• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Masaibu ya Sonko sasa yachochea marekebisho kwenye Katiba

Masaibu ya Sonko sasa yachochea marekebisho kwenye Katiba

NA WINNIE ATIENO

MASAIBU yanayomkumba aliyekuwa gavana wa Nairobi, Bw Mike Sonko, kwa kubanduliwa mamlakani mwaka wa 2020, yameanza kuwatia kiwewe viongozi na wadau wengine wa kisiasa.

Siku chache baada ya maseneta kusema sheria kuhusu kung’atuliwa kwa viongozi wanaokosa maadili si ya haki, Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka nchini (IEBC) nayo imejitosa katika mijadala hiyo.

Bw Sonko anaendelea kutafuta ukombozi mahakamani baada ya IEBC kukataa kumwidhinisha kuwania ugavana Mombasa kupitia Chama cha Wiper.

Mwenyekiti wa IEBC, Bw Wafula Chebukati, sasa amewataka wabunge kujadili ni miaka mingapi ambayo viongozi wanaobanduliwa mamlakani wanafaa kutowania viti vya kisiasa.

“Katika nchi nyingine wanasiasa waliobanduliwa mamlakani wananyimwa nafasi ya kuwania viti vya kisiasa kwa miaka 10 ambapo wanajitakasa kabla ya kuruhusiwa kurudi ulingoni. Lakini hapa Kenya, hatuna sheria mahususi kuhusu swala hilo tata. Bunge linafaa libuni sheria ili wanasiasa waliobanduliwa wasihukumiwe maisha,” alisema Bw Wafula Chebukati, mwenyekiti wa IEBC.

Alipendekeza kuwa wanasiasa waliobanduliwa mamlakani wapigwe marufuku ya kuwa mamlakani miaka 10.

Wiki iliyopita, baadhi ya maseneta wakiwemo Kipchumba Murkomen (Elgeyo Marakwet) na Stewart Madzayo (Kilifi), walilalamika kuwa sheria inafaa iwe kwamba, kiongozi anapoondolewa mamlakani kwa ukiukaji wa sheria, atapewa muda fulani kabla kukubaliwa tena kushikilia wadhifa wa uongozi wa umma.

Hilo ni tofauti na sasa ambapo wale wanaotolewa mamlakani kwa kukiuka sheria hawakubaliwi daima kuwa uongozini tena.

“Anapoondolewa mamlakani tayari hiyo ni adhabu kwake, kwa hivyo akikatazwa kuwa uongozini daima, ni adhabu mara mbili,” akasema Bw Madzayo katika kikao cha seneti juma lililopita.

Seneta wa Siaya, Bw James Orengo, alidokeza kuwa kubadilisha sheria hiyo kutahitaji marekebisho ya Katiba.

Mbali na hayo, Bw Chebukati aliwataka wanasiasa ambao walikatazwa kugombania viti vya kisiasa na kuwasilisha malalamishi mahakamani kukubali uamuzi wa jopo la IEBC kwani mahakama ilithibitisha tume hiyo ndiyo ina mamlaka ya kutatua malalamishi aina hiyo.

Alisema IEBC ishamaliza uteuzi wa wagombea wa wanasiasa. Awali Tume ya Kupambana na Ufisadi Nchini, (EACC) ilitaka wanasiasa 241 wasikubaliwe kugombania viti vya kisiasa sababu ya madai ya kuhusika na ufisadi.

“Hawana budi ila kukubali uwamuzi wa makahama, sisi tushamalizana na uteuzi wa wagombea na sasa tunajitayarisha kuchapisha makaratasi ya kugombea. Tulipokea ripoti kutoka EACC ambayo ilikuwa imewakataza wanasiasa 241 kugomania siasa, tulichunguza na tukatoa uwamuzi wetu,” alisema Bw Chebukati.

Akiongea kwenye mkutano na wahariri huko katika hoteli ya Diani Reef, mwenyekiti huyo aliwaahidi Wakenya kuwa uchaguzi utakuwa wa haki, usawa na huru.

  • Tags

You can share this post!

Ukora wa bunge la 12 na kamati zake

Rovanpera mfalme mpya Safari Rally, Toyota iking’aa

T L