketi ya chama cha ODM.

Orodha hiyo ya NIA pia inajumuisha waliokuwa magavana wa Nairobi Mike Sonko, anayewania ugavana wa Mombasa kwa tiketi ya Wiper na Dkt Evans Kidero anayewania uigavana Homa Bay kama mgombea wa kujitegemea.

Walisema wanasiasa hao wamekiuka hitaji la Sura ya Sita ya Katiba kuhusu Maadili na Uongozi bora na hivyo hawapaswi kushikilia nyadhifa za umma.

“Wanasiasa hawa ambao tumewataka wamehusishwa na kashfa mbalimbali na kesi zao ziko mahakamani au zinashughulikiwa na asasi mbalimbali za umma za kupambana na utovu wa maadili. Kwa hivyo, hawafai kuruhusiwa kuwania nyadhifa za umma,” Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mzalendo Trust Caroline Geita akasema.

Alikuwa ameandamana na Mkurugenzi Mkuu wa shirika la kupambana na ufisadi, Transparency International (TI) Sheila Masinde, Mkurugenzi wa shirika la kuteta haki za kibinadamu (KHRC) Davis Malombe na mshirikishi wa kitaifa wa shirika la The Institute of Social Accountability (TISA) Wanjiru Gikonyo.

Chini ya mwavuli wa Muugano wa Kitaifa wa Kutetea Maadili (National Intergrity Alliance) watetezi hao wa haki na utawala bora walizindua kampeni kwa jina “Red Card Campaign 2022” kuzuia watu waliopotoka kimaadili.

  • Tags

You can share this post!

Sababu za Karua kukwepa Uhuru

Kevin de Bruyne na Phil Foden washinda tuzo za Mchezaji...

T L