• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 5:59 PM
Mapasta, mapadri na mashemasi kulipwa na serikali – David Waihiga

Mapasta, mapadri na mashemasi kulipwa na serikali – David Waihiga

NA LEONARD ONYANGO

VIONGOZI wa makanisa wakiwemo mapasta, mapadri, mashemasi na wazee wa makanisa watalipwa mishahara na serikali mwaniaji wa urais wa chama cha Agano akishinda urais Agosti 9.

Bw Waihiga jana Jumatatu alisema kuwa serikali yake itabuni hazina maalumu itakayotumika kuwalipa viongozi hao makanisa kutokana na juhudi zao za kutetea maadili katika jamii.

Serikali ya Agano itafutilia mbali ada au ushuru unaotozwa makanisa.

Bw Waihiga pia ameahidi kulipa hela viongozi wa kidini ili makanisa yao yatumike kama madarasa kati ya Jumatatu na Ijumaa.

Aliahidi kuangamiza zimwi la ufisadi, kuinua sekta ya kilimo na kuboresha huduma za matibabu.

Bw Waihiga katika manifesto yake iliyozinduliwa Jumatatu jijini Nairobi aliahidi kurejesha nchini fedha za wizi zilizofichwa ughaibuni na wafisadi.

Bw Waihiga alisema kuwa Sh4 trilioni hupitia mikononi mwa walanguzi wa fedha kila mwaka.

“Nitatwaa fedha zote haramu zinazoingizwa humu nchini kutoka ng’ambo na zirejeshwe kwa wananchi,” akasema Bw Waihiga.

Mwaniaji huyo wa urais alisema kuwa ufisadi umechangia pakubwa katika kudorora kwa sekta za kilimo na afya.

“Serikali yangu itaanzisha uchunguzi dhidi ya mawaziri wa kilimo wa zamani, makatibu wa wizara na wajumbe wa bodi zinazohusika na mazao mbalimbali,” akasema.

Naibu wa Rais William Ruto atakuwa miongoni mwa mawaziri wa zamani wa kilimo watakaochunguzwa iwapo Bw Waihiga atashinda Uchaguzi Mkuu wa mwezi ujao.

Kuhusu afya, Bw Waihiga ameahidi kuunda tume ya kuchunguza gharama ya juu ya matibabu nchini.

“Serikali itapunguza kiasi cha fedha ambazo Wakenya wanalipia kwa ajili ya kadi ya bima ya matibabu (NHIF),” akasema Bw Waihiga aliyekuwa ameandamana na mwaniaji mwenza wake Ruth Mucheru-Mutua.

Serikali ya Agano pia itasajili familia zote nchini na kuhakikisha kuwa kila familia inakuwa na angalau mtu mmoja aliyeajiriwa.

Ushuru ambao hutozwa mishahara (PAYE) utapunguzwa kwa asilimia 50 chini ya utawala wa serikali ya Agano.

“Serikali ya Agano itahakikisha kuwa mikataba yote ikiwemo Reli ya Kisasa (SGR) na bandari za Mombasa, Lamu, Naivasha na Kisumu zinawekwa wazi,” akasema Bw Waihiga.

  • Tags

You can share this post!

Wanasiasa wachoma mabilioni njaa ikiuma

Elija Lidonde: Majagina kucheza Jumapili

T L