• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Matumaini kijijini kwa Wajackoyah

Matumaini kijijini kwa Wajackoyah

NA BERNARD MWINZI

HATUA ya Profesa George Wajackoyah kujitosa katika kinyang’anyiro cha urais, imebadilisha maisha ya kwao mashambani karibu na mji wa Mumias, Kaunti ya Kakamega.

Baada ya kuidhinishwa na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka Nchini (IEBC) kuwania Urais, kijiji anakotoka Wajackoyah, kimeanza kuwa na umaarufu sana. Wakazi wanafurahishwa na matunda ambayo yameanza kuonekana hata kabla ya mwana wao kuingia ikulu.

Ziara ya Taifa Leo kijijini humo, ilifahamishwa kuwa miundomsingi duni imeanza kurekebishwa, hasa barabara ya kufika katika boma lake.

Nyumbani kwake, kulikuwa na shughuli nyingi huku wafanyakazi nao wakiendelea kukarabati nyumba zake, pengine zifikie hadhi ya mtu ambaye wanaamini huenda akawa Rais wa tano wa Kenya.

Miongoni mwa wakazi wa Nairobi, Profesa Wajackoyah amejizolea jina ‘The Fifth’ na hilo limeshaajisha wanakijiji waamini kuwa atashinda Urais.

Ulinzi umeimarishwa katika boma lake huku maafisa wawili wa polisi wa utawala wakililinda mchana na wengine usiku kwa zamu. Katiba inaamrisha kuwa kila mwaniaji wa urais lazima awekewe ulinzi mkali hadi uchaguzi mkuu ufanyike na matokeo kutangazwa.

Ulinzi

Kuwepo kwa polisi hao kumechangamsha kijiji hicho mno kwa sababu si jambo la kawaida kwa huduma kali za ulinzi kama hizo kupatikana hapo.

Prof Wajackoyah alianza ujenzi wa jumba lake hivi majuzi kwa sababu ana jumba lingine jijini Kisumu ambapo yeye hulala akienda nyumbani.

Babake mdogo, Bw Charles Luchiri aliambia Taifa Leo kuwa Prof Wajackoyah anashabikiwa sana kijijini humo.

“Tunaamini kuwa atapata kura katika vituo vyote hapa. Yeye ni maarufu sana hapa kwa sababu amewalipia wanafunzi wengi karo na pia kuwajengea wasiobahatika katika jamii nyumba zao,” akasema Bw Luchiri.

Kutoka boma la Prof Wajackoyah ni kilomita chache tu kutoka mpaka wa kaunti za Siaya na Kakamega na katika chaguzi zote ambazo Kinara wa ODM Raila Odinga amewania Urais, amekuwa chaguo la wakazi.

Hata hivyo, Bw Luchiri anasema mara hii Bw Odinga atabwagwa kwa sababu Prof Wajackoyah anatazamwa na wakazi kama mmoja wao na mwanao ambaye amekuwa akiwafaa wakati wa dhiki na shida.

Ujana wake

Hata hivyo, maisha ya Profesa Wajackoyah, ujanani na utotoni yanachora taswira tofauti na jinsi yalivyo kwa sasa. Picha zake za zamani zinamsawiri kama kijana mtanashati aliyevalia nadhifu na mchangamfu.

Pengine hii ndiyo siri ya ufanisi wake masomoni kwa kuwa ana shahada 16 ikiwemo shahada ya uzamifu kutoka Chuo Kikuu cha Walden Marekani. Amesafiri kwingi na ana ufasaha mkubwa wa Kiingereza kando na kuwa wakili maarufu kimataifa.

Profesa alikuwa mpenda masomo na mara nyingi alikuwa akivalia suti kinyume na sasa ambapo anavalia kama ‘Rastafara’ na long’i za ‘jeans’ ambazo zimechakaa akiwa kwenye msafara wa kampeni na hata mashati ambayo hayana vifungo.

Akiwa katika runinga ya NTV wiki jana, Prof Wajackoyah alionekana kutokuwa na subira na alikataa kujibu maswali kuhusu baadhi ya sera zake. Alivurugana na mtangazaji wa zamu na kuondoka kwenye shoo akiwa amehamaki sana akionekana kukerwa na maswali aliyoulizwa.

Profesa George Wajackoyah. PICHA | MAKTABA

Hata hivyo, hakuna kilichoko kwenye manifesto yake ambacho kimevutia uungwaji mkono na wakati huo huo ukosoaji kama ahadi ya kuhalalisha bangi. Anadai kuwa mauzo ya bangi nje ya nchi, yataipa Kenya Sh9.2 trilioni kila mwaka, pesa ambazo zinaweza kumaliza deni la Kenya na pia kumpa kila Mkenya ruzuku ya Sh200,000.

“Mataifa ya Magharibi yamehalalisha bangi. Kwa nini Kenya tusifuate mkondo huo? Tukipanda bangi kaunti ya Nyeri pekee, Kenya itakuwa na hazina ya kutosha kwenye Shirika la Kimataifa la Kifedha (IMF) na hatutahitaji kukopa fedha,” akasema.

Ingawa kiuchumi, hakuna hoja za kutosha kuunga kauli yake, ahadi anazotoa wakili huyo mashuhuri imewavutia raia, baadhi wakianza kumuiga kupitia kuvaa mashati yenye nembo yake ya kampeni.

Wengi wamechangia kauli mbiu ya ‘Wajackoyah The Fifth” au “Tingiza Miti” ambazo anazitumia sana kwenye mikutano ya kampeni.

Hata hivyo, viongozi wa kidini nao wamejitokeza kumpinga, wakidai anaeneza tabia za kishetani na kwa ujumla wanasema kampeni yake haizingatii maadili.

  • Tags

You can share this post!

Njaa yakeketa maelfu Nyandarua na Laikipia

WANDERI KAMAU: Dunia ishirikiane kudhibiti makundi yenye...

T L