• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 7:50 AM
Mbunge ataka korti izuiwe kumtuza Raila

Mbunge ataka korti izuiwe kumtuza Raila

NA JOSEPH WANGUI

MBUNGE wa Mugirango Kusini Silvanus Osoro na wapigakura watatu, wamewasilisha kesi kortini wakitaka ufafanuzi wa kisheria kuhusu nguvu za Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati katika kutangaza matokeo ya uchaguzi wa urais.

Katika kesi mbili tofauti zilizowasilishwa katika kitengo cha Mahakama ya Kikatiba na Haki za Binadamu, Milimani, Nairobi, walalamishi pia wanapinga nguvu za Mahakama ya Juu kutangaza mshindi wa uchaguzi wa urais iwapo kura zitahesabiwa na kujumulishwa upya.

Wanataka sehemu ya 80(4) ya Sheria ya Uchaguzi inayoruhusu Mahakama ya Juu kutangaza mshindi wa uchaguzi wa urais iwapo makosa yatapatikana katika hesabu ya kura, itangazwe kuwa kinyume cha katiba.

Sehemu hiyo ya sheria waliyotaja, inapatia Mahakama ya Juu mamlaka ya kutangaza mshindi wa uchaguzi wa urais na kuagiza tume ya uchaguzi kutoa cheti cha ushindi kwa mgombeaji baada ya kuhesabu upya kura zilizopigwa.

Inasema “mahakama inayosikiliza kesi ya uchaguzi inaweza kuagiza tume kutoa cheti cha uchaguzi wa urais, mbunge au mwakilishi wa wadi iwapo baada ya kuhesabu kura, mshindi atabainika; na mshindi hatakuwa amepatikana kuhusika na makosa ya uchaguzi”.

Kulingana na Bw Osoro, ambaye ni mshirika wa Rais Mteule William Ruto, sehemu ya sheria hiyo ni kinyume cha katiba kwa kuwa inakiuka ibara ya 138(10) ya katiba na inahujumu uhuru wa IEBC.

Ibara 138(10) ya katiba inasema kwamba ndani ya siku saba baada ya uchaguzi wa urais, mwenyekiti wa IEBC anapaswa kutangaza matokeo ya uchaguzi wa urais na kuwasilisha ilani ya maandishi kwa Jaji Mkuu na Rais aliye madarakani.

“Ni kwa msingi huu ambapo ninahisi kwamba Bunge ilikiuka mamlaka yake kwa kupatia Mahakama ya Juu nguvu za kuagiza IEBC kupatia mgombeaji cheti cha uchaguzi,” anasema Bw Osoro.

Anasema kwamba sheria ya uchaguzi inaacha nje magavana wa kaunti kutoka ofisi ambazo mahakama inaweza kuagiza IEBC kutoa cheti cha ushindi wa uchaguzi baada ya kuhesabu na kujumulisha upya kura.

Kulingana na mbunge huyo, kuna tisho ya kukiuka haki za kikatiba, iwapo mgombeaji anayeshindwa katika uchaguzi wa urais ataenda katika Mahakama ya Juu kutaka atangazwe rais mteule kwa kutegemea sehemu ya sheria.

“Mahakama ya Juu ikiwa mahakama ya uchaguzi katika kesi ya kupinga matokeo ya kura ya urais inaweza kuamua matokeo ni halali au si halali pekee. Walioandika katiba hawakunuia Bunge kutunga sheria kuhusiana na uchaguzi wa urais,” anasema Bw Osoro.

Anataka Mahakama Kuu kuamua kwamba sehemu 80(4) ya sheria ya uchaguzi inakiuka katiba kwa kuwa “inapatia Mahakama ya Juu nguvu za kutangaza mshindi wa uchaguzi wa urais’.

  • Tags

You can share this post!

Hasira wafanyakazi wa Mumias wakitaka mwekezaji atimuliwe

Wakazi waalikwa kwa hafla ya ‘kihistoria’ ya kuapisha...

T L