• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:50 AM
Masuala ya SGR, ardhi kuendelea kushamiri katika kampeni

Masuala ya SGR, ardhi kuendelea kushamiri katika kampeni

NA VALENTINE OBARA

MZOZO kuhusu usafirishaji mizigo kwa reli ya SGR, na mizozo ya tangu jadi kuhusu umiliki wa mashamba, inatarajiwa kuendelea kutoa mwelekeo wa kampeni za uchaguzi ujao katika Kaunti ya Mombasa.

Utafiti wa shirika la Infotrak umebainisha kuwa, asilimia 43 ya wakazi wa Mombasa wanataka viongozi watakaochaguliwa watatue mzozo kuhusu usafirishaji mizigo kwa reli ya SGR, ambao uliathiri nafasi nyingi za ajira mjini humo.

Kando na hayo, asilimia 46 ya wakazi walisema watachagua viongozi kwa kuzingatia kujitolea kwao kusuluhisha mizozo ya umiliki wa mashamba.

Ripoti ya utafiti huo iliyotolewa jijini Nairobi jana Jumapili inaonyesha kwamba ukosefu wa ajira bado ni donda sugu ambalo wakazi wengi wa Mombasa wanataka utatuliwe kwa dharura na viongozi wao.

Suala hilo lilitajwa na idadi kubwa zaidi ya wakazi (asilimia 28) walipoulizwa ni suala lipi ambalo wanataka serikali ya kaunti itatue kwa dharura, ikilinganishwa na masuala mengine ambayo wangependa yatatuliwe.

Kando na ukosefu wa ajira, wakazi wengi walilalamikia gharama ya juu ya maisha (asilimia 18), ukosefu wa maji safi (asilimia 13), ukosefu wa usalama (asilimia saba), na miundomsingi duni kama vile barabara (asilimia sita).

Asilimia mbili pekee ya wakazi ndio walitaja ufisadi na matumizi ya dawa za kulevya kama masuala yanayohitaji kutatuliwa kwa dharura.

Katika maeneobunge, ukosefu wa ajira uliibuka changamoto kuu katika maeneo yote isipokuwa Jomvu ambapo wakazi walisema tatizo lao kuu ni ukosefu wa maji safi.

“Imebainika kuwa ukosefu wa usalama umesababishwa na changamoto kuu zinazokumba wakazi kama vile ukosefu wa ajira na gharama ya juu ya maisha. Mawili hayo yalitajwa kuwa matatizo makuu,” ripoti ya Infotrak ikasema.

You can share this post!

Nassir ana nafasi nzuri kumrithi Joho, utafiti waonyesha

Raila kumlemea Ruto debeni sasa – Utafiti

T L