• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 10:50 AM
Mdahalo wa wagombeaji wa urais kuandaliwa siku 13 kabla ya upigaji kura

Mdahalo wa wagombeaji wa urais kuandaliwa siku 13 kabla ya upigaji kura

NA LEONARD ONYANGO

MDAHALO wa wawaniaji wa urais utafanyika siku 13 kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

Mkuu wa tume andalizi ya Mdahalo wa Urais, Clifford Machoka jana Jumatatu alisema mdahalo huo utafanyika Julai 26.

Mdahalo wa wawaniaji wenza utafanyika Julai 19.

Sekretariati hiyo pia imeandaa mdahalo wa wawaniaji wa ugavana Kaunti ya Nairobi ambao utafanyika Julai 11.

Midahalo hiyo yote itafanyika katika Chuo Kikuu cha Catholic Eastern Africa (CUEA) mtaani Karen, Nairobi, kuanzia saa kumi na moja jioni.

Bw Machoka alisema kuwa wanahabari watakaowahoji wawaniaji hao ni Bi Serfine Achieng’ Ouma wa KBC, Bw Ayub Abdikadir wa K24, Bi Zubeida Koome wa KTN News na Bw Mark Masai wa NTV.

Mwenyekiti wa midahalo hiyo yote atakuwa Bw Waihiga Mwaura wa Citizen TV.

“Wanahabari watakaoshiriki mahojiano hawataruhusiwa kukutana na timu za kampeni za wawaniaji au kuwapa maswali,” akasema Bw Machoka.

Naibu wa Rais William Ruto alikuwa ametishia kususia mahojiano hayo akidai kuwa amekuwa akibaguliwa na vyombo vya habari.

Dkt Ruto alidai kuwa baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikitenga muda mwingi kupeperusha mikutano ya kampeni ya wapinzani wake na kumbagua.

Lakini wamiliki wa vyombo vya habari walishikilia kuwa wanahabari wamekuwa wakitekeleza majukumu yao kwa usawa bila kupendelea.

  • Tags

You can share this post!

Elija Lidonde: Majagina kucheza Jumapili

Mahakama yampa Sonko matumaini ya kuwa debeni

T L