• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Sijajiunga na DP – Muturi

Sijajiunga na DP – Muturi

Na George Munene

SPIKA wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi amekanusha kujiunga na Democratic Party. Bw Muturi, ambaye amejiunga na kinyang’anyiro cha urais 2022, alitaja habari hizo kama uvumi.

“Kinachoenezwa ni uvumi unaopaswa kupuuziliwa mbali,” alisema Ijumaa, akiwa nyumbani kwake kijijini Kanyuambora, Kaunti ya Embu. Spika huyo alisisitiza kuwa bado hajaunda chama atakachotumia kugombea urais.

“Wakati ukiwadia nitafichua chama nitakachotumia tiketi yake kugombea urais,” alisema.

Alifafanua kwamba anataka kuwa rais ili ahakikishe maendeleo yanasambazwa kwa usawa katika sehemu zote nchini.Bw Muturi alitaja eneo la Mlima Kenya Mashariki kama lililotengwa zaidi kimaendeleo nchini.

Akihutubia viongozi wa kidini, Spika huyo alisema wakati umewadia kwa Mlima Kenya Mashariki kutoa rais.“Rais mpya anapaswa kutoka eneo hili. Tunapanga kuwa na chama chetu binafsi kitakachounda serikali ijayo,” alisema.

Aliwahimiza viongozi kutoka Mlima Kenya Mashariki wasihadaiwe kupigia debe chama ambacho si chao.Bw Muturi alitoa wito kwa viongozi wa kidini kumakinika na kuwatathmini viongozi wa kisiasa wanaogombea nyadhifa mbalimbali za uongozi na kuwashauri watu ipasavyo.

Alieleza kuwa viongozi wa kidini huchangia nafasi muhimu katika siasa za Kenya na wanapaswa kusaidia kuhakikisha kuna viongozi bora Kenya.Alisema kuwa yuko tayari kufanya kazi na viongozi wenye mtazamo sawa na wake wa kubadilisha taifa.

You can share this post!

Mbinu za Raila kuzima Mudavadi na Ruto Magharibi

Ruto kukabiliwa na mtihani mkali 2022 akiepuka miungano