• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 5:59 PM
Mahakama yampa Sonko matumaini ya kuwa debeni

Mahakama yampa Sonko matumaini ya kuwa debeni

NA PHILIP MUYANGA

MATUMAINI ya Gavana wa zamani wa Nairobi Mike Sonko kuwania kiti cha ugavana katika Kaunti ya Mombasa jana Jumatatu yalipigwa jeki baada ya Mahakama Kuu kusitisha kuchapishwa kwa majina ya wawaniaji wa wadhifa huo kwenye gazeti rasmi la serikali.

Mahakama iliamuru Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini (IEBC) isichapishe majina hayo hadi kesi aliyowasilishwa Bw Sonko isikizwe na kuamuliwa.

Uamuzi wa majaji hao watatu Justices Olga Sewe, Stephen Githinji na Ann Ong’injo sasa unaizuia IEBC kuendelea na mpango wake wa kuchapisha majina ya wawaniaji.

Bw Sonko ambaye alikuwa kortini aliahidi kuwa hatakata tamaa hadi kile anachodai ni haki itendeke kwa chama chake cha Wiper na wapigakura wa kaunti ya Mombasa.

“Nimefurahia amri hii. Ingawa bado hatujashinda, angalau sasa naona haki itatendeka. Tuipe mahakama muda na nina imani mwishowe tutashinda,” akasema Bw Sonko.

Korti pia ilitoa amri kuwa Wiper isimteue mwaniaji mwingine wa kuchukua nafasi ya Bw Sonko.

Gavana huyo wa zamani anaitaka korti ifutilie mbali uamuzi wa Afisa Msimamizi wa Uchaguzi wa IEBC katika Kaunti ya Mombasa Swalha Ibrahim kutomuidhinisha.

Hata hivyo, majaji hao waliruhusu ombi la Tume ya Maadili na Kukabili Ufisadi (EACC) kujumuishwa katika kesi hiyo.

Kupitia kwa wakili Philip Kagucia, EACC ilisema kuwa ilifaa kujumuishwa kwenye kesi hiyo ili nayo itoe matokeo ya uchunguzi wake iwapo Bw Sonko anastahili kuruhusiwa kuwania wadhifa huo.

Ombi la EACC lilikuwa likisikilizwa hapo Jumatatu mchana.

Bw Sonko pia anataka mahakama iamuru kuwa amehitimu kuwania ugavana wa Mombasa mnamo Agosti 9 na pia mahakama imwamuru Bi Ibrahim kukubali stakabadhi zake za uteuzi.

Makataa

Bw Sonko katika kesi hiyo alidai kuwa Kitengo cha Kusuluhisha Mizozo cha IEBC (DRC) kiliidhinisha uamuzi wa Bi Ibrahim kuwa shahada yake na nakala yake ziliwasilishwa kwa kuchelewa ilhali msimamizi wa uchaguzi wa kaunti awali alikuwa amekiri kuwa aliwasilisha stakabadhi hizo kwa wakati uliowekwa siku ya uteuzi.

Anadai hatua ya Msimamizi wa Uchaguzi wa Kaunti hiyo kukataa kupokea nakala ya shahada yake ilikuwa kimaksudi ili makataa yaliyowekwa yapite.

Pia anasema DRC ilikataa kutilia maanani kuwa aliwasilisha rufaa yake katika Mahakama ya Juu kuhusu kutimuliwa kwake mamlakani na madiwani wa Bunge la Kaunti ya Nairobi na pia Bunge la Seneti.

Gavana huyo wa zamani amekuwa akidai kuwa hana hatia hadi kesi iliyowasilishwa dhidi yake kortini iamuliwe jinsi ambavyo Katiba imekuwa ikiamrisha.

Hata hivyo, amekuwa akipinga dai jingine kuwa aliwasilisha stakabadhi zake siku ya uteuzi nje ya muda uliowekwa wa saa nane mchana hadi saa 10 jioni mnamo Juni 7.

  • Tags

You can share this post!

Mdahalo wa wagombeaji wa urais kuandaliwa siku 13 kabla ya...

Wakazi wamlilia Kibicho awapunguzie ‘kelele’ za...

T L