• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 5:01 PM
Joto kali Azimio, Kenya Kwanza wakimenyana Magharibi

Joto kali Azimio, Kenya Kwanza wakimenyana Magharibi

NA BRIAN OJAMAA

HUKU ikiwa imesalia miezi minne uchaguzi mkuu ufanyike, pambano kali la kisiasa linaendelea kujitokeza kati ya mirengo ya Azimio la Umoja na Kenya Kwanza Alliance magharibi mwa Kenya.

Katika kaunti eneo hilo, joto la kisiasa linaendelea kupanda huku wanasiasa wakihama kutoka mrengo mmoja hadi mwingine wakitumai kuwa hilo litawazolea ushindi katika uchaguzi huo.

Kenya Kwanza anayoiongoza Naibu Rais Dkt William Ruto inajivunia wabunge watano pamoja na Seneta Moses Wetang’ula huku Azimio analoliongoza Kinara wa ODM Raila Odinga likijivunia wabunge wanne pamoja na Gavana Wycliffe Wangamati.

Hivi majuzi mbunge wa Sirisia John Waluke aligura UDA na kujiunga na Jubilee huku nayo Ford Kenya ikivuna baada ya kumkabidhi Spika wa Seneti Ken Lusaka tiketi ya moja kwa moja ya kuwania ugavana.

Akitangaza kurejea Jubilee juma moja lililopita, Bw Waluke alisema kuwa alichukua hatua hiyo baada ya ushawishi wake Kenya Kwanza kudhoofishwa na ujio wa Mabw Wetang’ula na Lusaka.

Akizungumza katika hafla moja ya mazishi Jumamosi, Bw Waluke hasa alimrejelea Bw Lusaka kama aliyepotea kisiasa kwa kukubali kugombea ugavana ilhali alikuwa akishikilia wadhifa wa juu ambao ulimwezesha kushauriana na Rais Uhuru Kenyatta moja kwa moja.

“Kama wewe ni wa tatu kwenye itifaki ya uongozi baada ya rais na naibu wake, unakubali kivipi urejee tena hapa kuwania kiti cha ugavana badala ya kukiendea kiti kikubwa zaidi?” akauliza Bw Waluke.

Mbunge huyo alisisitiza kuwa ataendeleza kampeni kali dhidi ya Bw Lusaka kwa kuwa alipokuwa gavana kati ya 2013-2017, utawala wake ulizingirwa na sakata mbalimbali za ufisadi.

Alidai kuwa ushirikiano wa spika huyo na Bw Wetang’ula unalenga kuifilisi kaunti hiyo iwapo watapata ushindi mnamo Agosti 9.

“Ni Wetang’ula ambaye alituambia kuwa gavana wa sasa Wangamati atatuongoza vizuri kwa kuwa Lusaka alikuwa kiongozi fisadi ambaye alinunua wilbaro kwa bei za juu na kutusababishia aibu na kejeli kote ulimwenguni. Inakuaje sasa anasema Wangamati ni mbaya na Lusaka amekuwa mzuri?” akauliza tena.

Alisisitiza kuwa kama kiongozi katika kaunti hiyo hatamruhusu kinara huyo wa Ford Kenya kuwapendekezea raia kiongozi wanayefaa kumchagua kwenye nyadhifa mbalimbali kila mwaka wa uchaguzi.

“Amekuwa mbunge kwa zaidi ya miaka 35 lakini hakuna maendeleo yoyote aliyowapa wakazi wa Bungoma. Kwa hivyo, hafai kutuamuliwa mkondo wetu wa kisiasa,” akaongeza.

Hata hivyo, mbunge wa Kabuchai Majimbo Kalasinga alimshutumu Bw Waluke akisema alishawishiwa na Rais Uhuru Kenyatta arejee Jubilee ili aidhinishwe kutetea kiti chake cha ubunge licha ya sakata ya ufisadi inayomwandama kortini.

  • Tags

You can share this post!

Raila na Karua kuzoa asilimia 60 ya kura za Mlima Kenya...

Mchujo wazua hofu miongoni mwa wawaniaji

T L