• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 10:55 AM
Mandago adai nia ya Raila ni kuyumbisha serikali ya Ruto

Mandago adai nia ya Raila ni kuyumbisha serikali ya Ruto

NA TITUS OMINDE

SENETA wa Uasin Gishu Jackson Mandago amesema maandamano ya leo Jumatatu yaliitishwa na kiongozi wa Azimio Raila Odinga hayakuwa ya lazima na ni ya ubinafsi.

Bw Mandago na wabunge wengine wa eneo hilo wamesema maandamano hayo yalilenga kuhujumu serikali ya Rais William Ruto ambaye amekuwa uongozini kwa miezi sita pekee.

Bw Mandago alimlaumu Bw Odinga kwa kutumia maandamano kushika nchi mateka kwa miaka mingi kwa sababu ya ubinafsi wake wa kutaka mamlaka kwa kutumia kile ameita ni fujo.

Viongozi hao wamemtaka Rais Ruto kumpuuza Bw Odinga na kuzingatia utekelezaji wa ahadi zake za kampeni kwa Wakenya.

Hayo yamejiri huku shughuli za kawaida katika mji wa Eldoret zikiendelea kama kawaida Jumatatu huku wakazi wakipuuza wito wa Azimio la Umoja-One Kenya wa kushiriki maandamano.

Shughuli za kibiashara katika mji huo zimeendelea bila usumbufu wowote.

Viongozi wa eneo hilo wamewataka wakazi kuendelea na shughuli zao za kila siku bila wasiwasi wowote.

Wakazi waliozungumza na Taifa Leo wamesema waliendelea na shughuli zao za kawaida na hawakuona umuhimu wa kushiriki maandamano.

“Maandamano haya hayana maana yoyote kwetu kama wakazi wa Uasin Gishu. Kama mkazi wa Uasin Gishu ninataka mbolea na mbegu kwa msimu huu wa upanzi. Hakuna haja ya maandamano,” akasema Bw Jackson Mutung, mkazi wa Eldoret mjini.

Naye mkazi wa Eldoret Daniel Chesire amesema kuwa ingawa wakazi wa Uasin Gishu hawashiriki maandamano hayo kuna haja ya Rais Ruto kushirikisha viongozi wa upinzani katika mazungumzo.

“Wakati umefika kwa viongozi hao wawili kushiriki mazungumzo ili kuboresha uchumi wa nchi yetu. Ni mjinga pekee anayefikiri kuwa mambo ni sawa katika nchi yetu. Ni lazima tuepuke ukabila na kukumbatia kila Mkenya bila kujali misimamo yetu ya kisiasa,” amesema Bw Chesire.

Mkazi mwingine, Julius Rugut amesema alikuwa akiendelea na shughuli zake za kila siku akibainisha kuwa maandamano ni ghali mno.

Aliwataka Wakenya walioshiriki katika maandamano kuwaruhusu viongozi hao wawili kushiriki mazungumzo kwa ajili ya nchi.

“Kuna haja ya viongozi wetu kupigia debe njia ya ustawi wa nchi yetu,” akasema Bw Rugut huku akihimiza upinzani umpe rais Ruto mwaka mmoja ili kuimarisha uchumi wa nchi.

  • Tags

You can share this post!

Maandamano: Shughuli muhimu zasimama jijini Nairobi

MAANDAMANO: Raila ahutubia wafuasi Eastleigh, raia...

T L