• Nairobi
  • Last Updated June 12th, 2024 4:24 PM
Ukora wa bunge la 12 na kamati zake

Ukora wa bunge la 12 na kamati zake

NA CHARLES WASONGA

UTENDAKAZI wa Bunge la 12 ambao ulitamatisha vikao vyake juzi na kutoa nafasi kwa wabunge na maseneta kushiriki kampeni za uchaguzi mkuu wa Agosti 9 haujafikia matakwa ya wananchi kulingana na hitaji la Katiba, ripoti mpya inaonyesha.

Hii ni licha ya kwamba bunge hilo lenye vitengo viwili (Bunge la Kitaifa na Seneti) kujisifu kupitisha miswada mingi zaidi ikilinganishwa na mabunge yaliyotangulia. Kiongozi wa Wengi katika bunge la kitaifa, Bw Amos Kimunya alisema kati ya jumla ya miswada 362 iliyowasilishwa katika bunge hilo kuanzia Septemba 31, 2017, 140 ilipitishwa, 114 ikatiwa saini na Rais Uhuru Kenyatta huku mingine 24 ikifutiliwa mbali. Mwenzake wa Seneti, Bw Samuel Poghisio naye alisema kati ya miswada 75 iliyoshughulikiwa na bunge hilo ndani ya miaka mitano, 17 ilifaulu kuwa sheria baada ya kupata saini ya Rais.

Lakini kulingana na ripoti ya Shirika la Mzalendo Trust, ambalo hufuatilia utendakazi wa wabunge na maseneta, mingi ya miswada ilimwongezea ‘Wanjiku’ shida huku miswada yenye manufaa kwa raia ikikosa kupitishwa.

“Kwa mfano, mswada wa Fedha wa 2018 ambao ulianzisha ushuru wa VAT wa kiwango cha Sh8 kwa kila lita ya mafuta ndio chanzo cha kupanda kwa bei ya mafuta na gharama ya maisha kwa jumla.

“Pili, mswada wa marekebisho ya Sheria ya Kupambana na Ufisadi na Uhalifu wa Kiuchumi uliodhaminiwa na Mbunge wa Kiharu, Ndindi Nyoro ulipigwa vita na kusambaratishwa. Hii ni licha ya kwamba ufisadi hufyonza karibu Sh600 bilioni, pesa za umma, kila mwaka,” anasema mkurugenzi mkuu wa shirika hilo Caroline Gaita, katika mukhutasari wa ripoti hiyo.

Mbali na hayo, bunge la kitaifa liliahirisha vikao vyake Juni 9, kabla ya kupitisha mswada uliolenga kupunguza ushuru mwingi unaotozwa mafuta, na ambao huchangia bei ya juu ya bidhaa hiyo. Mswada huo uliwasilishwa bungeni Septemba 20, 2021 kwa udhamini wa Kamati ya Bunge kuhusu Fedha chini ya uenyekiti wa Mwakilishi wa Kike wa Homa Bay, Gladys Wanga.

Inakadiriwa kuwa ushuru huchangia zaidi ya asilimia 50 ya bei ya lita moja ya mafuta. Hii ina maana kuwa zaidi ya Sh75 katika bei ya petroli ambayo ni Sh159 wakati huu ni ushuru ambao hutozwa na serikali kwa bidhaa hiyo.

Ripoti ya Mzalendo Trust pia inawaelekezea kidole cha lawama wabunge na maseneta kwa kuendesha chunguzi kuhusu sakata nyingi lakini mapendekezo kwenye ripoti walizoaanda yakakosa kutekelezwa. Aidha, ripoti nyingine ziliangushwa katika mabunge hayo kutokana na ubovu wa ripoti husika, ushawishi kutoka serikali kuu, sababu za kisiasa na hongo. Miongoni mwa chunguzi ambazo hazikuzaa matunda ni uchunguzi wa sakata ya uagizaji sukari yenye sumu, bila kulipiwa ushuru, ulioendeshwa na kamati ya pamoja ya Kilimo na Biashara mnamo Agosti, 2018.

Lakini ripoti ya uchaguzi iliyowaelekezea kidole cha lawama aliyekuwa Waziri wa Fedha Henry Rotich na aliyekuwa Waziri wa Biashara Adan Mohamed kwa uovu huo, ilizimwa katika bunge la kitaifa. Baadaye kuliibuka madai kuwa wabunge walihongwa, kwa Sh10,000, kutupilia mbali ripoti hiyo. Hii ni licha ya serikali kupoteza zaidi ya Sh7 billioni kama ushuru mbali na madhara ya sukari ya sumu ya zaibaki (mercury) kwa maisha ya wananchi.

SAKATA YA ARDHI

Mabunge ya kitaifa na seneti pia yalichunguza sakata ya ardhi ya ununuzi wa ardhi wa shule ya Ruaraka kwa Sh1.5 bilioni lakini wahusika, wakiwemo waziri mmoja mwenye ushawishi mkubwa na wakuu wa Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC) walikwepa adhabu. Hii ni baada ya ripoti za chunguzi huo zilizoendeshwa na Kamati ya Seneti kuhusu Uhasibu (CPAIC) na Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Elimu, kuitupilia mbali, licha ya maseneta na wabunge kulipwa pesa nyingi za umma kama marupurupu ya vikao vya kamati hizo.

Mabunge hayo pia yalichunguza sakata ya ununuzi wa bidhaa za kupambana na Covid-19 kwa bei ya juu kupita kiasi, ya Sh7.6 bilioni Aprili 2020. Lakini licha ya mabunge hayo kupendekeza kufunguliwa mashtaka kwa wakuu watatu wa Mamlaka ya Usambazaji Dawa (KEMSA), hilo halikutendeka.

Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) ingali inajivuta kuwafungulia mashtaka wahusika hao ambao tangu wasimamishwa kazi mnamo Juni 30, 2020, wanaendelea kupokea nusu ya mishahara yao. Hii ni kwa msingi kuwa hawajapigwa kalamu rasmi.

Bunge lilifeli kushinikiza kutekelezwa kwa ripoti za kamati zake kuhusu sakata hiyo ya Kemsa kupitia Kamati kuhusu Utekelezaji Mapendekezo ya Bunge inayoongozwa na Mbunge wa Narok Kaskazini Moitalel Ole Kenta. Kilele cha utendakazi mbaya wa mabunge hayo mawili, kulingana na Mzalendo Trust, ni hatua ya kuongeza kiwango cha fedha ambazo serikali inaweza kukopa kutoka Sh9 trilioni hadi Sh10 trilioni.

  • Tags

You can share this post!

Wanawake Garissa walalamika kunyanyaswa kisiasa kupitia...

Masaibu ya Sonko sasa yachochea marekebisho kwenye Katiba

T L