• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 6:55 PM
Mchujo wazua hofu miongoni mwa wawaniaji

Mchujo wazua hofu miongoni mwa wawaniaji

NA BENSON MATHEKA

MCHUJO wa vyama vya kisiasa unaotarajiwa Aprili umeanza kuzua tumbojoto miongoni mwa wawaniaji wanaohisi kwamba huenda vyama vyao vikawanyima tiketi.

Hii ni baada ya baadhi ya vyama vikubwa vya kisiasa kukosa kutoa orodha ya wanachama ili waikague.

Vyama vya United Democratic Alliance UDA cha Naibu Rais William Ruto, ODM cha aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga na Jubilee kinachoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta ni baadhi ya vyama vinavyotarajiwa kufanya uteuzi baada ya wawaniaji zaidi ya 5,000 kumezea mate tiketi ya kila kimoja.

Kulingana na sheria, vyama vinafaa kutoa orodha ya wanachama watakaoshiriki mchujo siku kumi kabla ya tarehe ya uchaguzi.

Hata hivyo, chama cha UDA kimesema kwamba hakitatoa orodha hiyo kikidai inaweza kutumiwa na washindani wao kuingilia uteuzi.

“Tunalinda orodha yetu iwe siri ili isiingiliwe. Tunataka kuepuka hali ambapo mtu anadhani jina lake liko katika orodha na kisha alikose siku ya mchujo,” alisema mwenyekiti wa Bodi ya Uchaguzi ya UDA, Bw Antony Mwaura.

Ingawa alisema kwamba wataalika waangalizi wakiwemo wa kimataifa wakati wa mchujo utakaofanyika Aprili 14, baadhi ya wawaniaji na wanachama wameingiwa na wasiwasi kwamba huenda wakakosa majina yao na kukosa kushiriki kwenye mchujo.

Mwaniaji mmoja wa kiti cha seneta ambaye aliomba tusitaje jina lake alisema kuwanyima orodha kutawanyima haki ya kufanya kampeni miongoni mwa wanachama waliosajiliwa.

“Kulingana na sheria, ni watu wasio wanachama hawawezi kushiriki mchujo. Hivyo basi kutoa orodha kwetu kwa wakati kutatuwezesha kujiandaam,” akasema.

Chama cha UDA kinasema kimepokea wawaniaji zaidi ya 6,000 wa vyama viti tofauti.

Hali ni kama hiyo miongoni mwa wanachama wa ODM ambao wanalalamika kuwa wako gizani kuhusu mbinu ambayo kitatumia kwenye mchujo.

Kulingana na mwaniaji wa ugavana kaunti ya Siaya George Mugoye Mbeya, makao makuu ya ODM yanafaa kuelezea wawaniaji mapema kuhusu mbinu ya kutumia kwenye uteuzi.

“Kama wawaniaji, tunafaa kufahamishwa moja kwa moja mchakato ambao watatumia katika uteuzi. Kwa sasa tunasoma tu au kusikia kutoka kwa watu ambao hata hawajalipa ada za uteuzi,” akasema Bw Mbeya.

Baadhi ya wawaniaji wanahofia kuwa maafisa wa vyama watawachezea shere na kutoa tiketi kwa watu wanaochukuliwa kuwa waaminifu kwa viongozi hata kama sio maarufu mashinani.

Inadaiwa kuwa baadhi ya maafisa wa vyama tayari wanapendelea baadhi ya wawaniaji na ndio sababu hawataki kutoa orodha ya wanachama.

Haya yanajiri huku maafisa wakuu wa vyama vya kisiasa wakihakikishia wanachama kuwa zoezi hilo litakuwa huru na la haki.

Katika baadhi ya maeneo vyama vinapanga kutosimamisha wawaniaji na kuacha washirika wao katika miungano ya Azimio la Umoja na Kenya Kwanza.

Tayari chama cha ODM kimeashiria kuwa hakitakuwa na wawaniaji katika ngome za Kanu, Wiper na Jubilee ambavyo vinaunga azima ya urais ya Bw Odinga.

Vile vile, kuna hofu kwamba huenda UDA kisiwe na wawaniaji katika kaunti za Magharibi mwa Kenya ambako Amani National Congress ANC cha Musalia Mudavadi na Ford Kenya cha Moses Wetangula vina wafuasi wengi, Musalia na Wetangula ni washirika wa Dkt Ruto katika Kenya Kwanza Alliance.

  • Tags

You can share this post!

Joto kali Azimio, Kenya Kwanza wakimenyana Magharibi

TAHARIRI: Pombe haramu ni janga kwa taifa letu

T L