• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
Maseneta kuendesha vikao vya kukusanya maoni kuhusu mswada wa sheria za vyama

Maseneta kuendesha vikao vya kukusanya maoni kuhusu mswada wa sheria za vyama

Na CHARLES WASONGA

UMMA na wadau mbalimbali wana siku 14 za kutoa maoni na mapendekezo kuhusu mswada tata wa mageuzi ya sheria za vyama vya kisiasa ambao Jumanne uliwasilishwa rasmi katika Seneti.

Shughuli hiyo ya kukusanya kauli za umma kwa njia ya taarifa na mawasilisho ya moja kwa moja, itaendeshwa na Kamati ya Seneti kuhusu Haki, Masuala ya Kikatiba na Haki za Kibinadamu.

Kamati hiyo inayoongozwa na Seneta wa Nyamira, Okong’o Omogeni, ina maseneta ambao ni wataalamu katika masuala ya sheria. Miongoni mwao ni; kiongozi wa wachache James Orengo, Mkuu wa Sheria wa zamani Amos Wako (Busia) na kiranja wa wachache Mutula Kilonzo Junior.

Mswada huo ambao wiki jana ulipitishwa katika bunge la kitaifa kwenye vikao vilivyosheheni kelele na vita miongoni mwa wabunge wa mirengo miwili hasimu, ilisomwa kwa mara ya kwanza katika seneti na kingozi wa wengi Samuel Poghisio.

“Naamuru kwamba mswada huo uwasilishwe kwa kamati ya seneti kuhusu sheria ili iweze kuendesha vikao vya kukusanya maoni na mapendekezo kutoka kwa umma,” akasema Bw Lusaka.

Baada ya siku 14, kamati ya Bw Omogeni itaandaa ripoti na kuwasilisha ripoti yake kwa kikao cha bunge lote.

Ni baada ya kuwasilishwa kwa ripoti yake ambapo mswada huo unaopendekeza kuundwa kwa vyama vya miungano, itajadiliwa na maseneta na kupigiwa kura.

Kamati ya Seneta Okong’o inatarajiwa kuwasilisha ripoti hiyo mnamo Januari 25, 2022, ambapo maseneta watapata fursa ya kuujadili kwa kina kabla ya kuupigia kura.

Kiongozi wa wengi Samuel Poghisio na mwenzake wa wachache James Orengo waliwahakikishia maseneta kwamba mjadala kuhusu mswada huo utaendeshwa bila vurumai zozote.

“Sarakasi tulizoshuhudia katika bunge lile lingine, zilishusha hadhi ya asasi ya bunge. Lakini tunaweza kurejesha heshima na hadhi hiyo,” akasema Bw Poghisio ambaye ni seneta wa Pokot Magharibi.

Naye Bw Orengo alielezea matumaini kwamba maseneta watajadili mswada huo kwa undani na ukomavu ili kuzuia fujo zilizoshuhudiwa katika bunge la kitaifa.

Hakikisho sawa na hilo lilitolewa na Spika wa Bunge hilo Kenneth Lusaka, kauli ambayo iliungwa mkono na maseneta wandani wa Naibu Rais William Ruto kama vile Kipchumba Murkomen na Samson Cherargei.

Wiki jana, mswada huo ulipitishwa katika bunge la kitaifa baada ya juhudi za wabunge wa mrengo wa ‘Tangatanga’ kuusambaratisha ama kuudhoofisha kuangushwa na wenzao wa mrengo wa ‘Handisheki’.

You can share this post!

AFCON: Limbukeni Sierra Leone waridhika kutoka sare na...

Raila kuvumisha Azimio mjini Thika mnamo Jumamosi

T L