• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
MDG yamsuta Raila kwa kupinga ‘tiba’ ya bungeni

MDG yamsuta Raila kwa kupinga ‘tiba’ ya bungeni

NA CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa chama cha Movement for Democracy and Growth (MDG) David Ochieng’ amepinga vikali pendekezo la kiongozi wa upinzani Raila Odinga kwamba masuala tata yaliyoibuliwa na mrengo wake yashughulikiwe nje ya bunge.

Amesema chama chake, ambacho ni mshirika katika halali katika serikali ya Kenya Kwanza, kinaunga mkono pendekezo la Rais William Ruto kwamba masaula hayo yajadiliwe na kutatuliwe kwa njia ya maelewano kupitia bunge.

“Inashangaza kuona Azimio ikiahidi kurejelea maandamano ikiwa bunge litahusishwa. Hii inaonyesha kuwa Bw Odinga anadharua uongozi wa bunge ambalo ndilo asasi ya kikatiba na lenye uwezo wa kushughulikia masuala yenye umuhimu kwa umma,” Bw Ochieng’, ambaye ni Mbunge wa Ugenya, akasema kwenya taarifa Jumanne, Aprili 4, jioni.

Mapema siku hiyo Bw Odinga alipinga pendekezo la Rais Ruto kwamba masuala yalichangia Azimio kuitisha maandamano yashughulikiwe bungeni.

Akiongea na wanahabari jijini Nairobi, kiongozi huyo wa Azimio alipendekeza kuwa masuala kama vile kupanda kwa gharama ya maisha na mageuzi katika Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka yashughulikiwe kwa kuzingatia mchakato wa Mwafaka wa Kitaifa wa 2008.

“Ni msimamo wetu kwamba masuala yetu yote hayawezi kushughulikiwa bungeni. Masuala  kama gharama ya maisha, ukaguzi wa sava za kupokea matokeo ya uchaguzi wa urais, mabadiliko na uteuzi wa makamishna wa IEBC yanaweza tu kujadilisha nje kisha yawasilishwe bungeni kuidhinishwa. Tunapendekeza mkondo wa Mwafaka wa Kitaifa wa 2008 uliosimamiwa na Koffi Annan,” Bw Odinga akawambia wanahabari katika kituo cha SKM command, mtaani Karen.

Lakini Bw Ochieng’ anasema kwa kutoa pendekezo kama hili, Azimio imeonyesha haina nia ya kutatua changamoto zinazowaathiri Wakenya, wanavyodai, bali wanayo lengo fiche la kuingia serikali “kwa njia haramu na inayokiuka katiba.”

“Ikiwa kweli viongozi wa Azimio wanataka kushiriki mazungumzo, wazingatie ukweli na wakome kuleta masuala yasiyo na umuhimu kwa Wakenya,” akasema.

  • Tags

You can share this post!

Kiunjuri aunga Raila vipengee vya Katiba virekebishwe

Leteni hao Arsenal – Klopp

T L