• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Kutimuliwa kwa wabunge chamani ODM kwaibua wameza mate

Kutimuliwa kwa wabunge chamani ODM kwaibua wameza mate

NA KASSIM ADINASI

KUTIMULIWA kwa Mbunge wa Gem Elisha Odhiambo kutoka kwa chama cha Orange Democratic Movement (ODM), pamoja na wabunge wengine kadha, kumeleta hisia mseto, huku dalili za kampeni za mapema kuelekea mwaka 2027 zikianza kujichora.

Sasa baadhi ya viongozi wameanza kukimezea mate kiti cha mbunge huyo wa muhula wa pili.

Meneja wa Jiji la Kisumu Abala Wanga, Mwanachama wa Bodi ya Umma ya Kaunti ya Siaya Otieno Rading na naibu mwenyekiti wa chama cha Communist Party of Kenya (CPK) Booker Ngesa Omole ni miongoni mwa viongozi ambao wako kwenye mstari wa mbele wakitaka kiti hicho.

Naibu mwenyekiti wa chama cha Communist Party of Kenya (CPK) Booker Ngesa Omole. PICHA | MAKTABA

Eneobunge la Gem katika Kaunti ya Siaya ni mojawapo ya maeneo ambayo chama cha ODM kinajivunia uungwaji mkono mkubwa huku wapigakura wengi eneo hilo wakimtambua kiongozi wa chama hicho, Raila Odinga, kuwa ndiye kigogo wa siasa za Luo Nyanza.

Akiwa tayari ameegemea mrengo tawala wa Kenya Kwanza, Bw Odhiambo atalazimika kupiga kampeni kali kuyeyusha umaarufu wa Bw Odinga endapo atataka kuingia bungeni kwa mara ya tatu.

Seneta wa Siaya Oburu Oginga akiwa kwenye hafla moja katika eneobunge la Gem, alisema Bw Odhiambo alionyesha usaliti mkubwa wakati Raila alikuwa anakabiliwa na kuandamwa na mahasimu wake katika siasa.

“Wakati kiongozi wetu wa chama alikuwa anakabiliwa na wakati mgumu, alituhitaji sana tumuunge mkono, lakini baadhi ya viongozi hapa nyumbani walimsaliti,” akasema seneta Oginga.

Kama viongozi wengine wa ODM wanaoshirikiana na Rais William Ruto, Bw Odhiambo anasema haja yake ni kuhakikisha wakazi wa Gem wanapata maendeleo.

“Tunataka barabara, maji safi na stima hapa Gem. Ufadhili mzuri wa miradi ya aina hii hutoka kwa serikali kuu,” akasema nyumbani kwake alipoalika baadhi ya wapigakura wa eneo hilo nyumbani kwake, akionyesha kutotishwa kwa kufukuzwa chamani.

Alijifananisha na dhahabu.

“Dhahabu hung’aa baada ya kupitishwa kwa tanuri la moto mkubwa, na yanayotokea kwangu na kwa viongozi wenzangu ni mapito yatakayotuimarisha kisiasa. Tayari haya yanajiri wakati Luo Nyanza tunatafuta mrithi wa kuchukua nafasi ya kigogo wa eneo. Bila shaka mahakama na jopo la kutatua migogoro ya kisiasa litatoa uamuzi wa busara,” akasema Bw Odhiambo aliyechaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2017 baada ya kumbwaga marehemu Jakoyo Midiwo kwenye mchujo wa ODM.

Wengine waliotimuliwa ni Seneta wa Kisumu Tom Ojienda, wabunge; Felix Odiwuor (Langata), Caroli Omondi (Suba Kusini), na Gideon Ochanda (Bondo).

Nao Mark Nyamita (Uriri) na Paul Abuor (Rongo) watatakiwa kulipa faini ya Sh1 milioni kila mmoja na kutuma barua za kuomba msamaha.

Naye Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Nairobi Esther Passaris kwa kuunga mkono Mswada wa Fedha wa 2023 uliopisha Sheria ya Fedha ya 2023, aliamuriwa alipe faini ya Sh250,000.

Shoka pia liliwateremkia madiwani wa Bunge la Kaunti ya Kisumu ambao uteuzi wao ulifutwa. Madiwani hao ni Caroline Opar, Kennedy Ajwang, Peter Obaso na Regina Kizito kwa kukiuka utaratibu wa chama cha ODM.

  • Tags

You can share this post!

Tatu City yashirikiana na miungano ya kibiashara ya China

Wenye hoteli zilizogeuka magofu Malindi waambiwa...

T L